Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimetoa maagizo matatu kwa Serikali kupitia Wizara ya Kilimo na taasisi zilizoko chini yake, hususan, Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TRFA) yakilenga kuweka mazingira mazuri kwa wakulima nchini kuzalisha zaidi, wanapojiandaa kuanza msimu mwingine wa kilimo, mwaka huu.
Maagizo hayo ya CCM yaliyotolewa na Katibu Mkuu wa Chama hicho, Komredi Daniel Godfrey Chongolo , ni pamoja na Wizara ya Kilimo kuweka na kutangaza utaratibu wa kulipa malipo ya wakulima wa mahindi, hususan wa mikoa ya Kusini, ukiwemo Mkoa wa Rukwa, ambao mazao yao yalinunuliwa na NFRA na hawajamaliza kulipwa.
Agizo jingine ni kuitaka Wizara ya Kilimo kupitia NFRA kutoa fedha za kununua mahindi ya wakulima ambayo bado yako kwenye maghala huku msimu mwingine wa kilimo ukikaribia kuanza, hali inayoweza kuathiri uzalishaji wao.
Ndugu Chongolo pia ameagiza Wizara ya Kilimo, kupitia TRFA kuhakikisha wakulima wanapata mbolea ya ruzuku mapema kabla ya msimu kuanza na waipate katika maeneo ya karibu, tofauti na msimu uliopita ambapo kulikuwa na malalamiko ya wananchi kuwa mbolea hiyo ilichelewa kufika na walilazimika kuifuata umbali mrefu kuipata.
“Kuna suala la malipo ya mahindi…tunaiagiza Wizara ya Kilimo kuwalipa wakulima wa mahindi yaliyonunuliwa na NFRA haraka ili waweze kujiandaa na msimu wa kilimo unaokuja. Lakini pia tunawaagiza Wizara ya Kilimo walete fedha ili NFRA wanunue mahindi ambayo bado yako kwa wakulima.
“Mmemsikia mara kadhaa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan akisisitiza suala la kuhifadhi chakula. Kwa mujibu wa wataalam wetu wa utabiri wa hali ya hewa, kuna dalili za kuwepo kwa El Nino kwenye msimu huu wa mvua, ambayo inaweza kuathiri uzalishaji. Hivyo Serikali lazima iweke mpango wa kununua chakula cha kutosha ili kuwa na uhakika wa chakula,” amesema Chongolo na kuongeza;
“Agizo jingine ni kuhusu mbolea…tunawaagiza wasogeze mbolea karibu ili ipatikane kwa karibu kwa wananchi. Huko nyuma, sehemu kubwa ilishia kupatikana makao makuu ya wilaya. Tunawataka Wizara ya Kilimo wafanyie kazi haya.”