Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais TAMISEMI, Profesa Tumaini Nagu, amewataka wauguzi wakuu wa mikoa kuhakikisha usimamizi wa ubora wa huduma zinazotolewa na wauguzi katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini.
Maelekezo haya ya Profesa Nagu yamewasilishwa na Dkt. James Kengia, mratibu wa tafiti za afya katika Ofisi ya Rais – TAMISEMI, wakati wa kikao kazi cha wauguzi wakuu wa mikoa kinachofanyika mkoani Morogoro leo Julai 22, 2025.
Dkt. Kengia akiwasilisha taarifa ya Profesa Nagu amesisitiza kwamba kukosekana kwa mawasiliano mazuri kati ya muuguzi na mteja kunaweza kusababisha utolewaji mbovu wa huduma za afya, jambo linaloweza kupelekea taswira mbaya kwa jamii.
"Unaweza ukafanya vizuri katika tiba lakini kama mawasiliano haya hayapo vizuri, wateja wetu watatoka bila kuridhika na huduma zetu," amesema.
Aidha, Dkt. Kengia amewataka wauguzi wakuu wa mikoa kusimamia kikamilifu suala la usiri wa afya ya mteja na usafi wakati wa utolewaji wa huduma huku akiongeza kuwa baadhi ya wauguzi wamekuwa wakikiuka kanuni hizo muhimu.
Kwa upande wake, Mratibu wa Huduma za Uuguzi na Ukunga katika Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Jesca Mugabilo, amesema kwamba kikao hicho kinalenga kuwakumbusha wauguzi kuhusu jukumu lao la kusimamia huduma za afya.
Kikao kazi hiki cha wauguzi wakuu wa mikoa ya Tanzania Bara kinafanyika kwa siku mbili, kuanzia Julai 22 hadi 23, 2025, katika Manispaa ya Morogoro, kikiwa na mada mbalimbali zinazohusu huduma bora za afya katika maeneo ya kutolea huduma za afya ya msingi.



