NBS WAJADILI KUBORESHA TAKWIMU NCHINI
Na Mwandishi Wetu Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imekutana kujadili utekelezaji pamoja na kupitisha Mpango Kazi wa Awamu ya Pili ya Mradi...
NBS WAJADILI KUBORESHA TAKWIMU NCHINI
Written By CCMdijitali on Thursday, July 17, 2025 | July 17, 2025
Na Mwandishi Wetu
Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imekutana kujadili utekelezaji pamoja na kupitisha Mpango Kazi wa Awamu ya Pili ya Mradi Kabambe wa Kuboresha Takwimu nchini (Tanzania Statistical Master Plan-TSMPT II).
Kikao hicho cha kujadili mradi wa TSMPT II kimefanyika jijini Dodoma jana chini ya mwenyekiti wake ambaye pia ni Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Dkt Natu El-maamry Mwamba. Mradi huo wa TSMPT II unatekelezwa katika kipindi cha mwaka 2022/23 hadi 2026/27.
Awamu ya kwanza ya utekelezaji Mradi Kabambe wa Kuboresha Takwimu nchini (TSMPT I) ulifanyika katika kipindi cha mwaka 2011/12 hadi 2017/18.
Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) mbali na mambo mengine ina jukumu la kutoa takwimu rasmi zilizo bora na huduma zinazokidhi mahitaji ya wadau wa kitaifa na kimataifa kwa ajili ya kupanga mipango na kufanya maamuzi yenye uthibitisho.
RAIS MWINYI AFUNGUA JENGO JIPYA LA TUME YA UCHAGUZI YA ZANZIBAR(ZEC)
Written By CCMdijitali on Wednesday, July 16, 2025 | July 16, 2025
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amezindua rasmi Jengo jipya na la kisasa la Afisi Kuu ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) lililopo Maisara, Mkoa wa Mjini Magharibi, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali kuimarisha mazingira bora ya utendaji wa taasisi hiyo muhimu kwa demokrasia nchini.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo tarehe 16 Julai 2025, wakati wa hafla ya uzinduzi wa jengo hilo, ambapo pia alifungua Afisi ya Wilaya ya Magharibi "B", na kusisitiza kuwa ujenzi wa majengo hayo ni utekelezaji wa ahadi aliyoitoa katika kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2020.
Rais Dkt. Mwinyi amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar haikusita kugharamia ujenzi wa makao makuu ya Tume hiyo pamoja na afisi za wilaya, kwa kutambua umuhimu wa taasisi hiyo katika kuhakikisha chaguzi huru, haki na wa kuaminika.
Kwa mujibu wa taarifa ya kitaalamu, Dkt. Mwinyi amesema kuwa Serikali imetoa jumla ya Bilioni 14,1 kwa ajili ya mradi huo uliojengwa na kampuni ya ujenzi ya CRJE na kutoa wito kwa watendaji wa Tume hiyo kuzitunza ofisi hizo ili ziendelee kuwa katika ubora wa hali ya juu.
Rais Dkt. Mwinyi ameipongeza Tume hiyo kwa kuendelea na maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu kwa ustadi mkubwa, ambapo uandikishaji wa wapiga kura ulifanyika kwa utulivu. Amehimiza wananchi ambao hawajachukua vitambulisho vyao vya kupigia kura kutimiza wajibu wao na kuhakikisha wanatumia haki yao ya kidemokrasia kwa utulivu na kuilinda amani ya nchi.
Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar umemtunukia Rais Dkt. Mwinyi tuzo maalum ya kutambua utendaji na juhudi zake za kuimarisha demokrasia nchini pamoja na kukamilika kwa jengo hilo.
Hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi wakuu wa Serikali na Vyombo vya Ulinzi na Usalama na Watendaji wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Viongozi wa vyama vya Siasa, Taasisi za Ujenzi, pamoja na wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya Unguja na Pemba.




















HATI MILKI ZA ARDHI 1,176 ZATOLEWA MAONESHO YA SABASABA
Na Munir Shemweta, WANMM
Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi imetoa jumla ya Hati Milki za Ardhi 1,176 wakati wa Maonesho ya Kimataifa maarufu kama Sabasaba yaliyomalizika mwishoni mwa wiki.
Katika maonesho hayo yaliyobeba kaulimbiu ya "Fahari ya Tanzania" Wizara ya Ardhi imetoa huduma mbalimbali ikiwemo hati milki za ardhi kwa wamiliki waliokamilisha taratibu za umiliki pamoja na utatuzi wa changamoto za sekta ya ardhi.
Akizungumza wakati wa hitimisho la maonesho hayo jijini Dar es Salaam, Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Dar es Salaam anayeshughulikia wilaya ya Ilala na Temeke Rehema Mwinuka alisema, kati ya hati hizo 1,176, hati 1,040 zimetolewa kwa wamiliki wa mkoa wa Dar es Salaam, 68 Pwani na 68 ni kwa mkoa wa Pwani.
