NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.
Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar Dkt.Mohamed Said Dimwa,amesema Serikali inakopa fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo ya Wananchi wote na sio kwa maslahi ya watu wachache.
Hayo ameyasema katika mwendelezo wa ziara yake wakati akizungumza na wanachama wa katika Tawi la CCM Mafufuni Jimbo la Bumbwini Wilaya ya Kaskazini "B" Kichama Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Dkt.Dimwa, alisema kauli za baadhi ya wanasiasa wa vyama vya upinzani kuilaumu Serikali juu ya masuala ya mikopo ya fedha kutoka kwa wadau wa maendeleo inatakiwa kupuuzwa kwani fedha hizo ni kwa ajili ya kuimarisha miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya barabara za lami,maji safi na salama,ujenzi wa Skuli za kisasa,hospitali,viwanja vya ndege vya kisasa pamoja na bandari za kisasa.
Alifafanua kuwa katika bajeti ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 2024/2025 iliyopitishwa hivi karibuni, zaidi ya asilimia 63 ya fedha za bajeti hiyo zimeelekezwa katika uimarishaji wa miradi ya maendeleo kwa ajili ya kukabili changamoto za wananchi wote wa mijini na vijijini.
"suala la kukopa fedha kwa ajili ya maendeleo sio la Zanzibar tu wala Jamhuri ya Muungano wa Tanzania bali nchi mbalimbali duniani zinakopa na kwa mujibu wa takwimu kutoka shirika la fedha duniani (IMF) nchi zilizoendelea kiuchumi mfano marekani,urusi,ufaransa na zingine ndio zenye madeni makubwa hivyo hao wanasiasa nawashauri wajiongeze kwa kufanya utafti wa kujua mwenendo wa uchumi wa dunia unaendaje.
Wito wangu kwenu tuendeleeni kuwaombea dua njema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan pamoja na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Mwinyi Mwenyezi Mungu awajaalie nguvu,busara na imani ili nchi iendelee kupiga hatua kubwa za kimaendeleo katika nyanja kiuchumi na kijamii",alisema Dkt.Dimwa.
Katika maelezo yake Dkt.Dimwa, aliwataka Wanachama wa CCM na Jumuiya zake kwa ngazi za Mashina na Matawi kufanya vikao vya mara kwa mara ili kujadili masuala ya maendeleo,changamoto na mikakati ya pamoja ya kuimarisha taasisi hiyo.
Naibu Katibu Mkuu huyo Dkt.Dimwa, aliwasihi Viongozi,Watendaji na wanachama kwa ujumla kuhamasisha wananchi na wafuasi wa Vyama vya upinzani kujiunga na Chama ili kuongeza idadi ya wapiga kura wa Chama Cha Mapinduzi.
Mapema Dkt.Dimwa akizungumza na wanachama,viongozi na watendaji wa Chama na Jumuiya zake baada ya kuwasili katika Mkoa huo,aliwapongeza kwa kazi kubwa ya kusimamia kikamilifu utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM mwaka 2020-2025 ndani ya Mkoa huo.
Naye Katibu wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Organazesheni CCM Zanzibar Omar Ibrahim Kilupi, aliwasisitiza Wanachama hao kuhakikisha wanapata kadi za kupiga kura ili wawe na uhalali wa kukipigia kura nyingi Chama Cha Mapinduzi.
Alitoa shukrani Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM ya Mkoa huo, Haji Juma Hajialiahidi kuwa wamejipanga vizuri kuhakikisha CCM inapata ushindi mkubwa wa majimbo yote ya Mkoa huo katika Uchaguzi Mkuu ujao.