Home » » Dk. MWINYI NA GAVANA BENKI KUU

Dk. MWINYI NA GAVANA BENKI KUU

Written By CCMdijitali on Thursday, December 19, 2024 | December 19, 2024

 ZANZIBAR,

19 DISEMBA, 2024

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema kushuka kwa thamani ya dola nchini ni faraja kubwa kwa Uchumi kwani kutapunguza ugumu wa gharama za maisha kwa wananchi.

Dk. Mwinyi ameyasema hayo Ikulu, Zanzibar alipozungumza na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Emmanuel Tutuba pamoja na ujumbe alioongozana nao waliofika kumtembelea.

Rais Dk. Mwinyi amesema, ni mategemeo yake kushuka kwa dola kutasaidia pia kupungua gharama za baadhi ya mahitaji kwenye maisha ikiwemo kupungua bei kwa bidhaa muhimu ikiwemo chakula na mafuta.

Alibainisha kuwa bidhaa zote zilizoathirika kutokana na kupanda kwa dola duniani ni matarajio yake kwamba zitarejea kwenye uhalisia wake.

Akizungumzia suala la uingizwaji wa bidhaa nyingi na athari za kupanda kwa dola,Rais Dk. Mwinyi alieeleza kwamba iliathiri sana Uchumi wa nchi licha ya kuwa baadhi ya bidhaa zinazozalishwa nchini zilifidia hasara hasa wakati wa mavuno akitolea mfano bidhaa za chakula ikiwemo mchele kwa kiasi ilipunguza kasi ya uagiziaji kutoka nje.

Wakati huo huo, Rais Dk. Mwinyi ameipongeza Benki Kuu ya Tanzania kwa weledi wa kuendelea kuwahamasisha wananchi juu ya kubadilisha noti za zamani zinazoondoshwa kwenye mzunguko kwa matumizi yao ya kila siku.

Aliahidi kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendeleza ushirikiano na benki hiyo ili kushajihisha jamii na kuwajengea uelewa wananchi wa kubadili noti za zamani ili kusaidia kuondoka kwenye mzunguko kwa wakati.

Naye, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Emmanuel Tutuba amemueleza Rais Dk.Mwinyi kwamba benki hiyo inaendeleza zoezi la kuondoa kwenye mzunguko noti za zamani za shilingi 20, 200, 500, 1000, 2000, 5000 na 10,000 kwa matoleo ya mwaka 1985 hadi 2003.

Amesema Benki hiyo pia imetoa muda maalumu kwa Watanzania kuanzia Januari 2025 hadi Aprili 2025 kuutumia muda huo kwa zoezi la kubadilisha noti za zamani kupitia Ofisi zote za benki kuu ya Tanzania na benki zote za biashara kwa kupatiwa malipo yenye thamani sawasawa na kiasi kinachobadilishwa.

Aidha, Gavana Tutuba alieleza matumizi ya noti hizo yatafikia ukomo wa kuwa fedha halali za Tanzania ifikapo Aprili o6 mwaka 2025 na kusisitiza kuwa baada ya tarehe hiyo noti hizo hazitatumika kwa matumizi yoyote popote duniani.

Pia, Gavana Tutuba ametoa rai kwa wananchi wenye noti za zamani kuzibadilisha au kuziweka amana kwenye benki yoyote ndani ya kipindi kilichowekwa.

Akizungumzia kuhusu kushuka kwa thamani ya dola nchini, Gavana Tutuba amesema ni hatua moja ya benki hiyo kuipandisha thamani na kuirejesha kwenye mzungungo wa soko, fedha ya ndani ambayo kwa kipindi kirefu ilishuka, hivyo ametoa indhari kwa wafanyabishara wote nchini pamoja na kuwajuulisha Watanzania kwamba ni marufuku kwa mfanyabiashara yeyote kuuza ama kununua bidhaa kwa kutumia dola ama fedha yoyote ya kigeni.

Amesema, kufanya hivyo ni kulitangaza na kulipandisha thamani soko la nje na kuua la ndani suala ambalo halikubaliki kisheria kwa mujibu wa sera na kanuni za soko na Uchumi wa nchi.

Hivyo, Gavana Tutuba aliwashauri wafanyabiashara kote nchini wakiwemo wamiliki wa mahoteli na sekta nyengine za utalii na uwekezaji kuwashajihisha wateja wao kuendelea kufanya malipo kwa kutumia thamani ya fedha za ndani akiwashauri pia kuweka mazingira ya kubadilisha fedha za kigeni kwenye sehemu zao za biashara ili wageni waendelee kutumia thamani ya fedha ya ndani.

Pia, alieleza matarajio yake kwa wafanyabiashara kupunguza bei ya bidhaa zao kutokana na kushuka kwa thamani ya dola akizisihi mamlaka za Serikali kuingilia kati ili kuwasaidia wananchi kupunguza mzigo wa gharama za maisha.





IDARA YA MAWASILIANO, IKULU ZANZIBAR.

Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link