ZANZIBAR,
05 DISEMBA, 2024
MKE wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Mama Mariam Mwinyi ameizindua bodi na ofisi mpya ya taasisi anayoingoza ya “Zanzibar Maisha Bora Foundation” (ZMBF).
Uzinduzi wa bodi na ofisi hiyo umefanyika Kilimani Mnara wa mbao Mkoa wa Mjini Magharibi ambako kwasasa ndio itakua ofisi itakayoratibu na kutekeleza shuguli zote za ZMBF nchini.
Aidha, uzinduzi wa bodi mpya ya “Zanzibar Maisha Bora Foundation” umekuja baada ya kumaliza muda wake bodi ya zamani ambayo Mama Mariam Mwinyi ameisifu kwa kazi kubwa waliyoifanya kwa ZMBF na jitihada waliyoweka hadi kuifanikisha taasisi hiyo kujivunia mafanikio makubwa iliyonayo sasa.
Mama Mariam Mwinyi ambae pia ni Msarifu na Mwenyekiti wa Bodi ya wadhamini ya ZMBF ameeleza kazi ya Bodi hizo ni kusimamia, kushauri na kuiwekea malengo na kuujengea upeo pamoja na kuuongoza uongozi wa taasisi hiyo katika kuhakikisha inafanikisha malengo yake iliyojiwekea na kusimamia mpango mkakati wa taasisi hiyo.
Hivyo, aliiomba bodi iliyomalizika kuendea kuisemea vizuri ZMBF, kuikumbuka kwa fursa mbalimbali na kuendelea kuiungamkono kwa hali zote.
“Niwaombe sana muendee kutusemea kwa mazuri yetu, ZMBF kuendelea kupokea fursa, ushauri kwa kila hali, kutokana na ushirikiano mzuri uliojengeka baina yetu” alisisitiza Mama Mariam.
Kuhusu bodi mpya ya taasisi hivyo, Mama Mariam ameitakia na kutegemea mazuri zaidi kama yaliyofanywa na bodi iliyopita, na kuisifia ZMBF ilipotoka hadi sasa ipo vizuri.
Pia, Mama Mariam Mwinyi, aliishukuru taasisi ya “Benjamin Mkapa Foundation” kwa msaada mkuwa walioutoa kwa “Zanzibar Maisha Bora Foundation” amesema taasisi hiyo imekua dada wa ZMBF kwa kila hatua ya mafanikio iliyopiga.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Makamo Mwenyekiti mstaafu wa bodi iliyomaliza muda wake kwa taasisi hiyo, Mama Asha Bilali ametoa shukurani zake za dhati kwa ushirikiano mkubwa alioupata wakati wakiisimamia ZMBF hadi kuifanikisha ilivyosasa akisifia kazi nzuri iliyofanywa na bodi hiyo, huku akiitarajia zaidi ZMBF kufika mbali zaidi kwa mafanikio.
Naye, Mkurugenzi na Mtendaji Mkuu wa “Zanzibar Maisha Bora Foundation”, Fatma Fungo, amesema taasisi hiyo imetimiza miaka minne ya usajili wake na miaka mitatu ya utendaji wake akisifia mafanikio makubwa waliyoyafikia kwa juhudi ya bodi inayomaliza muda wake, hivyo ameeleza matarajio yake kwa bodi mpya wanayoendelea nayo akiwa na matarajio zaidi ya kusongambele kwa mafanikio makubwa zaidi.
Kwa upande wake mjumbe wa bodi mpya ya ZMBF, Dk. Josephine Kimaro ameeleza matarajio ya bodi mpya kwa taasisi hiyo huku akiahidi mafanikio zaidi kiutendaji kwa kasi yenye ufanisi wa hali ya juu.
Bodi mpya ya “Zanzibar Maisha Bora Foundation” iliyozinduliwa rasmi itafanyakazi kwa mwaka 2024/2025 hadi 2026/2027.
Taasisi ya “Zanzibar Maisha Bora Foundation” iliasisiwa Julai mwaka 2021 na kuzinduliwa rasmi Febuari mwaka 2022. Aidha taasisi hiyo inafanya kazi kwa karibu na tasisi za Serikali zikiwemo Mahakama ya Zanzibar, Wizara ya Afya, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Wizara ya Uchumi wa Buluu, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee Wazee na watoto, Wizara ya Habari na Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda.