Home » » TANZANIA IMEJIZATITI KUENDELEZA USHIRIKIANO WA KIKANDA NA USTAWI WA PAMOJA - MAKAMU WA RAIS

TANZANIA IMEJIZATITI KUENDELEZA USHIRIKIANO WA KIKANDA NA USTAWI WA PAMOJA - MAKAMU WA RAIS

Written By CCMdijitali on Friday, December 6, 2024 | December 06, 2024

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema Tanzania inaendelea kufanya mashauriano ndani ya Serikali ili kuona namna itakavyoweza kushiriki katika uendelezaji wa Ushoroba wa Lobito kwa kuzingatia vipaumbe vya kitaifa, makubaliano baina yake na mataifa mengine pamoja na makubaliano ya kikanda. 

Makamu wa Rais amesema hayo wakati alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Angola, Marekani, Kongo na Zambia kuhusu Ushoroba wa Lobito (Lobito Corridor), ambapo Tanzania ni mgeni mwalikwa katika Mkutano huo uliyofanyika katika Mji wa Lobito nchini Angola. 

Amesema Tanzania inauzoefu wa kuunganisha mataifa mengine kwani tayari inaziunganisha nchi za Afrika ya Kati zisizo na bahari na Mataifa ya Mashariki ya kati, Bara la Asia na Mashariki ya mbali. Ameongeza kuwa reli ya TAZARA na Bomba la Mafuta la TAZAMA vimeimarisha ushirikiano, ustawi wa pamoja tangu miaka ya 1970. 

Makamu wa Rais amesema kupitia Protokali ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ya Mawasiliano, Usafiri na Hali ya hewa, Tanzania tayari imeunganika na Mataifa jirani na eneo kubwa zaidi la ukanda wa SADC, na hivyo kuimarisha usafirishaji wa watu, bidhaa na fursa mbalimbali. 

Ameongeza kwamba kupitia reli ya TAZARA inaruhusu treni kusafiri kutoka nchini Tanzania hadi baadhi ya nchi za SADC kama vile Zambia, Zimbabwe na Afrika Kusini. 

Makamu wa Rais amesema Tanzania imejizatiti kuendeleza ushirikiano wa kikanda na ustawi wa pamoja. 

Amepongeza hatua iliyofikiwa katika uendelezaji wa Ukanda wa Lobito ambapo amesema kupitia ushirikiano na ubunifu huo Ajenda ya Afrika 2063 itafikiwa. Ushoroba wa Lobito unahusisha ujenzi wa reli itakayounganisha Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Zambia hadi Angola kwa lengo la kuunganisha bahari ya Atlantiki na Bahari ya Hindi.

 Mkutano huo umehudhuriwa na Rais wa Jamhuri ya Angola Mhe. João Lourenço , Rais wa Marekani Mhe. Joe Biden, Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Mhe. Félix Antoine Tshisekedi na Rais wa Zambia Mhe.Hakainde Hichilema.































Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link