Home » » MANENO YA NAIBU WAZIRI PINDA YATAKA KUMLIZA DIWANI WA KISAKI SINGIDA

MANENO YA NAIBU WAZIRI PINDA YATAKA KUMLIZA DIWANI WA KISAKI SINGIDA

Written By CCMdijitali on Tuesday, December 12, 2023 | December 12, 2023

 

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kisaki mkoani Singida alipokwenda kutafuta suluhu ya mgogoro wa ardhi baina ya wananchi na mwekezaji tarehe 11 Desemba 2023.



 

Na Munir Shemweta, WANMM SINGIDA

 

Maneno ya Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe Geophrey Pinda wakati wa kutafuta suluhu ya mgogoro wa ardhi kati ya wananchi wa Kisaki na Mwekezaji wa Sekta ya Nyuki katika eneo la Kisaki B Manispaa ya Singida mkoani Singida nusra yamlize Diwani wa Kata ya Kisaki Moses Shaban kutokana na kujaa hekima na busara.

 

Naibu Waziri Pinda alifika kijiji cha Kisaki kilichopo mpakani mwa manispaa ya Singida na na wilaya ya Ikungi mkoani Singida tarehe 11 Desemba 2023 kwa lengo la kusikiliza na kutatua mgogoro wa ardhi baina ya Wananchi na Mwekezaji wa Nyuki.

 

"Nikupongeze sana Mhe Naibu Waziri naweza kusema hata kama hutujafika mwisho wa jambo hili, umenipa hadidu za rejea kumkumbuka Mizengo Pinda alipokuwa waziri mkuu hekima yake na maelekezo yake juu ya utendaji kazi". Alisema Shaban

 

"Nilikuwa nimesimama na kukusikiliza natamani kulia kwa sababu umekuja katika mgogoro huu hakika umeiwakilisha vyema serikali ". Alisema


 

Diwani huyo wa Kata ya Kisaki amesema, maneno yaliyozungumzwa na Naibu Waziri Mhe Geophrey Pinda kuhusu utatuzi wa mgogoro baina ya wananchi na Mwekezaji ni tunu yenye afya na mbolea katika kutatua mgogoro wa ardhi katika eneo hilo.

 

"Umeongoza kikao kilaini na kitamu hata aliyekuwa na hasira zimepotea na hata yule aliyekuwa na silaha ameshusha nakupongeza sana". Aliongeza Diwani Shaban


 

Kwa upande wake, Naibu waziri wa ardhi Geophrey Pinda aliwataka wananchi wa kisaki katika manispaa ya Singida mkoa wa Singida kuhakikisha wanadumisha amani katika muda wote wa kushughulikia migogoro ya ardhi kwenye maeneo yao.

 

"Niwatangazie kipande cha amani wote bila kujali ukoo wa nani na muwe na lugha moja iliyo bora. Siri ya mgongano inapata adui anayeingia bila matatizo"alisema mhe. Pinda.


 

Amewataka wananchi wa kijiji cha Kisaki kwenda kuanza vikao vya suluhu ya mgogoro wao na suala la kukutana na serikali basi ofisi ya mkuu wa wilaya ya Singida italisimamia kwa kuwa suala hilo lishatoka katika ngazi ya kijiji.

 

Awali mkuu wa wilaya ya Singida Mhandisi Paskasi Muragili alieleza kuwa Mgogoro wa ardhi baina ya wananchi wa kijiji cha Kisaki na Mwekezaji wa Sekta ya Nyuki katika eneo la Kisaki B ulifika ofisini kwake mwaka 2022 ambapo wananchi walidai maeneo kutwaliwa  Mwekezaji.

 

Hata hivyo, mkuu huyo wa wilaya ya Singida alisema, kufuatia kadhia hiyo aliunda Tume ili kubaini  kama madai ni ya kweli au la ambapo Tume  ilimalia kazi mei 2023 na kupeleka mrejesho katika ofisi yake oktoba 2023.
Mkuu wa wilaya ya Singida Mhandisi Paskasi Muragili akizungumza katika kutatufa suluhu ya mgogoro wa ardhi baina ya wananchi wa kijiji cha Kisaki na mwekezaji wa sekta ya Nyuki tarehe 11 Desemba 2023.

Sehemu ya wananchi wa kijiji cha Kisaki mkoani Singida wakimsikiliza Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda (hayupo pichani) alipokwenda kutatufa suluhu ya mgogoro wa ardhi tarehe 11 Desemba 2023.

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda akikatiza eneo la hifadhi ya msitu wa Mwekezaji wa Sekta Nyuki alipokwenda kutatufa suluhu ya mgogoro wa ardhi baina ya wananchi na mwekezaji katika kijiji cha Kisaki Singida tarehe 11 Desemba 2023.

 

Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link