Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Japan zimetia Saini Hati za Mkataba wa Yen za Japan bilioni 22.742 sawa na takribani shilingi bilioni 354.45 za kitanzania kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa Uendelezaji wa kilimo vijijini unaojulikana kama “Agriculture and Rural Development Two Step Loan Project”.
Mkataba huo umetiwa saini Jijini Dar es Salaam kati ya Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), na Makamu wa Rais wa Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA), Bi. Miyazaki Katsura na kushuhudiwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Japan, Mhe. Fujii Hisayuki, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Cosato Chumi, Balozi wa Japan nchini anayemaliza muda wake, Mhe. Yasushi Misawa, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bi. Jenifa Omolo, na viongozi wengine waandamizi wa Serikali.
Akizungumza baada ya kusaini Hati hizo za Mikataba ya mkopo huo wenye masharti nafuu, Dkt. Nchemba alisema kuwa, utekelezaji wa mradi huo utachochea ukuaji wa sekta ya kilimo kwa kuongeza uzalishaji kwa wakulima kupitia upatikanaji wa mitaji nafuu na pia itasaidia utoaji wa mikopo ya muda wa kati na mrefu kwa wakulima, vikundi vya uzalishaji, na taasisi zinazojihusisha na kilimo kwa kuziwezesha kuwekeza katika kilimo cha kisasa, kupata pembejeo bora na teknolojia ya juu ya kilimo.
Aliongeza kuwa Upatikanaji wa mitaji ya kilimo kupitia mradi huo utawawezesha pia wakulima kulima mazao mchanganyiko, na kuwa na kilimo kinachostahimili mabadiliko ya tabia nchi, ambako kutachangia usalama wa chakula, maendeleo vijijini na uimara wa uchumi kwa ujumla.
“Mradi huu unaendana na Mpango wetu wa Maendeleo wa Miaka Mitano ambao una maudhui ya kufikia ushindani na Uchumi wa viwanda kwa maendeleo ya watu ili kuongeza tija na uzalishaji kwa kutumia rasilimali zilizopo na pia unaendana na Mpango wa Pili wa Maendeleo ya Sekta ya Kilimo ambao unalenga kuimarisha na kuchochea matumizi ya zana za kisasa za kilimo, usalama wa chakula na lishe, kuwezesha upatikanaji wa masoko, na kuwezesha uongezaji wa thamani” alisema Dkt. Nchemba.
Aidha Dkt. Nchemba, alisema kuwa Tanzania imenufaika na ufadhili wa Japan kwa miaka zaidi ya 60 hasa kwenye sekta za kilimo, maji, Afya, Nishati, usafirishaji na elimu kupitia kujengewa uwezo kupitia mashirika makubwa ya kimataifa ambako Serikali ya Japan inachangia kwa ajili ya miradi mingine ya kijamii na kiuchumi.
“Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatambua na kushukuru kwa ufadhili ambao umekuwa ukitolewa na Serikali ya Japan ambao hutekelezwa na JICA, Uhusiano huu wa muda mrefu umechangia kwa kiasi kikubwa katika kuchochea ukuaji endelevu wa uchumi na kuboresha maisha ya Watanzania” alisema Dkt. Nchemba.
Kwa upande wake Makamu wa Rais wa Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA), Bi. Miyazaki Katsura, alisema kuwa Mradi huo unalenga kuboresha uzalishaji wa kilimo na mapato ya wakulima katika mnyororo wa thamani wa mazao manne yaliyopewa kipaumbele katika Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano wa Serikali ya Tanzania, (FYDP III), ambayo ni Mpunga, Mahindi, Ngano, na Alizeti, na kuimarisha usalama wa chakula nchini.
Bi. Katsura aliongeza kuwa, JICA imekuwa ikiweka kipaumbele katika Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (FYDP III) pamoja na Mpango wa Maendeleo ya Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDP2) katika shughuli zake na itaendelea kushirikiana na Tanzania ili kuendana na Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2025.