Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Alhajj Hemed Suleiman Abdulla amesema hatua ya kuwashirikisha watoto katika harakati mbali mbali za dini ya kiislamu ikiwemo mashindano ya kuhifadhi Qur-an ni njia sahihi inayochangia kuwakuza watoto kimaadili na kiroho pamoja na tabia njema.
Ameyasema hayo katika uzinduzi wa Mashindano ya Kuhifadhi Qur-an Afrika uliyofanyika katika Ukumbi wa Hotel ya Madinat Al Bahr Mbweni jijini Zanzibar.
Alhajj Hemed amesema kuwa mashindano ya Kuhifadhi Qur-an yanawajenga watoto kuwa na tabia njema zenye kumtii Mwenyezi Mungu na kuifahamu vyema dini yao sambamba na kuwaepusha kujiingiza katika vitendo viovu ukiwemo Wizi, Ujambazi, Ubakaji na Matumizi ya madawa ya kulevya.
Amesema jamii inapaswa kufahamu kuwa jukumu la kuhimiza na kusimamia maadili mema ni wajibu wa kila mmoja na kwa nafasi yake kuhakikisha suala la maadili linapewa kipaombele ili vijana waweze kuishi katika miongozo mema ya dini ya kiislamu na kuepuka kufuata mila, silka na desturi za kigeni zinazokwenda kinyume na maamrisho Allah ( S.W )
Alhajj Hemed amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inatambua na kuthamini mchango mkubwa unaotolewa na Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) kwa kushirikiana na Afisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar katika kuijenga jamii yenye maadili mema na kuahidi Serikali itaendelea kuunga Mkono juhudi hizo kwa kutoa kila aina ya ushirikiano utakaohitajika ili kuendeleza dini ya Kiislam na kuimarisha maadili mema nchini.
Sambamba na hayo Mhe. Hemed amesema Zanzibar imeweza kupiga hatua kubwa ya kimaendeleo katika sekta mbali mbali kutokana na kuwepo kwa amani na mshikamano hivyo ametoa wito kwa wananchi kuzidi kuitunza amani na umoja uliopo nchini pamoja na kuwataka Mashekhe, maimamu, wahadhiri, viongozi wa dini na viongozi wa vyama vya kisiasa kuwataka wafuasi wao kudumisha amani na mshikamano hasa katika kupindi hiki cha kuelekea uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) ambao ndio waandaaji wa Mashindano hayo Bwana RAMADHAN ATHUMANI BUKINI amesema lengo la kamati ya Mashindano ya kuhifadhi Qur-an ni kuona mashindano hayo yanakuwa makubwa na kushirikisha nchi zote duniani kwa na lengo la kuwaandaa vijana kiroho na kiimani katika kuiisimamisha dini ya kiislamu.
Bukini amesema mashindano hayo ya kuhifadhi Qur-an Afrika yanayotarajiwa kufanyika mwezi Machi 2025 na kushirikisha nchi tisa(9) ikiwemo Afrika Kusini, Nigeria, Senegal, Komoro, Kenya, Algeria, Kongo, Tanzania Bara na Wenyeji Zanzibar yatasaidia kuwaendeleza vijana katika kukihifadhi na kukisoma kwa weledi kitabu kitakatifu cha Qur-an .
Amesema hamasa ya Mashindano hayo imekuwa ni kubwa jambo ambalo limepelekea nchi mbali mbali duniani kuwa na utayari wa kushiriki katika mashindano hayo na kuahidi kila mwaka kuongeza idadi ya nchi washiriki pale ambapo hali ya udhamini itaimarika zaidi.
Akitoa salamu za Afisi ya Mufti Mkuu Zanzibar katika uzinduzi wa Mashindano hayo Katibu Mtendaji Ofisi ya Mufti Mkuu Zanzibar Sheikh Khalid Ali Mfaume amewataka waislamu kuekeza katika mambo ya kheri na kuwa tayari kujitoa kwa Elimu zao, Mali zao pamoja na nguvu zao katika kuilingania na kuisimamisha dini ya Kiislamu.
Sheikh Mfaume amesema ni wajibu wa Kila muislamu kwa nafasi yake kuunga mkono mashindano hayo kwa kuyatangaza ili yaweze kutambulika ulimwenguni kote na waislamu kupata fursa ya kushiriki kwa wingi katika mashindano hayo.
Imetolewa na Kitengo cha Habari ( OMPR )
Leo tarehe…25 / 01 / 2025.