Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amewataka wanachama wa CCM kuzidisha mshikamano ndani ya chama kwa kipindi chote cha maandalizi ya uchaguzi hadi utakapomalizia mwezi Oktoba.
Ameyasema hayo alipokutana na Viongozi wa Halmashauri Kuu ya Wilaya, Kamati za Siasa za Jimbo na wadi ikiwa ni muendelezo wa ziara yake ya kuimarisha chama ndani ya Wilaya ya Kaskazini "A", Mkoa wa kazkazini ungaja katika Tawi la CCM Chaani.
Amesema ili kuwa na nguvu kubwa ya ushindi katika uchaguzi wa mwezi oktoba, ni lazima wanachama kuwa na umoja na kuzungumza sauti moja ya kukisemea chama vizuri kwa wananchi jambo litakalorahisisha ushindi wa chama hicho.
Mhe. Hemed amesema katika kuelekea kwenye viakao vya uteuzi wa wagombea ni vyema viongozi na wajumbe wa kamati kufanya maamuzi kwa kufuata katiba ya chama inavyoelekeza ili kuweza kupata wagombea watakaweza kuwatetea wananchi majimboni mwao.
Amesema uaminifu, uadilifu, kuacha utashi binafsi, visasi na chuki ni jambo pekee litakalopelekea kupata wagombea wenye sifa na uwezo wa kukiletea ushindi wa kishindo chama cha mapinduzi.
Amewaasa viongozi wa CCM kutokubali kutumiwa vibaya kwa kukununuliwa ama kupokea rushwa katika kipindi chote cha harakati za uchaguzi Mkuu ili kiendelea kulinda heshima na hadhi zao pamoja na chama chao.
Mhe.Hemed amewataka wanachama wa CCM kufanya kazi kwa umoja na mshikamano katika kukijenga na kukiimarisha chama cha Mapinduzi hasa kipindi hiki muhimu cha kukipambia chama kiweze kushinda katika uchaguzi wa mwezi oktoba na kuebelea kushikilia dola.
Amesisitiza kuwa kila mwanachama wa CCM ana haki ya kugombea akiwa na sifa zinazokubalika hivyo hakuna haja ya kutishana, kubezana na kudharauliana badala yake watiane mioyo na kusaidiana.
Amewahamasisha wanawake na vijana kujitokeza kwa wingi katika kitumia haki yao ya kikatiba kwa kugombea nafasi mbali mbali ili waweze kukitumikia chama chao na Taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake Katibu wa Idara ya Siasa, Itikadi, Uwenezi na Mafunzo ya chama ndugu Khamis Mbeto amesema Bajeti ya Serikali ya mwaka 2025/2026 iliyosomwa jana Baraza la Wawakilishi inaenda kumaliza changamoto ndogo ndogo zilizobakia na kuendeleza utekelezaji wa miradi ya kimkati kwa lengo la kuwaletea wananchi maendeleo.
Mbeto amesema Rais Dkt Samia Suluhu na Rais Dkt Hussein Mwinyi hawana deni kwa wananchi kwani kupitia uongozi wao kero na changamoto nyingi za wananchi zimetatulia hivyo amewataka wana CCM kuendelea kuwaunga mkono viongozi hao ili wawndelee kuwatumikia Watanzania.
Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa kazi za Chama cha Mapinduzi kwa kipindi cha Januari hadi Mei, Katibu wa CCM Wilaya ya Kaskazini "A" ndugu Aboud Said Mpate amesema wamejipanga Kimikakati kukiletea ushindi chama chao katika uchaguzi Mkuu kwa kushinda kwenye Majimbo yote yaliyomo ndani ya Mkoa huo.
Mpate amesema Wilaya ya Kaskazini "A" haina shaka na kazi itakayofanywa na kamati ya uteuzi wa wagombea na kusema kuwa wanaamini watapatikana wagombea wenye sifa ya kukitumikia chama kwa uzalendo na kutatua kero na changamoto za wazanzibari.
Imetolewa na Kitengo cha Habari(OMPR)
Tarehe 13.06.2025