Songea, Ruvuma
Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mkoa wa Ruvuma kwa mwaka wa fedha 2024/2025 umeidhinishiwa Shilingi bilioni 38.394 kwaajili ya kufanya matengenezo na ujenzi wa barabara zenye urefu wa kilomita 1145, madaraja madogo 50 na makalavati 57.
Kati ya fedha hizo Sh.bilioni 7.8 bajeti ya barabara kuu, Sh.bilioni 9.8 zinatokana na tozo ya mafuta, Sh.bilioni 4.5 fedha kutoka mfuko wa Jimbo na Sh.bilioni 16.2 ni fedha za mradi wa Agri-connect chini ya Umoja wa Ulaya(EU).
Hayo yamesemwa na Meneja wa TARURA wa Ruvuma, Mhandisi Silvester Chinengo wakati akitambulisha barabara mpya ya Muungano-Majengo na barabara ya Kilimo Mseto-Pm House zenye urefu wa Km 1.5 kwa gharama ya Sh.milioni 949 pamoja na barabara ya Mjimwema-Mkuzo yenye urefu wa Km 1.1 kwa gharama ya Sh.milioni 426.
“Barabara hizi zimejengwa kutokana na fedha za tozo ya mafuta na zimeleta mabadiliko makubwa kwenye mitaa kwa sababu wakati wa mvua wananchi waliathirika na mafuriko pamoja na matope, kwa sasa ni msaada mkubwa kwa wakazi wa mitaa hiyo na mali zao, pia zitarahisisha sana shughuli za usafiri na usafirishaji kwa wananchi”.
TARURA mkoa wa Ruvuma inahudumia mtandao wa barabara wenye jumla ya Km. 71,146.21,madaraja 306, makalavati 531, drifti 14 na mitaro yenye urefu wa Km. 6.91 ambapo Km. 2312 ni za mjazio, Km. 3873.85 ni za mkusanyo, Km. 959.52 ni za jamii, Km. 128.66 ni lami na zege, Km. 1429 ni changarawe na Km. 5588 ni udongo.
Aidha, aliongeza kuwa, Serikali imetenga Sh.bilioni 2.28 kwaajili ya kuondoa vikwazo barabarani chini ya mradi wa RISE ikiwemo kujenga madaraja na barabara za changarawe katika Halmashauri ya Madaba, Mbinga Mji, Halmashauri ya wilaya Mbinga, Nyasa, Namtumbo na Tunduru.
Denis Timoth mkazi wa mtaa wa Matogoro, ameipongeza Serikali kwa kuendelea kutekeleza miradi mingi ya barabara ili kuwaondolea wananchi kero ya kusafiri wanapotoka eneo moja kwenda lingine kwaajili ya shughuli zao za kiuchumi.
Agnes Komba mkazi wa mtaa wa Makambi alisema, ujenzi wa barabara za lami umewasaidia wananchi kujikomboa na umaskini na kuimarika kwa uchumi wa mtu mmoja mmoja kwani hivi sasa mitaa na maeneo mengi hakuna adha ya usafiri na usafirishaji.