Home » » Baraza la Vijana Zanzibar kuendelea kushirikiana na taasisi mbali mbali za Vijana ndani na nje ya Nchi kutunza Mazingira

Baraza la Vijana Zanzibar kuendelea kushirikiana na taasisi mbali mbali za Vijana ndani na nje ya Nchi kutunza Mazingira

Written By CCMdijitali on Sunday, October 12, 2025 | October 12, 2025

Baraza la Vijana Zanzibar limesema litaendelea kushirikiana na taasisi mbali mbali za Vijana ndani na nje ya Nchi katika kutunza Mazingira na kukabiliana na athari za Mabadiliko ya Tabianchi.


 Hayo yameelezwa na Katibu Mtendaji wa Baraza la Vijana Zanzibar ndugu Ali Haji Hassan wakati wa shughuli ya kufanya Usafi na upandaji miti katika Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya Kitengo cha Wazazi - META ikiwa ni sehemu ya shughuli za shamrashamra za Wiki ya Vijana Kitaifa inayofanyika Mkoa wa Mbeya.


Amesema athari za Mabadiliko ya Tabianchi zinapotokea basi Vijana,Wanawake na Watoto ndio waathirika wakubwa hivyo hakuna budi kwa Vijana kuungana kwa pamoja katika kuunga mkono jitahada zinazochukuliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Dk.Samia Suluhu Hassan na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Dk.Husein Ali Mwinyi. 


"Jukumu la kutunza Mazingira, kuifanya Tanzania kuwa ya Kijani na kupanda miti ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya Tabianchi ni letu sote hasa sisi Vijana." Alihimiza Katibu Mtendaji huyo. 


Aidha Ndugu Hassan alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa Vijana wote wa Tanzania kujitokeza na kushiriki kwa wingi siku ya Uchaguzi tarehe 29 Oktoba 2025 kwa kuhakikisha wanapiga Kura ili kuchaguwa Viongozi ambao watawaletea maendeleo na kuwa sauti ya Vijana huku wakidumisha amani na usalama Nchini. 


Nae Mkurugenzi wa Taasisi ya Empower Youth Prosperity (EYP) Ipyana Mwakyusa amelipongeza Baraza la Vijana Zanzibar kwa jitahada zao za kushirikiana nao na kufanya shughuli tofauti za maendeleo ya Vijana wakiwa Mbeya katika Wiki ya Vijana.


 "Natoa wito na kusisitiza mashirikiano kwa Taasisi hususan katika suala la Mazingira na tunaahidi tutakuwa wasimamizi wazuri na kuhakikisha miti tulioipanda leo inakuwa na kuwa kivutio kwa wanaofika Hospitali hii" Alisisitiza Mwakyusa


Nae Afisa Afya wa Hospitali hiyo Bi Julieth George amewashukuru vijana hao kwa kuichagua Hospital yao kuwa sehemu ya zoezi hilo na kuwataka Vijana hao kuwa zoezi hilo liwe endelevu na sio katika matukio maalum.


Shughuli hiyo imefanyika kwa mashirikiano ya Baraza la Vijana Zanzibar, Taasisi ya Empower Youth Prosperity (EYP) pamoja na wadau Tasisi za Vijana zilizopo Mbeya na zinazotekeleza Mradi wa Vijana Plus uliochini ya Save the Children kwa ushirikiano na Tanzania Bora Iniatives kwa ufadhili wa Umoja wa Ulaya.
Published from Blogger Prime Android App
Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link