Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Waziri wa Nishati Dkt. Doto Biteko amewataka wataalamu wa manunuzi na Ugavi kufanya tathimini binafsi ya utendaji wao ili kujua endapo wamefanikiwa kufikia malengo ya kuanzishwa kwa taaluma hiyo ya Ugavi na manunuzi.
Mapema leo Jumanne Disemba 17, 2024 wakati akifungua Jukwaa la 15 la wataalam hao Jijini Arusha kwenye Kituo cha Kimataifa cha Mikutano AICC, Dkt. Biteko amewataka wataalam hao pia kutopuuza sauti za watu wanaosema kuhusu taaluma yao na badala yake wazibebe kauli hizo na kuzifanyia kazi.
"Mtasikia wengine wanalaumu wanasema taaluma yenu imekuwa ikiongeza urasimu zaidi badala ya kurahisisha kazi, Imeongeza mazingira ya watu kupendeleana, Mtasikia kuwa unapotaka kununua jambo kwa kufuata utaratibu wa manunuzi gharama yake itaongezeka kuliko kununua kitu moja kwa moja, mtasikia.Wengine wanasema ili uweze kufanikiwa lazima uwe rafiki wa Afisa manunuzi, mtazisikia." Amesema Dkt. Biteko.
Naibu Waziri Mkuu amesisitiza umuhimu wa taaluma hiyo kwenye maendeleo akisema ili kupunguza umaskini wa watanzania kupitia rasilimali kidogo walizonazo ni muhimu kwa Maafisa hao kujitambua na kutimiza majukumu yao kikamilifu pamoja na kusimamiana kikamilifu na kukataa vitendo vya rushwa kwenye manunuzi na ugavi.