Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ametoa salamu za shukrani kwa kupokea Tuzo ya Miaka 30 ya Baraza la Habari Tanzania (MCT) kwa niaba ya Familia ya Hayati Mzee Ali Hassan Mwinyi, Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kutambua mchango wake katika kuimarisha uhuru wa vyombo vya habari nchini.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 15 Julai 2025, katika hafla ya maadhimisho ya miaka 30 ya Baraza hilo iliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa (AICC) Arusha.
Rais Dkt. Mwinyi ameeleza kuwa tuzo hiyo ni uthibitisho wa mchango mkubwa wa Hayati Mzee Ali Hassan Mwinyi, aliyeruhusu kuanzishwa kwa vyombo vya habari binafsi na kutoa uhuru kwa wanahabari, hatua iliyochangia kwa kiasi kikubwa kujenga na kuimarisha tasnia ya habari nchini Tanzania.
Rais Dkt. Mwinyi amesema kuwa kutambuliwa kwa mchango wa Marais waliopita, akiwemo Hayati Julius Kambarage Nyerere na Hayati Mzee Ali Hassan Mwinyi, kunaongeza hamasa kwa kizazi cha sasa kuendelea kuwa wazalendo na kuchangia ustawi wa Taifa.
Katika salamu zake, Rais Dkt. Mwinyi amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa uongozi wake unaowapa wanahabari mazingira bora ya utekelezaji wa majukumu yao kwa Taifa na kuendelea kuwa karibu nao katika ujenzi wa Taifa.
Rais Dkt. Mwinyi amewasihi wanahabari kutumia uhuru wa habari kuhamasisha wananchi, kuendeleza mshikamano wa kitaifa na kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini.
Amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kushirikiana na sekta ya habari katika kukuza maadili, uwajibikaji, uadilifu na uhuru kwa wananchi.
Naye Makamu wa Rais Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango akiwa mgeni rasmi amesisitiza umuhimu wa kuwa na sera, sheria na mifumo madhubuti ya usimamizi wa vyombo vya habari ili kulinda weledi wa tasnia hiyo katika karne ya 21, hususan kwa kuzingatia mapinduzi yanayoletwa na teknolojia ya Akili Unde (Artificial Intelligence – AI).
Mapema, Makamu wa Rais, Mhe. Dkt. Mpango, alimkabidhi Ndg. Madaraka Nyerere Tuzo Maalum ya Miaka 30 ya Baraza la Habari Tanzania (MCT), kwa niaba ya Familia ya Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kwa kutambua mchango wa Baba wa Taifa katika kutumia vyombo vya habari kwa ajili ya ukombozi wa Mataifa ya Kusini mwa Afrika, kujenga umoja wa kitaifa, na kudumisha demokrasia.
Hafla hiyo imehudhuriwa na Mawaziri, Viongozi mbalimbali wa SMT na SMZ, Viongozi wa Vyombo vya Habari, Wawakilishi wa Mabaraza ya Habari kutoka mataifa mbalimbali na wadau wa maendeleo.






















