Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe Hemed Suleiman Abdulla amesema ujenzi wa kituo cha Karakana ya Uchongaji kilichopo Mwera PONGWE ni hatua muhimu ya utekelezaji wa miradi jumuishi ya elimu itakayowawezesha vijana walio nje ya mfumo rasmi wa elimu kupata ujuzi utakaowasaidia katika maisha yao.
Ameyasema hayo katika hafla ya Uzinduzi wa kituo cha ujuzi kwa vijana cha utekelezaji wa mpango changmani wa kuwawezesha vijana rika wenye umri wa miaka 15- 19 iliyofanyika katika viwanja vya skuli ya Mwera Pongwe, Wilaya ya Kati Unguja.
Amesema utekelezaji wa mradi huo unatoa fursa kwa vijana kujifunza kwa vitendo na kuweza kuwa mafundi mahiri wa kuchonga aina mbali mbali za samani pamoja na kupatiwa ujuzi wa kutengeneza vifaa vya aluminium ili kuwajengea uwezo zaidi katika kukabiliana na harakati za kimaisha.
Mhe. Hemed amesema kituo hicho pamoja na kutoa ujuzi kwa vijana pia kitatoa msaada mkubwa wa kufanya ukarabati wa vifaa mbali mbali kama vile meza, viti na madawati yatakayo haribika katika Maskuli sambamba na kuwataka walimu wakuu kuitumia fursa hio kwa kwa kufanya marekebisho ya samani zilizoharibika katika maskuli yao ili ziendelee kutumika kwa muda mrefu.
Aidha Mhe. Makamu wa Pili wa Rais amesema kuwa Bajeti ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali imeongezwa na kufikia Bilioni 830 lengo ikiwa ni kuiwezesha wizara hio kufikia mageuzi ya elimu ya juu na kuimarisha miundombinu ya elimu kwa kujenga madarasa 1500 ilj kufikia azma ya Serikali ya kuingia mkondo mmoja wa asubihi kwa idadi ya wanafunzk 45 kwa kila darasa.
Sambamba na hayo amesema katika kuimarisha mafunzo ya Ufundi na Amali Serikali imejipanga kujenga vituo viatano vya Mafunzo ya amali vitakavyojengwa Unguja na Pemba pamoja na kujenga vituo vya ujuzi bunifu katika skuli 33 za Sekondari kwa Unguja na Pemba ambapo kwa sasa zitajengwa katika skuli tatu (3 ) kila Wilaya lengo ikiwa ni kuwatayarisha vijana kupata ujuzi ambao utawasaidia katika kujiajiri baada ya kumaliza masomo yao.
Mhe. Hemed amewashukuru washirika wa maendelo Serikali ya Canada na Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto Duniani (UNICEF) Kwa kufadhili mradi huu wenye lengo la kuwasaidia vijana kupata ujizi utakaowadaidia katika kupata ajira na kujikwamua kiuchumi.
Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesisitiza suala la kutunza Amani iliyopo ndani ya nchi na kuvitaka vyombo husika kutumia zaidi busara wakati wa kudhibiti vitendo vya uvunjifu wa amani kwa bila ya amani hakuna maendeleo nchini.
Kwa upande wake Kaimu Waziri wa elimu Zanzibar Ali Abulghulam Hussein amesema Serikali ya Awamu ya Nane(8) imeazimia kufanya mabadiliko makubwa katika Sekta ya Elimu kwa kusomesha Mafunzo ya Amali na ubunifu kuanzia ngazi ya msingi hadi vyuoni.
Amesema Wizara itahakikisha wanafunzi wanaomaliza katika vyuo hivyo wanapata ujuzi ambao utawasaidia katika kujiajiri na kuajiriwa katika mashirika na Taasisi mbali mbali ndani na nje ya nchi sambamba na kujenga vituo vya elimu amali kila wilaya kwa unguja na pemba.
Akitoka maelezo ya Kitaalamu kuhusu program ya ZIPOSA Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Khamis Abdulla Said amesema uwepo wa mradi huo utawasezesha watoto wa kike na kiume katika kumaliza elimu yao ya lazima ambayo waliikosa kutokana na chamgoto mabali mbali za kimaisha.
Amesema kuwa jumla ya vijana 150 wapo katika vituo vya elimu mbadala Unguja na Pemba wakijifunza fani mbali mbali za ufundi pamoja na kujiongezea ujuzi na maarifa unaoendana na soko la ajira nchini.
Mapema Mwakilishi Mkaazi kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto Duniani UNICEF nchini Tanzania Bibi Elke Wisch ameipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuendelea kuboresha Sekta ya Elimu nchini na kutoa kipaombele kwa vijana hasa wale walioacha skuli kwa sababu mbali mbali na kuhakikisha wanawarudisha skuli na kuendelea na masomo yao.
Imetolewa na kitengo cha Habari (OMPR)
Tarehe 15.06.2024
..................................................................................
|
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe Hemed Suleiman Abdulla akikata utepe kuashiria Uzinduzi wa kituo cha ujuzi kwa vijana kilichopo Mwera Pongwe Wilaya ya Kati Unguja. |
|
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe Hemed Suleiman Abdulla akiweka jiwe la zinduzi wa kituo cha ujuzi kwa vijana kilichopo Mwera Pongwe Wilaya ya Kati Unguja. |