Home » » MAKAMU WA PILI WA RAIS ZANZIBAR AFUNGUA KONGAMANO,WARSHA NA MKUTANO WA 51 WA CHAMA CHA WAKUTUBII

MAKAMU WA PILI WA RAIS ZANZIBAR AFUNGUA KONGAMANO,WARSHA NA MKUTANO WA 51 WA CHAMA CHA WAKUTUBII

Written By CCMdijitali on Monday, February 10, 2025 | February 10, 2025

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amesema Serikali zote mbili  zinatambua mchango mkubwa unaotokana  na wanataaluma ya Ukutubi ambayo inachangia kwa kiasi kikubwa  maendeleo kwa Taasisi za Serikali na Taasisi binafsi hapa nchini.


Ameyasema hayo kwa  niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dkt Hussein Mwinyi wakati wa  ufunguzi wa Kongamano na  Warsha inayoenda sambamba na Mkutano Mkuu wa 51 wa Chama cha Wakutubi Tanzania uliofanyika katika Ukumbi wa Hotel ya Golden Tulip Uwanja wa Ndege jijini Zanzibar.

Amesema kuwa kujifunza kupitia  huduma za maktaba za kidijitali itakuwa chachu ya kuwarahisishia wananchi kupata taarifa na habari sahihi kwa wakati sambamba na kujiongezea uwezo wa kukabiliana na changamoto mbali mbali zinazojitokeza kwa mtu mmoja mmoja na jamii kwa  ujumla.

Makamu wa Pili wa Rais amesema ni wajibu wa wakutubi na watoa huduma za Maktaba kuwekeza katika elimu na ubunifu ili kubaini vyanzo mbali mbali vya taarifa na maarifa vilivyopo kwa ajili ya kuboresha huduma za maktaba katika mfumo wa kidijitali.

Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar amesema Serikali inaendelea na azma yake ya kujenga Mktaba kuu ya kisasa katika eneo la Maisara ambayo itakidhi viwango vya kitaifa na  Kimataifa ikiwemo huduma za kidijitali pamoja na kujenga Maktaba kwa kila Wilaya ambazo zitafungamana na utoaji wa huduma za kisasa kwa jamii husika.

Sambamba na hayo MakAmu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewataka wakutubi kusimamia malengo ya Chama chao kwa kuwaunganisha wanataaluma ya ukutubi katika kukuza ushirikiano wa Taasisi wanachama katika utoaji wa huduma za maktaba na kuboresha viwango vya huduma hio  kwa Tanzania nzima.

Mhe. Hemed amesema anatambua kuwa Sera ya Taifa ya Maktaba ipo katika hatua za mwisho hivyo amewaagiza  Wakuu wa Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania (BOHUMAZA) kushirikiana na vyama wa wakutubi katika kuandaa miongozo mbali mbali ambayo itarahisisha utekelezaji wa Sera hiyo na kuleta mabadiliko chanya kwa tasnia ukutubi, huduma za maktaba na wakutubi wenyewe.

Nae Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Ndugu Khamis Abdulla Said amesema kongamano hilo na warsha kwa wana taaluma ya Ukutubi litaleta mabadiliko makubwa hasa  katika upatikanaji wa taarifa za usahihi, na zenye ufanisi na kuwafikia walengwa kwa wakati.

Khamis amesema Serikali kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar imetenga bajeti maalum kwa ajili ya ununuzi wa vitabu vyote muhimu vya kusomea na kufundishia kwa ajili ya kuboresha huduma za maktaba ili kuweza kuakisi mahitaji ya watumiaji.

Amesema Wizara ya Elimu imejipanga kuimarisha Mifumo ya kidijitali katika Maktaba zote za Zanzibar ambao utawezesha kuongeza ufanisi wa huduma za maktaba na kupunguza changamoto ya upotevu wa vitabu pamoja na kuwapatia fursa za mafunzo ndani na nje ya nchi wanataaluma ya ukutubi ili kuendana na mabadiliko ya Teknolojia na ongezeko la  mahitaji ya huduma za Maktaba nchini.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania Profesa Ali Mcharazo amesema wakati umefika kwa Wakutubi kuwezeshwa kielimu na kupatiwa vifaa  vya kisasa ili kuweza kufanya kazi zao kwa uweledi na ubora wa hali ya juu katika kutoa huduma za Maktaba nchini.

Profesa Mcharazo amesema wakutubi wana wajibu wa kujiendeleza kitaaluma na  kujifunza ubunifu katika kada yao kwa kuzingatia kuwa Elimu bora hutegemea vifaa bora na wataalamu bora wa kuisambaza elimu hio.

Mapema  Mkurugenzi wa Bodi ya Huduma za Maktaba Zanzibar Dkt. Ulfat Abdulaziz Ibrahim amesema Bodi ya Huduma za Maktaba Zanzibar imejipanga kufanya Mapinduzi ya Kifikra juu ya maana, matumizi na umuhimu wa Maktaba na wakutubi katika kufikia malengo ya elimu Tanzania.

Dkt. Ulfat amesema kufanyika kwa Kongamano na Warsha kwa Wakutubi wa Tanzania litasaidia kuongeza ujuzi na taaluma kwa watatoa huduma hio kuweza  kutoa taaluma bora kwa watumiaji wa Maktaba popote walipo nchini.


Imetolewa na Kitengo cha Habari ( OMPR )
Leo tarehe  10. 02. 2025

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akipokea maelezo kutoka kwa Mkuu wa Divisheni ya Huduma za Maktaba kutoka Bodi ya Huduma za Maktaba Zanzibar Ndugu Ramadhan  Said Yussuf wakati akikagua kazi mbali mbali zinazofanywa na Wakutubi Tanzania kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na  Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dkt Hussen Mwinyi katika Ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip Uwanja wa Ndege Zanzibar.


Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link