- Amkabidhi Nyumba jijini Dodoma
- Mheshimiwa Majaliwa asema Simbu ameliheshimisha Taifa
- Atoa zawadi kwa Timu zilizofanya vizuri kimataifa
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amempongeza Mwanariadha Alphonse Simbu kwa kuwa Bingwa wa Dunia wa mbio za marathon za Tokyo na kwamba ataendelea kutoa kipaumbele katika sekta ya michezo ili itoe mchango zaidi katika kukuza uchumi wa nchi na kuongeza wigo wa upatikanaji ajira kwa vijana
Pongezi hizo zimetolewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa leo Jumamosi (Septemba 27, 2025) alipomwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye hafla kuwapongeza wanamichezo na timu zilizofanya vizuri kwenye medani za kimataifa, hafla hiyo imefanyika katika ukumbi wa mikutano wa hotel jijini Dar es Salaam.
Katika tukio hilo Mheshimiwa Majaliwa alitangaza kuwa, Mheshimiwa Rais. Dkt. Samia amempatia Mwanariadha Simbu zawadi ya nyumba jijini Dodoma, sambamba na kikabidhiwa kitita cha shilingi milioni 20 ikiwa ni ishara ya kutambua ushindi huo ambao umeliletea Taifa heshima kwenye jukwaa la kimataifa"
"Mheshimiwa Rais Dkt. Samia ameandaa nyumba iliyopo mkoani Dodoma, ambayo itakabidhiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na zoezi hilo lisichukue muda mrefu kuanzia leo, tusiwe tunatamka ahadi za viongozi halafu zinakaa muda ambao mtu anajiuliza"
Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Mwanariadha Simbu ameandika ukurasa wa upekee kwa kuwa mtanzania wa Kwanza kutwaa tuzo ya dhahabu katika marathoni ya Dunia ya mwaka 2025 "Haya ni Mashindano makubwa zaidi ya riadha duniani baada ya Michezo ya Olympic, yakihusisha wanariadha Bora kutoka Mataifa yote duniani"
Amesema kuwa Serikali mara zote umekuwa ikiweka jitihada za kutosha za kuhakikisha sekta ya Michezo inakuwa na mchango kwa Taifa "Matokeo tunayoyashuhudia hivi sasa ni matokeo ya uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali ikiwemo ukarabati WA viwanja na kuongezwa kwa bajeti kutoka shilingi bilioni 38 mwaka 2022 Hadi bilioni 326 mwaka 2025/2026"
Katika hatua nyingine Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa wanamichezo nchini kuweka jitihada binafsi katika kushiriki katika michezo kwani ushindi unaweza kupatikana kwa kuweka nia "Wekeni mikakati ya ushindi ili muweze kuipeperusha bendera ya Taifa letu kimataifa".
Naye RAIS wa Shirikisho la Riadha Tanzania (SRT) Rogath Stephen ameishukuru Serikali kwa namna inavyotoa mchango kubwa kwa vyama na namna anavyoendeleza Michezo. "Hatujawahi kufanyiwa mambo ambayo kwasasa yanafanyika, kupitia Serikali tumekuwa tunahudumiwa kwa namna ya kipekee"
Kwa Upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Gerson Msigwa amesema kuwa Medali ya dhahabu ya Alphose Simbu imefanikiwa kupata tiba ya kiu ya Watanzania ya kupata Medali za dhabau katika michezo ya kimataifa. "Hii imewezekana kutokana na na maamuzi ya viongozi wetu kuwa na maono ya kurudisha heshima kwa Taifa baada ya kufanya uwekezaji mkubwa mchezoni"
Ameongeza kuwa Kiu kubwa iliyobaki ni kuhakikisha watanzania wanapata medali kwenye Michezo ya Olympic pamoja na michezo ya jumuiya ya madola "Sisi kama Serikali tumejipanga kuhakikisha tunafanikiwa kuleta medali hizi hapa nyumbani, tunaweka mikakati imara ya usimamizi, kwa sasa kuwa wasindikizaji imetosha, Tunaamini mwakani tunaweza kupata media kwenye Michezo ya jumuiya ya madola na 2028 tutapata medali kwenye olympic"
Timu nyingine zilizopongezwa na kupewa zawadi ya shilingi milioni kumi ni Timu ya Taifa ya Futsal ya Wanawake ambayo imefuzu kushiriki kombe la dunia (Philippines 2025), Timu ya JKT Queens ambao ni mabingwa wa Mashindano ya CAF Woman's Championship League Cecafa Qualifiers 2025.
Timu nyingine ni timu ya Taifa ya Cricket U-19 ambayo itashiriki mashindano ya Dunia 2026 nchini Zimbabwe na timu ya wenye ulemavu (Tembo Worriers) ambao wamekuwa mshindi wa Pili wa Michezo ya Afrika Mashariki na Kati.









