Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi ameanza ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo kuelekea shamra shamra za miaka mitatu ya Serikali ya awamu ya nane madarakani ambapo amefungua hospitali ya Kivunge baadae aliweka jiwe la msingi katika ujenzi unaoendelea wa Skuli ya ghorofa Donge Mkoa wa Kaskazini Unguja leo tarehe 23 Oktoba ,2023.
Rais Dk.Mwinyi amesema Serikali imekuja na utaratibu mpya wa kushirikisha sekta binafsi katika kutoa huduma kwa hospitali za Serikali ikiwemo maabara, utoaji wa dawa, huduma za Xray na Ultra sound, chakula pamoja na usafi lengo ni kutoa huduma bora za kisasa na za haraka kwa wananchi.
Rais Dk.Mwinyi amesema hayo leo wakati akifungua rasmi Hospitali ya wilaya ya Kivunge, Wilaya ya Kaskazini "A" Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Vilevile Rais Dk.Mwinyi amewahakikishia wananchi Serikali itaendelea kujenga Skuli za Msingi na Sekondari za Ghorofa kwa pesa ya Serikali, ujenzi wa barabara, miradi ya maji na miradi ya maendeleo yote kwa pesa za Serikali.
Rais Dk.Mwinyi amesema wapigaji makelele wachache ni wale wabadhirifu na mafisadi ambao mirija yao imezibwa kwa sasa Serikali malengo yake fedha zinakwenda kwenye miradi ya huduma za kijamii, mishahara ya wafanyakazi wa Serikali, pensheni kwa wastaafu na jamii.
🗓️23 Oktoba 2023