Suala la kuwapatia vyeti vya uraia wa Tanzania kwa Tajnisi wahamiaji wasiohamishika Zanzibar ni mpango wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuwajali wananchi wake kwa kuweka haki na wajibu wa kuishi bila ya ubaguzi wowote.
Akiakhirisha Mkutano wa Kumi na mbili (12) wa Baraza la Kumi (10) la wawakilishi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amesema Serikali ya Awamu ya Nane inayoongozwa na Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi imeandika historia mpya kwa kuwapatia uraia wa Tajnisi jumla ya wahamiaji wasiohamishika 3,319 wanaoishi Zanzibar ni jambo linalodhihirisha mapenzi ya Rais Dkt. Mwinyi kwa wananchi wake kwa kuhakikisha wanapata haki sawa pasi na upendeleo wala ubaguzi.
Amesema Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya ndani ya nchi imefanikiwa kukamilisha suala hilo kwa mashirikiano baina ya Idara ya uhamiaji, Wizara ya nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais na Ofisi ya Rais Ikulu kwa kusimamia maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameeleza kuwa Serikali imedhamiria kukuza uchumi wake kupitia sekta mbali mbali ikiwemo Bandari ambapo imeamua kumkabidhi mwekezaji Kampuni ya Afrika Global Logistics (AGL) kuendesha Bandari ya Malindi kwa lengo la kuongeza ufanisi wa utendaji na uendeshaji wa Bandarini hiyo.
Amewatoa wasi wasi wananchi, wafanyabiashara na wadau wanaotumia Bandari ya Malindi kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na kupokea ushauri kutoka wadau hao ili kusaidia kuleta maendeleo kupitia Sekta ya Bandari.
Aidha Mhe. Hemed ameeleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea na ujenzi wa Barabara kuu na Barabara za ndani kwa mji wa Zanzibar ili kurahisisha huduma za usafiri na usafirishaji bidhaa hivyo, amewaomba wananchi waendelee kuwa wastahamilivu wakati wa ujenzi wa Barabara hizo na kuwataka kutoa mashirikiano kwa kampuni za ujenzi wa miradi hiyo.
Sambamba na hayo amesema Serikali imeamua kuwawekea mazingira mazuri wafanyabiashara wakubwa na wadogo kwa kujenga masoko katika maeneo mbali mbali Unguja na Pemba kama ilivyoelekezwa katika Ibara ya 228 ya Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2020-2025.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameuagiza Uongozi wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ kuwasimamia wajenzi wa masoko hayo kufuata mikataba kwa kujenga majengo bora na yenye viwango na kumaliza kwa wakati kwa mujibu wa Mkataba na kuchukuliwa hatua mkandarasi yoyote asieheshimu Mikataba na kwa watendaji wa Serikali wanaohusika na uzembe kwa kuzorotesha utekelezaji wa miradi hiyo.
Pamoja na hayo Mhe. Hemed amesema Serikali imeamua kujenga Hospital za Mikoa na Wilaya ambazo baadhi zimeshaanza kazi ambapo ametoa wito kwa Wizara ya Afya kuwasimamia wafanyakazi na Madaktari ili kuwahudumia wananchi kwa weledi.
Aidha amesisitiza kuwa Serikali haitosita kumchukulia hatua za kisheria na kinidhamu Mfanyakazi yoyote atakaekwenda kinyume na maadili ya utumishi wa umma.
Akimalizia Hotuba yake Mhe. Hemed amewataka wananchi kusafisha mitaro na maeneo yanayowazunguka na kwa wanaoishi mabondeni wachukuwe tahadhari mapema za kuhama katika maeneo hatarishi katika kipindi hichi cha Mvua za alninyo zinazotabiriwa kuwa kubwa ili kujilinda na maafa yasiyo na lazima.
Imetolewa na Kitengo cha Habari (OMPR)
04/10/2023