Home » » Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aipongeza Mamlaka ya Mapato ZANZIBAR

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aipongeza Mamlaka ya Mapato ZANZIBAR

Written By CCMdijitali on Saturday, March 1, 2025 | March 01, 2025

 

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla ameipongeza Mamlaka ya Mapato Tanzania Ofisi ya Zanzibar (TRA) kwa kufanikiwa katika ukusanyaji wa Mapato Nchini.
 

Ameyasema hayo katika hafla ya maadhimisho ya siku ya Mlipa Kodi iliyofanyika katika Ukumbi wa Zanzibar Beach Resort Mazizini Zanzibar. 

Mhe. Hemed amesema mafanikio yaliyofikiwa katika ukusanyaji wa mapato umetokana na mashirikiano yaliyopo Baina ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA) kwa kuwaweka karibu wafanyabiashara hali ambayo imepelekea wafanyabiashara hao kuwa wepesi katika suala la ulipaji wa Kodi. 

Aidha amesema TRA Ofisi ya Zanzibar imefikia mafanikio ya kuvuka malengo ya ukusanyaji wa kodi waliyopangiwa kutokana na ushirikiano mzuri  baina yao na walipa kodi ikiwa ni njia muhimu ya kuunga mkono juhudi za Serikali za kuwaletea maendeleo Wananchi wake. 

Amesema juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi zimechangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa mapato na kuchochea Kasi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa Miundombinu na utoaji wa huduma Bora kwa jamii. 

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameutaka Uongozi wa TRA Zanzibar kuzidisha juhudi katika kusimamia ukusanyaji wa mapato na kuongeza wigo wa walipakodi kwa kusimamia vizuri mifumo mbali mbali ya ukusanyaji wa mapato, kusisitiza maadili ya watendaji, kupambana na rushwa na kutoa huduma bora kwa walipa kodi. 

Mhe.Hemed amewahimiza watendaji wa TRA Zanzibar kuendelea kutoa elimu ya mlipa kodi ili kila mtu ajue faida ya kodi katika kutekeleza miradi ya maendeleo ikiwa ni pamoja na kuiwezesha Serikali kutoa huduma za kijamii kama vile maji safi na salama, afya,elimu, nishati ya umeme na nyenginezo. 

Aidha Mhe. Hemed amewahakikishia kuwa Serikali zote mbili zinatambua na kuthamini mchango mkubwa wa wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla ambao ndio wanaoiwezesha Serikali kutekeleza shughuli mbali mbali za maendeleo pamoja na kutoa huduma za kijamii. 

Sambamba na hayo amewahakikishia kuwa mapato yote yatokanayo na kodi yatatumika ipasavyo katika kuwaletea maendeleo wananchi na kuendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wafanyabiashara wakubwa , wa kati na wadogo, pamoja na wawekezaji kwa ili kupunguza gharama za uwajibikaji na kuleta wepesi katika ulipaji wa kodi, kuongeza mapato, kukuza ajira na kuondoa umasikini Nchini. 

Amewataka wananchi wote kuendelea kulipa kodi na kudai risiti kila wanapopata huduma na watoa huduma wahakikishe wanatoa risiti kila wanapotoa huduma na kusisitiza kuwa Serikali haitamfumbia macho mtu yoyote atakaekwepa kulipa kodi na hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake ili kukomesha vitendo hivyo visiendelee. 

Nae Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Zanzibar Mhe. Dkt. Saada Mkuya Salum amesema Serikali kupitia Mamlaka za Mapato zinajipanga kuweka mazingira mazuri, wezeshi na rahisi kwa wafanyabiashara na walipa kodi nchini ili kuendelea kuwajenga kuwa na utayari wa kulipa kodi kwa wakati. 

Amesema jukumu la Serikali ni kuweka Sheria na kanuni Bora zitakazosaidia kuwawezesha walipa Kodi waweze kutimiza wajibu wao wa kulipa Kodi kupitia mifumo madhubuti iliyowekwa na Mamlaka za Mapato Tanzania. 

Kwa upande wake Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania Ndugu Yussuf Juma Mwenda  amewapongeza wafanyabiashara Nchini kwa kuchangia kulipa Kodi kwa hiari hatua iliyopelekea kuwapatia tunzo kutokana na mchango wao Mkubwa katika kufikia malengo ya kukusanya Kodi Nchini. 

Amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa kuweka Mazingira rafiki na wezeshi kwa wafanyabiashara hatua ambayo imepelekea kuongezeka kwa wawekezaji na kutanua wigo wa Kodi Nchini Tanzania. 

Akitoa salamu kwa niaba ya sekta binafsi bwana Suleiman Ali Moh'd kutoka Taasisi ya Uwekezaji ya Utalii(ZATI) amesena Taasisi yake imekuwa ikifanya kazi kwa karibu na TRA Zanzibar hasa katika suala zima la kutoa elimu na kuwaelimisha wawekezaji juu ya umuhimu wa kipa kodi kwa hiari. 

Amesema Taasisi binafsi zianatambua umuhimu wa kulipa kodi kwa maendeleo ya Taifa hivyo, watakuwa mstari wa mbele kuhakikisha wanalipa kodi kwa hiari na ndani ya wakati ili kupata maendeleo endelevu ya Taifa.

Makamu wa Pili wa Rais wa zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akikabidhi zawadi ya Mshindi wa kwanza wa tunzo za walipaji kodi bora mwaka 2023/2024 kwa Wawakilishi wa Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) katika hafla ya siku ya mlipa kodi iliyofanyika Ukumbi wa Zanzibar Beach Resort.






Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link