Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imefanikisha maboresho makubwa katika miundombinu ya Bandari ya Mtwara, jambo ambalo limeongeza ufanisi katika sekta ya uchukuzi na kukuza uchumi wa ukanda wa kusini.
Maboresho hayo yamepelekea kupungua kwa vikwazo vya usafirishaji na kusaidia kuondoa changamoto zilizokuwa zikiikumba bandari hiyo.
Kwa sasa, zaidi ya tani 100,000 za korosho zimeweza kusafirishwa kupitia bandari ya Mtwara, ikichangiwa na ongezeko la vifaa vya kupakia na kushusha mizigo, hatua ambayo imewezesha meli nyingi zaidi kuanza kutia nanga katika bandari hiyo, hivyo kuchochea uchumi wa mkoa wa Mtwara na maeneo jirani.
Waziri wa Uchukuzi, Mhe. Profesa Makame Mbarawa, ameeleza hayo Leo Tarehe 19 Desemba 2024 alipozungumza na waandishi wa habari akiwa mkoani Mtwara wakati wa ziara ya kukagua maendeleo na maboresho ya bandari hiyo.
Ameeleza kuwa maboresho haya ni sehemu ya mkakati wa serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wa kukuza uchumi, kuongeza fursa za ajira, na kuboresha sekta ya uchukuzi.
“Leo hii kuna meli mbili kubwa ambazo zipo katika bandari hii, moja ikiwa na uwezo wa kubeba tani 9,000 na nyingine tani 30,000, aidha, kesho kutakuwa na meli nyingine tatu zitakazokuwa zikifanya kazi kwa wakati mmoja. Vitendea kazi vimeongezeka na tunatarajia kupata mitambo mingine kutoka bandari ya Dar es Salaam ili kuimarisha huduma zaidi,” alisema Prof. Mbarawa.
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Patrick Sawala, alimpongeza Waziri Mbarawa kwa kutafsiri kwa vitendo maono ya Rais Dk. Samia kufungua uchumi wa mikoa ya kusini kupitia bandari.
Aidha Maboresho hayo yanatarajiwa kufungua milango zaidi kwa wawekezaji na kukuza biashara za kimataifa, huku wananchi wa mkoa wa Mtwara wakinufaika na fursa za ajira zinazojitokeza katika sekta ya uchukuzi na usafirishaji.