WAKILI MKUU WA SERIKALI ATOA WITO WA MATUMIZI YA MIFUMO YA KIDIJITALI KWA AJILI YA UFUATILIAJI WA MIGOGORO NA UIMARISHAJI WA HAKI
Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Ally Possi ametoa wito kwa
taasisi zote za kisheria na wadau wa haki nchini kutumia mifumo ya kidijitali
kupata takwimu sahihi zitakazowawezesha kufuatilia migogoro yote
waliyoisikiliza ili kuhakikisha inamalizika kwa mafanikio.
Dkt. Possi ametoa wito huo tarehe 01 Februari, 2025
alipotembelea mabanda ya maonesho ya taasisi mbali mbali nchini zinazoshiriki
Maadhimisho ya Wiki ya Sheria nchini yanayoendelea kwenye viwanja vya Nyerere
Square vilivyopo jijini Dodoma. Dkt. Possi ameeleza kuwa matumizi ya mifumo ya kisasa
yatasaidia kuboresha usimamizi wa haki na kuongeza uwajibikaji katika utatuzi
wa migogoro ya kisheria kwa kuwa kwa kiasi kikubwa itawezesha kutoa takwimu
sahihi na kwa haraka pale taasisi husika itakapohitaji kufahamu mwenendo wa
mgogoro husika ulioshughulikiwa.
Akizungumza na watumishi wa Wizara ya Katiba na Sheria, Dkt. Possi amesisitiza kuwa mifumo ya kidijitali ina uwezo mkubwa wa kuboresha utendaji kazi wa taasisi za kisheria kwa kuwezesha upatikanaji wa taarifa kwa wakati hatua itakayosaidia kuhakikisha migogoro yote inayoshughulikiwa kwenye kliniki za sheria inamalizika ili wananchi waweze kufanya shughuli zao za kukuza uchumi kwa amani. “Kwa kutumia mifumo ya kisasa, tunaweza kufuatilia mwenendo wa migogoro yote kwa urahisi ili kuhakikisha migogoro yote inasimamiwa kwa weledi na kupunguza ucheleweshaji wa haki ili wananchi waendelee na shughuli zao za kujiletea maendeleo wao binafsi na taifa kwa ujumla,” alisema Dkt. Possi.
Alibainisha kuwa matumizi sahihi ya mifumo hiyo yatasaidia
kuondoa changamoto zinazoikabili Sekta ya Sheria nchini katika kushughulikia migogoro
ikiwa ni pamoja na kupotea kwa nyaraka muhimu ambazo zimechangia ucheleweshaji
wa maamuzi huku akisisitiza taasisi zinazohusika na usimamizi wa sheria
kushirikiana katika kuunda na kutekeleza mifumo ya ki dijitali inayolenga
kuboresha uwajibikaji na uwazi.
Dkt. Possi alieleza kuwa mifumo hii itaiwezesha Serikali
kupata takwimu sahihi kuhusu migogoro inayoshughulikiwa, muda wa utatuzi wa
migogoro husika na kiwango cha mafanikio ya migogoro inayosimamiwa na
kumalizika kwa mafanikio makubwa hatua hii itatimiza azma ya Serikali ya Awamu
ya Sita chini ya Uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia
Suluhu Hassan kuhakikisha tunajenga jamii imara isiyo na migogoro kwa
kuhakikisha wananchi wanaishi kwa amani ili waweze kuendelea na shughuli zao za
kujiletea maendeleo.
Akizungumzia namna Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali
inavyochangia kukuza pato la taifa, Dkt. Possi amesema kuwa Ofisi ya Wakili
Mkuu wa Serikali imehakikisha wakati wote kuwa rasilimali za nchi zinalindwa
ikiwemo miradi mikubwa ya maendeleo kama vile bwawa la kufua umeme la Mwalimu Nyerere,
mradi wa bomba la mafuta kutoka Hoima Uganda hadi Chongoleani mkoani Tanga,
ujenzi wa madaraja makubwa ya Tanzanite na Kigongo Busisi Feri linalojengwa
Jijini Mwanza ambayo miradi hii imekuwa chachu ya maendeleo katika kujenga na
kukuza uchumi wa nchi.
“Miradi inalindwa kwa kuhakikisha kuwa utekelezaji wake hauathiriwi wala kukwama kutokana na migogoro na pale inapotokea changamoto Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali inasimama kuhakikisha kuwa mradi hausimami,haukwami au kushindwa kutekelezwa kutokana na migogoro na Ofisi yetu imekuwa inashughulika kwa njia moja au nyingine katika uendelezaji wa miradi na kuhakikisha kuwa migogoro haiwi chanzo cha kuzuia utekelezaji wa miradi mbali mbali nchini”, amesisitiza Dkt. Possi.
Ameongeza kuwa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali imeendelea kuzishauri taasisi za Serikali ipasavyo pamoja na kumaliza mashauri nje ya Mahakama hatua ambayo imesaidia kupunguza migogoro na kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi. Naye Afisa Mchunguzi Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria ndugu Laurent Bulilo amesema kuwa wamekuwa na kawaida ya kufuatilia migogoro na mashauri yote kupitia Mfumo wa Mama “Samia Legal Aid Campaign System” hatua ambayo imesaidia kwa kiasi kupunguza migogoro kwenye jamii.
Dkt. Possi ameonyesha jinsi Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali inavyochangia kukuza pato la taifa kupitia usimamizi wa mali za umma, mikataba ya kimataifa na uimarishaji wa mazingira ya biashara. Pia, ameahidi kuendelea kushirikiana na wadau wote wa sheria hasa wadau wa haki madai katika matumizi ya TEHAMA ili kuhakikisha mifumo inasomana ili kuongeza ufanisi katika uendeshaji wa mashauri ya Serikali.
![]() |
Msajili wa Mahakama ya Tanzania, Bi. Eva Nkya akimkabidhi
cheti cha ushiriki wa Maadhimisho ya Wiki ya Sheria, Wakili wa Serikali wa
Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, ndugu Salehe Manoro wakati wa maadhimisho
hayo yanayoendelea Jijini Dodoma. |
![]() |
Wakili Mkuu wa Serikali Dkt. Ally Possi akiwa na watumishi
wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kwenye banda la Ofisi hiyo alipotembelea
Maadhimisho ya Wiki ya Sheria yanayoendelea Jijijni Dodoma. |