Home » » MAKAMU WA PILI WA RAIS ZANZIBAR- KUFUNGA KONGAMANO MKOKOTONI - KWA NIABA YA RAIS WA ZANZIBAR

MAKAMU WA PILI WA RAIS ZANZIBAR- KUFUNGA KONGAMANO MKOKOTONI - KWA NIABA YA RAIS WA ZANZIBAR

Written By CCMdijitali on Sunday, June 2, 2024 | June 02, 2024

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dkt Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kushirikiana na Jumuiya ya wasioona Zanzibar (ZANAB) na Jumuiya nyengine za watu wenye ulemavu ili kuhakikisha inaweka mazingira wezeshi ambayo yatawasaidia watu wenye ulemavu kufaidika na fursa mbali mbali nchini.

Ameyasema hayo katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla wakati wa kuahirisha maadhimisho ya kuongeza uwelewa kwa jamii juu ya watu wenye Ulemavu katika Viwanja vya Mpira wa Mto wa Pwani Wilaya ya Kaskazini 'A' Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Amesema kwa kutambua kuwa watu wenye ulemavu wamekuwa wakikumbana na chamgamoto mbali mbali katika jamii, kumeanzishwa Baraza la Taifa la watu wenye ulemavu na mabaraza ya Wilaya ya watu wenye Ulemavu yenye dhamana ya kusimamia , kutekeleza, kutetea na kulinda haki nafursa za watu wenye Ulemavu ambapo jumla ya shilingi za Kitanzania Bilioni 1.2 zimetenga kwa mwaka wq fedha 2024-2025 kwa ajili ya kuendeshea mabaraza hayo.

Rais Dkt Mwinyi amesema Serikali imeweza kutoa nafasi za Uongozi kwa watu wenye ulemavu katika Wizara mbali mbali ambapo wamekuwa wakitekeleza majukumu kwa ufanisi mkubwa jambo ambalo linazidi kutoa hamasa lwa Serikali kuendelea kuweka mazingira mazuri kwa watu wenye ulemavu ili kuwawezesha kufikia katika ndoto zao walizojipangia.

Dkt. Mwinyi amesema Serikali itahakikisha sheria ya watu wenye Ulemavu inafanyiwa kazi na kupelekwa Baraza la Wawakilishi kwa ajili ya kujadiliwa na hatimae kupitishwa kuwa Sheria kamili ambayo itatoa miongozo mbali mbali kwa Taasisi na Jumuiya za watu wenye ulemavu ili kuwawezesha kufanikisha malengo yao walkyojipangia.

Rais Dkt Mwinyi amesema kupitia Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2020-2025 Serikali imekuwa ikichukua hatua za kuweka mazingira bora kwa watu wenye ulemavu ikiwemo kutunga Sheria ya watu wenye Ulemavu Namba (8) ya mwaka 2022 kwa lengo la kulinda na kutetea haki na fursa za watu wenye ulemavu.

Aidha Rais wa Zanzibar na mwenyekiti wa baraza la mapinduzi Amesema Serikali kupitia Wizara ya Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais itaandaa program maalum itakayowajengea uwelewa wananchi juu ya kutambua haki na wajibu wa watu wenye ulemavu katika Mikoa yote ya Zanzibar.

Sambamba na hayo Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi ametoa wito kwa Jumuiya za watu wenye Ulemavu kuongeza nguvu zaid ya uwajibikaji na kuwahamasisha watu wenye ulemavu kuchangamkia fursa mbali mbali zinazojitokeza katika Taifa.

Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Mhe. Dkt KHALID SALUM MUHAMMED amesema Serikali zote mbili zimefanya mapitio ya Sera na Sheria kuhakikisha watu wote wanapata haki sawa ikiwa ni pamoja na makundi maalum katika nyanja zote za kiuchumi na kijamii.

Dkt Khalid amefahamisha kuwa Serikali kupitia Mfuko wa uwezeshaji imejipanga kumaliza kilio cha muda mrefu cha watu wenye ulemavu kwa kuwapatia mikopo itakayowasaidia kujiendeleza kiuchumi katika miradi yao pamoja na kujikimu kimaisha.

Akisoma Risala iliyoandaliwa na Jumuiya ya watu wasioona Zanzibar Ndugu AWENA HASSAN SEIF amesema (ZANAB) inaiomba Serikali kuongeza uwelewa kwa jamii katika kushirikiana na watu wenye ulemavu katika kutambua haki na ustawi wao katika mambo mbali mbali ya kijamii.

Amesema kuwa changamoto kubwa inayowakabili watu wenye ulemavu ni kutokufikishwa katika Baraza la Wawakilishi sheria ya Hati miliki ya Zanzibar kwa ajili ya kufanyiwa marekebisho ili iendane na Mkataba wa Markesh ambayo itatoa fursa kwa watu wasioona kupata nyaraka za maandishi kwa mfumo sikivu.

Mapema Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja RASHID HADID RASHID amesema jamii inapaswa kutambua kuwa watu wenye ulemavu wanaweza kuleta maendeleo katika jamii, hivyo tunapaswa kuwashirikisha na kuwapa kipaombele katika kushiriki mambo  mbali mbali ya kimaendeleo.

 

Hadid amesema Serikali ya Mkoa wa Kaskazini Unguja imekuwa ikifanya kazi kwa karibu na watu wenye ulemavu kwa kuwashirikisha katika mambo muhimu ya kimaendeleo ili kutoa mchango wao katika mambo yanayowahusu.

 

Imetolewa na Kitengo cha Habari (OMPR)

Tarehe  02.06.2024







Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link