Home » » MAMA MARIAM MWINYI ASHIRIKI HAFLA YA UGAWAJI WA TAULO ZA KIKE KWA WANAFUNZI WASICHANA

MAMA MARIAM MWINYI ASHIRIKI HAFLA YA UGAWAJI WA TAULO ZA KIKE KWA WANAFUNZI WASICHANA

Written By CCMdijitali on Sunday, June 16, 2024 | June 16, 2024

Published from Blogger Prime Android App

MICHEWENI, PEMBA

16  Juni, 2024

MKE wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Mama Mariam Mwinyi amesema suala kumkomboa msichana wa Zanzibar linahitaji ushiriki wa taasisi zote za umaa na binafsi pamoja na jamii kwa jumla wakiwemo wazazi na walezi.

Alisema, wasichana wana haki ya kupata fursa sawa ya elimu kama wavulana kwani nao ni walezi wa familia na jamii kwa ujimla. 

Mama Mariam Mwinyi ambae pia ni Msarifu na Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya “Zanzibar Maisha Bora Foundation” (ZMBF), aliyasema hayo viwanja vya Shamata, Shehiya ya Majenzi, Wilaya ya Micheweni, Mkoa wa Kaskazini, Pemba, kwenye hafla ya ugawaji wa taulo za kike kwa wanafunzi wa kike wa Skuli ya Sekondari ya Micheweni kwaajili ya hedhi salama.

Pia Mama Mariam ameisifu Taasisi ya “Lady Fatma ya Korea ya Kusini kwa kuungamkono jitihada na malengo ya mradi wa “Tumaini Initiative” wa “Zanzibar Maisha Bora Foundation” ya kumkomboa mtoto wa kike wa Zanzibar kwa kutengeneza taulo za kike 1500 na kila moja zikiwemo tano ndani yake.

Alisema, taulo hizo zimewakomba wasichana wengi kupata haki yao ya elimu kwa kuondoa hofu iliyowatafuna muda mrefu walipokuwa kwenye ada zao za kila mwezi.

Mama Mariam Mwinyi, alisema, zoezi la ugawaji wa taulo hizo kwa wasichana wa Zanzibar ni endelevu wa kuwafikia wasichana wote nchi nzima ili kuondosha changamooto inayowakumba wengi wanaoshindwa kuhudhuria masomo yao wakiwa kwenye ada zao za mwezi.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Mhe. Ali Abdul Gulam Hussein aliipongeza Taasisi ya “Zanzibar Maisha Bora Foundation” kwa jitihada zake za kuisaidia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia ushiriki wake wa kuendelea kumkomboa mtoto wa kike wa kizanzibarika kwenye hifadhi ya hedhi salama.

Pia alisema, taasisi hiyo inaungamkono juhudi za Serikali kupitia kampeni yake ya kumrejesha mtoto wa kike skuli ambayo inashirikiana na Qatar na Shirika la kimataifa la UNICEF pia kusaidia kupunguza utoro kwa wanafunzi.

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Mhe. Salama Mbarouk Khatibu pia aliipongeza taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation kwa jitihada zake na kuendelea kutoa huduma bora za jamii ikiwemo elimu na afya hasa kwa watu wa mkoa huo.

Alisema, hivi karibuni taasisi hiyo imewafikia Wanakaskazini Pemba   20303 baada ya kuweka kambi ya matibabu bure Mkoani humo ambapo Wananchi 9,099 walipata matibabu.

Kwa upande wake, Mratibu wa Taasisi ya “Zanzibar Maisha Bora Foundation”, Gulam Abdul Karim, alisema lengo  la mradi wa “Tumaini Initiative” wa taasisi hiyo ni kutatua changamoto za hedhi kwa wanafunzi wote wa kike wa Zanzibar.

Taasisi ya “Zanzibar Maisha Bora Foundation” (ZMBF) iliasisiwa Julai mwaka 2022 na kuzinduliwa rasmi Febuari mwaka 2023. Mnamo Mwezi Machi mwaka jana ZMBF ilizindua Mpango Mkakati wake wa miaka mitatu na mradi wa “Tumaini kit” ambao hadi sasa umefanikiwa kuzalisha taulo za kike zaidi ya 5000 na kuzisambaza kwa wanafunzi na wasichana  zaidi ya1500 wa skuli za msingi na sekondari kwa Unguja na Pemba.

Aidha, taasisi hiyo inafanya kazi kwa karibu na tasisi za Serikali zikiwemo Mahakama ya Zanzibar, Wizara ya Afya, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Wizara ya Uchumi wa Buluu, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee Wazee na watoto, Wizara ya Habari na Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda.


IDARA YA MAWASILIANO IKULU, ZANZIBAR.


Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link