HOTUBA YA MHESHIMIWA WAZIRI WA AFYA, JENISTA MHAGAMA KWA WAANDISHI WA HABARI WAKATI WA KUMTAMBULISHA PROF.
MOHAMED YAKUB JANABI KAMA MGOMBEA MTEULE WA NAFASI YA UKURUGENZI WA SHIRIKA LA
AFYA DUNIANI (WHO) KANDA YA AFRIKA UTAKAOFANYIKA TAREHE 18 MEI 2025, GENEVA,
USWISI.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya – Dkt. Seif Shekalaghe
Kaimu Mganga Mkuu wa Serikali –
Mshauri wa Rais wa Masuala ya Afya na Lishe na
Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Taifa Muhimbili – Prof. Mohamed Janabi.
Mkurugenzi Huduma za Kinga na Mkurugenzi Mkuu wa
Jumuiya ya Afya ya Afrika Mashariki, Kati na Kusini (ECSA – HC) – Dkt. Ntuli A.
Kapologwe
Wageni Waalikwa mliopo hapa
Ndugu Wanahabari:
Nawasalimu kwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania…
Mnamo tarehe 14 Januari 2025 Shirika la Afya Duniani
Kanda ya Afrika liliitisha kikao maalum na nchi wanachama wake 47 kwa ajili ya
kujadili uchaguzi wa Mkurugenzi wa Shirika hilo kwa Kanda ya Afrika.
Ikumbukwe mnamo mwezi Agosti 2024, Tanzania iliwania
nafasi hii kupitia Marehemu Dkt. Faustine E.Ndugulile aliyekuwa pia alikuwa
Mbunge wa Jimbo la Kigamboni. Dkt. Ndugulile alishinda nafasi hiyo katika
uchaguzi uliofanyika mnamo tarehe 26 Agosti 2024 wakati wa Mkutano wa 74 wa
Shirika la Afya Duniani Kanda ya Afrika uliofanyika Brazaville, Jamhuri ya
Kongo.
Dkt.
Faustine alishinda nafasi hiyo baada ya kuwashinda wagombea wengine watatu
ambao ni Dkt. Socce Fall (Senegal), Dkt. Richard Mihigo (Rwanda) na Dkt.
Boureima Hama Sambo (Niger).
Ndugu
Wanahabari;
Tarehe 27
Novemba 2024, Tanzania na Jumuiya ya
Kimataifa tulipokea kwa mshutko mkubwa taarifa za kifo cha mpendwa wetu Dkt.
Faustine Ndugulile ambaye alifariki kabla ya kuanza kuitumikia nafasi hiyo
Mwezi Februari 2025. Naomba tusimame kwa dakika moja kumuombea Marehemu Dkt.Faustine
Ndugulile apumzike kwa amani.
Ndugu Wanahabari:
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwa ni
miongoni mwa nchi wanachama wa Shirika la Afya Duniani Kanda ya Afya
ilimpendekeza Prof. Mohamed Yakub Janabi, Mshauri wa Rais kwenye Masuala
ya Afya na Lishe ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya
Muhimbili kuwania nafasi ya Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani Kanda ya
Afrika.
Kama mnavyofahamu, Shirika la Afya Duniani ni chombo
yenye mchango mkubwa katika kuboresha mifumo ya afya ulimwenguni. Nafasi hii ya
Ukurugenzi wa Kanda ya Afrika ni muhimu sana kwa sababu inatoa mwelekeo wa
kisera, kisayansi, na kimkakati katika kutatua changamoto za afya
zinazolikabili bara letu, hivyo tunaamini Tanzania kuwa na mwakilishi katika
Shirika hili itaweza kuongeza mchango wake katika maendeleo ya Sekta ya Afya
barani Afrika.
Ndugu Wanahabari;
Prof. Mohamed Janabi ni mtaalamu mwenye uzoefu mkubwa
katika sekta ya afya. Amehudumu katika nyadhifa mbalimbali za uongozi, ikiwa ni
pamoja na kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili ambapo
ameshiriki katika kuleta mageuzi makubwa ya utoaji wa huduma bora za afya na
kuimarisha mifumo ya rufaa kutoka vituo vya kutolea huduma za afya ngazi ya
msingi mpaka Taifa.
Akiwa Mkurugenzi Mtendaji wa kwanza na mwanzilishi wa
Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Janabi aliongoza mageuzi
makubwa katika huduma za matibabu ya moyo nchini Tanzania na Barani Afrika na
hivyo kupekelea kupunguza rufaa za nje ya nchi kwa asilimia 95.
Pamoja na sifa hizo mbili, Prof. Janabi amekuwa
akishiriki kwenye masuala ya utekelezaji wa afua za afya ya jamii kwa kutoa
elimu ya afya na kushiriki kwenye shughuli mbalimbali za uimarishaji huduma za
afya ngazi ya jamii. Prof. Janabi ameshiriki kwenye tafiti mbalimbali
zilizolenga kuboresha utoaji wa huduma za afya pia ni Mhadhiri katika Chuo
Kikuu cha Tiba na Afya Shirikishi Muhimbili (MUHAS) na Mhadhiri wa kualikwa
katika Vyuo mbalimbali Duniani.
