Utani wa jadi wa Klabu za Yanga na Simba umepamba uzinduzi wa Harambee ya Ujenzi wa Jengo la Ofisi Kuu ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Dodoma iliyofanyika katika eneo la Mradi la Nzuguni C, Jijini Dodoma, ambapo upande wa Wananchi (Yanga) uliongizwa na Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, wakati upande wa Ubaya Ubwela (Simba) ulisimamiwa na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaji Jabir Shekimweli.
Matukio mawili yaliyosisimua waumini na wageni waalikwa walioshiriki Harambee hiyo ni mnada wa mbuzi ambapo mbuzi wawili, mwenye rangi nyeusi akiwakilisha upande wa Yanga alinadiwa kwa shilingi milioni 31 na mbuzi mweupe (Simba) aliuzwa kwa bei kama hiyo ya shilingi milioni 31 na kufanya mbuzi hao wawili kunadiwa kwa jumla ya shilingi 61m.
Kama utani huo haukutosha, viliwekwa vikapu viwili bya sadaka ambapo waumini wanaoshabikia Yanga na Simba walipambanishwa na waumini mashabiki wa Yanga waliibuka kidedea kwa kuchangia shilingi 1,800,000 na Wekundu wa Msimbazi Simba walichangia shilingi 1,210,700.








