Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Ndugu. Hemed Suleiman Abdulla amesema kufanyika kwa makongamano ya kitaaluma ndani ya chama ni uimarishaji wa chama na kuunga mkono jitihada za viongozi wa Chama na Serikali katika kutekeleza majukumu yao ya kuwaletea maendeleo wananchi wake.
Ameyasema hayo wakati Akifungua Kongamano la Vijana la kuonesha mafanikio, fursa na maendeleo ndani ya miaka mitatu ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais Dkt Hussen Ali Mwinyi lililofanyika katika Ukumbi wa Umoja ni Nguvu Mkoani Pemba.
Mhe. Hemed amesema Jeshi la CCM ni Vijana ambao wanahitaji kupewa taaluma na kuelimishwa juu ya kazi mbali mbali zinazofanywa na Chama na Serikali ili nao wakawe mabalozi wazuri wa kuyatangaza mazuri yanayofanywa na viongozi wa nchi.
Mhe. Hemed ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewataka Viongozi wa chama na Serikali kuungana na kufanya kazi ya kukitumikia chama cha Mapinduzi kwa pamoja, kutangaza fursa kwa vijana zinazopatikana ndani ya Chama na Serikalini jambo ambalo litaendelea kuipa heshima CCM ya kuongoza Nchi awamu kwa awamu.
Sambamba na hayo Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa amekemea tabia ya baadhi wa wanachama kuanza kutangaza nia ya kugombea nafasi mbali mbali wakijua muda muafaka wa kugombea haujafika hivyo amewataka wanachama kushirikiana na viongozi waliopo madarakani katika kutekeleza majukumu yao ya kuwatumikia wananchi .
Aidha Mhe Hemed amemuagiza mwenyekiti wa UVCCM Taifa kuwachukulia hatua za nidhamu wale wote ambao wanaenda kinyume na Katiba na sheria za chama jambo ambalo linakiletea sifa mbaya chama cha mapinduzi na jumuiya zake, pamoja na kusisitiza kuwa Serikali iko tayari kutoa kila aina ya msaada ili kuhakikisha malengo ya vijana yanatimia hasa katika kukipigania chama cha Mapinduzi.
Nae Mwenyekiti wa UVCCM Taifa Ndugu Mohammed Ali Kawaida amesema kufanyika kwa kongamano hilo kutatoa fursa kwa vijana wa Mikoa miwili ya Pemba ya kuona fursa zilizomo ndani ya Chama Cha Mapinduzi na kutambua namna ya kuzifikia fursa hizo kwa maslahi yao binafsi na taifa kwa ujumla.
Kawaida amesema Serikali zote mbili zimetenga fedha nyingi kwa ajili ya kuwawezesha vijana hasa wa CCM ili kuhakikisha wanawekeza katika shuhuli mbali mbali za kimaendelo zitakazowakwamua kiuchumi.
Mapema Mbunge wa Vijana Mkoa wa kusini Pemba Mhe. Munira Mohammed Mustafa ambae pia ndie muandaaji wa Kongamano hilo amesema lengo la kuandaa kongamano hilo ni kuwaweka pamoja vijana wa CCM wa mikoa miwili ya Pemba ili kupatiwa mafunzo yatakayowasaidi kuzitambua fursa na namna ya kuzitumia fursa hizo zinazotolewa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mhe. Munira amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetenga zaidi ya Bilioni 16 kwa ajili ya vijana kujiendeleza kiuchumi, pamoja na kujenga vyuo vya mafunzo ya amali katika wilaya za Zanzibar ambavyo vinatoa fursa kwa vijana kujiendeleza kiufundi na kupata ujuzi utakaowasaidi kupiga hatua kimaendeleo.