Kwa mujibu wa Rehema, wizara ya Ardhi katika maonesho hayo ya Sabasaba ilihudumia zaidi ya wananchi 1,616 waliofika kuhitaji huduma za sekta ya ardhi katika maeneo mbalimbali.
"Katika maonesho ya mwaka huu wizara yetu ilijipanga kutoa huduma mbalimbali na imefanikiwa kuwahudumia zaidi ya wananchi 1,616 huku hati 1,176 zikitolewa" alisema Rehema.
Kwa upande wao, baadhi ya wananchi waliofika Banda la Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi walionesha kuridhishwa na huduma zilizokuwa zikitolewa wakati wote wa maonesho na kusisitiza umuhimu wa wizara ya Ardhi kuandaa huduma ya pamoja (One Stop Center) ili kuwarahisishia wananchi kupata huduma za sekta ya ardhi.
Walitolea mfano wa huduma ya utoaji Hati Milki za Ardhi pamoja na ukadiriaji kodi ya pango la ardhi kuwa, ni moja ya huduma iiliyopatikana kwa haraka jambo linaloonesha kuwa, wizara ilijipanga katika maonesho hayo
Jaji wa Mahakama Kuu kanda ya Arusha Mhe. Aisha Bade ambaye ni mmoja wa waliopata hati milki ya ardhi katika maonesho hayo alisema, wizara ya Ardhi kwa sasa imebadilika kwani huko nyuma kupata hati ilichukua zaidi ya mwaka.
"Niwapongeze wizara ya ardhi kwa hatua mliyofikia, huko nyuma kupata hati milki ya ardhi ni 'issue' lakini leo nimeipata hati yangu ndani ya muda mfupi, hongereni sana" alisema.
Naye Muigizaji wa sinema za kitanzania (Bongo Movie) Richie Mtambalike ameipongeza wizara ya ardhi kwa kutoa huduma za papo hapo hasa utoaji wa hati milki za ardhi katika maonesho ya kimataifa ya sabasaba.
"Niishukuru Wizara ya Ardhi kwa kutuletea huduma hapa katika maonesho maana kwa upande wangu nimefanikiwa kupata hati milki ya arhi hapa hapa" alisema.
Katika maonesho ya Sabasaba ya mwaka huu Wizara ya Ardhi ilitoa huduma za sekta ya ardhi kwa mkoa wa Dar es salaam ikihusisha manispaa za Kinondoni, Ubungo, Kigamboni, Ilala na Temeke, mkoa wa Pawani pamoja na Dodoma.
Vile vile, elimu kuhusiana na masula ya Sekta ya Milki, Urasimishaji Makazi Holela, Mbaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya pamoja na namna ya kujiunga na Chuo cha Ardhi Morogoro (ARIMO) katika masomo kwa ngazi ya Astashahada na Stashahada zilitolewa.
Msajili kutoka Chuo cha Ardhi Morogoro (ARIMO) Lemuel Ngowi akizungumza na wanafunzi waliotembelea banda la chuo hicho wakati maonesho wa kimataifa ya Biashara (Sabasaba) jijini Dar es Salaam. |
RAIS MWINYI:TUZO KWA HAYATI MZEE MWINYI NI CHACHU YA KUENDELEZA VYOMBO VYA HABARI
Written By CCMdijitali on Tuesday, July 15, 2025 | July 15, 2025
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ametoa salamu za shukrani kwa kupokea Tuzo ya Miaka 30 ya Baraza la Habari Tanzania (MCT) kwa niaba ya Familia ya Hayati Mzee Ali Hassan Mwinyi, Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kutambua mchango wake katika kuimarisha uhuru wa vyombo vya habari nchini.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 15 Julai 2025, katika hafla ya maadhimisho ya miaka 30 ya Baraza hilo iliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa (AICC) Arusha.
Rais Dkt. Mwinyi ameeleza kuwa tuzo hiyo ni uthibitisho wa mchango mkubwa wa Hayati Mzee Ali Hassan Mwinyi, aliyeruhusu kuanzishwa kwa vyombo vya habari binafsi na kutoa uhuru kwa wanahabari, hatua iliyochangia kwa kiasi kikubwa kujenga na kuimarisha tasnia ya habari nchini Tanzania.
Rais Dkt. Mwinyi amesema kuwa kutambuliwa kwa mchango wa Marais waliopita, akiwemo Hayati Julius Kambarage Nyerere na Hayati Mzee Ali Hassan Mwinyi, kunaongeza hamasa kwa kizazi cha sasa kuendelea kuwa wazalendo na kuchangia ustawi wa Taifa.
Katika salamu zake, Rais Dkt. Mwinyi amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa uongozi wake unaowapa wanahabari mazingira bora ya utekelezaji wa majukumu yao kwa Taifa na kuendelea kuwa karibu nao katika ujenzi wa Taifa.
Rais Dkt. Mwinyi amewasihi wanahabari kutumia uhuru wa habari kuhamasisha wananchi, kuendeleza mshikamano wa kitaifa na kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini.
Amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kushirikiana na sekta ya habari katika kukuza maadili, uwajibikaji, uadilifu na uhuru kwa wananchi.
Naye Makamu wa Rais Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango akiwa mgeni rasmi amesisitiza umuhimu wa kuwa na sera, sheria na mifumo madhubuti ya usimamizi wa vyombo vya habari ili kulinda weledi wa tasnia hiyo katika karne ya 21, hususan kwa kuzingatia mapinduzi yanayoletwa na teknolojia ya Akili Unde (Artificial Intelligence – AI).
Mapema, Makamu wa Rais, Mhe. Dkt. Mpango, alimkabidhi Ndg. Madaraka Nyerere Tuzo Maalum ya Miaka 30 ya Baraza la Habari Tanzania (MCT), kwa niaba ya Familia ya Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kwa kutambua mchango wa Baba wa Taifa katika kutumia vyombo vya habari kwa ajili ya ukombozi wa Mataifa ya Kusini mwa Afrika, kujenga umoja wa kitaifa, na kudumisha demokrasia.
Hafla hiyo imehudhuriwa na Mawaziri, Viongozi mbalimbali wa SMT na SMZ, Viongozi wa Vyombo vya Habari, Wawakilishi wa Mabaraza ya Habari kutoka mataifa mbalimbali na wadau wa maendeleo.























KIKWETE NA MALALA WAONYA: BAJETI ZA ELIMU ZISIPUUZWE WAKATI WA MISUKOSUKO YA KIUCHUMI NA KISIASA DUNIANI
Rais Mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete na mwanaharakati wa elimu wa kimataifa na mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel, Malala Yousafzai,wameonya juu ya mwenendo hatarishi duniani wa kupunguza au kupuuza bajeti za elimu hasa wakati wa misukosuko ya kiuchumi na kisiasa.
Wakizungumza kwenye mjadala kuhusu elimu uliofanyika Jumapili usiku katika hoteli ya Johari Rotana jijini Dar es Salaam, viongozi hao wawili waliwataka viongozi wa serikali, wafadhili na washirika wa maendeleo kulinda na kuendeleza uwekezaji kwenye elimu, wakisisitiza kuwa elimu ndiyo msingi wa maendeleo ya kudumu.
“Elimu haipaswi kuwa mhanga wa kwanza wakati wa janga. Si anasa—ni uhai wa maendeleo,” alisema Dkt. Kikwete. “Tukiacha kuwekeza katika elimu leo,tunajitengenezea matatizo makubwa kesho.”
Malala aliongeza kuwa madhara ya kupunguzwa kwa bajeti ya elimu huathiri zaidi wasichana. “Kila matatizo yanapotokea, wasichana ndiyo huathirika kwanza—hutolewa shule, ndoto zao hukatizwa. Hili si tu dhuluma, bali ni upumbavu wa kisera,” alisema.
Katika ziara yao katika Shule ya Sekondari Kibasila siku ya Jumatatu, Dkt.Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya GPE, alitangaza kuwa Tanzania itapokea msaada wa dola milioni 88 za Kimarekani kuanzia mwakani.
Dkt. Kikwete alisema tangu kujiunga na GPE mwaka 2013, Tanzania imepokea zaidi ya dola milioni 344 zilizowezesha ujenzi wa zaidi ya madarasa 3,000, vyoo 7,600, nyumba za walimu 64, shule mpya 18, vituo vya walimu 252, na usambazaji wa vitabu milioni 36.
Kwa upande wake, Malala alitangaza msaada wa dola milioni 3 kutoka kwenye Malala Fund kusaidia wasichana waliokatishwa masomo kutokana na ujauzito au sababu nyingine za kijamii.
Malala pia alipongeza hatua ya serikali ya Tanzania ya mwaka 2021 ya kuruhusu wasichana waliopata ujauzito kurejea shule.
“Uamuzi huu ulikuwa wa kishujaa na wa kibinadamu,” alisema. “Wasichana sasa wanaweza kurudi shule ndani ya miaka miwili au kujiunga na vituo vya elimu mbadala.”
Hata hivyo, wote walikiri changamoto bado zipo, na kwamba chini ya asilimia 50 ya wasichana wanaokamilisha shule ya msingi, na ni asilimia 16 pekee wanaoendelea hadi sekondari ya juu, sababu kubwa zikiwa ni umaskini, mila kandamizi, na uhaba wa miundombinu.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mh. Omary Kipanga, alieleza kuwa kupitia Mpango wa Samia Scholarship ulioanzishwa 2023, wasichana 1,320 tayari wamenufaika kwa kusomea kozi za sayansi vyuo vikuu.
“Mpango huu pamoja na sera ya re-entry ni silaha muhimu kuhakikisha ]wasichana hawapotei kwenye mfumo wa elimu,” alisema.
Dkt. Neema Mwakalinga, mchambuzi wa elimu, alisema ushirikiano na GPE na Malala Fund umeinua hadhi ya Tanzania kimataifa. “Sio tu fedha—ni pia ushauri wa kitaalamu, uraghibishaji, na dhamira ya kisiasa ya kweli.”
Picha na Issa Michuzi
MWISHO