Na Munir Shemweta, WANMM IRINGA
Serikali imewataka watendaji wa sekta ya Ardhi nchini kutochelewesha huduma za sekta ya Ardhi kwa makusudi wakati wanapowahudumia wananchi wanaokwenda kupata huduma katika ofisi zao.
Hayo yameelezwa Januari 31, 2025 mkoani Iringa na Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bw. Hamdouny Mansoor wakati wa kikao kazi cha watumishi wa sekta ya Ardhi Mkoa wa Iringa.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Mhandisi Anthony Sanga, Bw. Mansoor amesema kumekuwa na ucheleweshaji huduma kwa makusudi na wakati mwingine watendaji wa sekta ya Ardhi kuwatuma mwananchi wanaokwenda kupata huduma.
"Sasa anakuja mwananchi anasema anataka kulipa kodi anaelezwa, aah hiyo kazi ni ya Afisa Ardhi nenda kulee mimi mpima, si umuelekeze tu, wakati mwingine tunatoa kauli ambazo siyo nzuri kwa wananchi wanaofika kupata huduma za Ardhi kwenye ofisi zetu" amesema.
Aidha, Mansoor kupitia kikao hicho kilichoandaliwa na Ofisi ya Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Iringa ametaka kuwekwa utaratibu rasmi katika ofisi zote za Ardhi kuanzia ngazi ya wilaya wa namna ya kupata hati ili wananchi wauelewe na kuufuata utaratibu huo.
"Inasisitizwa ili upate hati ni vitu gani vya msingi vinatakiwa viwepo kwa wananchi kupata hati yake, viainishwe na vibandikwe katika ofisi zetu za ardhi" amesema.
Kwa upande wake Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Iringa Bw. Frank Minzikuntwe ameeleza kuwa, kikao kilichofanyika cha watumishi kilikuwa na lengo la kuzungumza na kupeana mikakati pamoja na mipango kazi ya namna ya kushughulikia kero na utoaji huduma za sekta ya ardhi kwa haraka zaidi.
"Sisi kama watendaji wa sekta ya Ardhi katika mkoa wa Iringa tunaahidi watumishi wote katika ngazi ya mkoa tutafanya kazi kwa weledi na uaminifu na kuwahudumia wananchi kwa tija ili waweze kupata huduma kwa wakati unaostahili’’. amesema
Kikao hicho cha siku moja kimeshirikisha watendaji wa sekta ya ardhi kutoka halmashauri zote za mkoa wa Iringa pamoja na wale wa Ofisi ya Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Iringa.
Sehemu ya watumishi wa sekta ya ardhi mkoa wa Iringa wakifuatilia majadiliano wakati wa kikao kazi cha watumishi wote wa sekta ya ardhi mkoa wa Iringa kilichofanyika jana. |
Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Iringa Bw. Frank Minzikuntwe akizungumza katika kikao kazi cha watumishi wa sekta ya ardhi mkoa wa Iringa jana. (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI) |
Sehemu ya watumishi wa sekta ya ardhi mkoa wa Iringa wakifuatilia majadiliano wakati wa kikao kazi cha watumishi wote wa sekta ya ardhi mkoa wa Iringa kilichofanyika jana. |