Prof. Janabi amefanya kazi kwa ukaribu na
Mashirika ya Kikanda, Kimataifa, Serikali mbalimbali pamoja na Wadau wa Sekta
ya Afya ili kuboresha upatikanaji wa huduma bora na endelevu za afya kwa
wananchi. Uzoefu wake wa kitaaluma na kiutendaji unampa sifa zinazohitajika
kuongoza Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika kwa ufanisi.
Ndugu Wanahabari;
Baadhi ya vigezo vilivyopelekea Prof.Janabi
kugombea nafasi hii ni pamoja na;
v
Uongozi Thabiti,
Prof. Janabi, ameonesha uwezo mkubwa
wa kuleta mageuzi katika Sekta ya afya kupitia uongozi wake kwenye taasisi
alizoziongoza lakini pia kuwa Mshauri Mkuu wa Masuala ya Afya na Lishe kwa
Waheshimiwa Marais wawili (Mhe. Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete na
Mhe. Dkt. Samia Suluh Hassan).
v
Uwezo wa Kitaalamu,
Prof. Janabi kupitia tafiti
alizozifanya ndani na nje ya Nchi zimemjengea uelewa mpana wa masuala ya Afya
ya Jamii na Lishe na kufanikiwa kuleta mabadiliko ya Sekta ya Afya nchini.
v
Mtazamo wa Kikanda na Kimataifa,
Prof. Janabi ana mtazamo na maono ya maendeleo ya
Sekta ya Afya yanayozingatia afya kwa wote na hii inatokana na uzoefu wake wa
kufanya kazi katika maeneo tofauti ndani na nje ya nchi.
v
Ushirikiano na Wadau wa Sekta ya Afya na Lishe,
Prof. Janabi ameendelea kuwa na uhusiano mzuri na
mashirika ya Kikanda na Kimataifa, Taasisi za utafiti, na wahisani wa Afya
ambayo kwa ujumla yanalenga kuimarisha mifumo ya Afya.
Ndugu Wanahabari;
Prof. Janabi anaingia katika uchaguzi huu akishindana
na wagombea wengine wanne ambao ni: Profesa Moustafa Mijiyawa (Togo), Dkt.
Michael Yao (Ivory Coast), Dkt. Boureima Hama Sambo (Niger) na Dr. Mohamed Lamine Drame (Guinea
Conakry).
Wagombea hawa wanaowania nafasi hii pamoja na Prof.
Janabi wote wanatokea nchi za Afrika ya Magharibi na wawili kati yao Dkt.
Michael Yao (Ivory Coast) na Dkt. Boureima Hama Sambo (Niger) walishiriki
katika uchaguzi uliopita ambao Marehemu Dkt. Ndugulile alishinda.
Ndugu Wanahabari;
Tanzania kupitia mgombea wetu Prof. Janabi tunaimani
kubwa ya kushinda tena kwenye uchaguzi wa Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani
Kanda ya Afrika kutokana na sababu zifuatazo:-
v
Historia, Diplomasia pamoja na Ushirikiano ambao Mheshimiwa Rais Dkt.
Samia Suluhu Hassan ameendelea kuuimirisha baina ya nchi yetu na mataifa
mengine, zinaipaisha Taifa letu kwenye majukwaa ya Kikanda na Kimataifa.
v
Taifa letu lina sifa ya kutoa viongozi wenye weledi katika nyanja
mbalimbali, na tunajivunia kwamba Prof. Janabi yuko tayari kulihudumia
Bara letu katika nafasi hii.
v
Uzoefu wa Prof. Janabi katika masuala ya ugharamiaji wa huduma za
afya kwa kuzingatia kipindi hiki ambacho Dunia inapita katika changamoto ya
kuwa na vyanzo vya uhakika wa ugharamiaji wa huduma za afya; uzoefu wake katika
kudhibiti na kupambana na magonjwa ya mlipuko, uzalishaji wa bidhaa za afya
nchini pamoja na usimamiaji wa mifumo ya utoaji wa huduma za afya zinatupa
nafasi kubwa ya kushinda nafasi hii.
Ndugu Wanahabari;
Kampeni za wagombea wa nafasi hii tayari zimeshaanza
kwa njia mbalimbali, nasi hatuna budi kushirikiana kumnadi mgombea wetu kwa
nguvu, ari na morari kubwa. Nitoe rai kwa wananchi, mashirika na wadau wa Sekta
wa ndani na nje kuungana pamoja katika kumnadi na kumuombea dua mgombea wetu.
Tuna imani kuwa kwa uongozi wake, Afrika itapiga hatua
kubwa katika kuboresha mifumo ya afya, kupambana na magonjwa, na kuhakikisha
kila mwananchi anapata huduma bora za afya.
Mungu ibariki Tanzania! Mungu ibariki
Afrika! Asanteni kwa kunisikiliza.