Home » , » Balozi Seif Ali Iddi ampa pole Kiongozi wa Madaktari wa Cuba Profesa Ulpiano

Balozi Seif Ali Iddi ampa pole Kiongozi wa Madaktari wa Cuba Profesa Ulpiano

Written By CCMdijitali on Monday, December 29, 2014 | December 29, 2014

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akimpa pole Kiongozi wa Madaktari wa Cuba Profesa Ulpiano Nyumbani kwake Vuga Mjini Zanzibar baada ya kuvamiwa na majambazi jana usiku yeye na wenzake maeneo kati ya Kikwajuni na SUZA.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akiagana na Mke wa Kiongozi wa Madaktari wa Cuba Dr. Ulpiano mara baada ya kuwapa pole kutokana na mtihani uliowapatya wa kuvamiwa na Majambazi.
Kati kati yao ni Dr. Barbara nyuma ya Balozi Seif ni Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar {SUZA } Dr. Idrissa Rai.
Balozi Seif akibadilishana mawazo na Madarkati wa Cuba hapo nyumbani kwao Vuga alipokwenda kuwafariji na kuwapa pole baada ya kuvamiwa na Majambazi.
Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.


Press Release:-


Kamanda wa Polisi Mkoa Mjini Magharibi Msaidizi Kamishna wa Polisi { ACP } Mkadam Khamis Mkadam alisema Jeshi la Polisi Mkoa huo linawashikilia watu wawili miongoni mwa majambazi wanaotuhumiwa kuhusika na uvamizi wa Madaktari Bingwa wa Cuba katika maeneo kati ya Kikwajuni Wireles na Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar {SUZA } mapema jana usiku.

Alisema polisi ilianza uchunguzi mara moja baada ya kupata taarifa ya kuvamiwa kwa Madaktari hao walionyang’anywa mikoba,vitu pamoja na Fedha zao ambapo mmoja kati yao Profesa Ulpiano alijeruhiwa kwa panga kichwani.

Kamishna Msaidizi wa Polisi { ACP } Mkadam Khamis Mkadam alieleza hayo wakati Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alipofika nyumbani kwa Madaktari hao Vuga Mjini Zanzibar kuwafaribi baada ya kupatwa na mkasa huo.

Kamanda Mkadam alisema Mkoa wa Mjini umekuwa na matukio ya kuibuka kwa vitendo vinavyoashiria kuichezea amani baadhi ya wakati jambo ambalo jamii inahusika kwa kiasi kikubwa katika kushirikiana na Jeshi la Polisi kukabiliana na vitendo hivyo.

Alisema ulinzi ni jukumu la watu wote, hivyo miundo mbinu iliyopo hivi sasa Duniani ya mitandao ya mawasiliani katika uwekaji wa Kamera za CCTV inahitajika kutumika kwa lengo la kuwabaini watu wanaojihusisha na matendo maovu.

Kamanda huo wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi alizishauri Taasisi za Umma, Binafsi na hata watu wa kawaida wakakijengea utamaduni wa kutumia mfumo huo mpya ili kuwa na maisha ya salama.

Akiwapa pole Madaktari hao Bingwa wa Cuba wanaotoa huduma katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja pamoja na kusomesha Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar { SUZA } Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema hilo ni tukio la ajabu na la kusikitisha katika visiwa vya Zanzibar.

Balozi Seif alisema vitendo hivyo viovu vinavyofanywa na baadhi ya wahuni vimekuwa vikileta sura mbaya kutokana na sifa ya Zanzibar yenye Utamaduni wa kistaarabu wa kupenda wageni tokea karne nyingi zilizopita.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwahakikishia Madaktari Bingwa hao wa Cuba kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia vyombo vyake vya ulinzi inaendelea na uchunguzi wa kina na wahusika wa vitendo hivyo watapopatikana mkondo wa sheria utafanya kazi zake dhidi ya wahalifu hao.

Balozi Seif aliwataka Madaktari hao kuendelea na majukumu yao kama kawaida na Serikali itakuwa makini katika kuwahakikishia usalama wao pamoja na wageni wengine wakati wao wote wawapo hapa Nchini.

Wakitoa shukrani zao kwa faraja hiyo pamoja na juhudi zilizochukuliwa na vyombo vya ulinzi katika kuwasaka wahalifu waliohusika na tukio hilo Madaktari hao wa Cuba waliahidi kuendelea kutoa huduma kama kawaida licha ya mkasa uliowakumba.

Madaktari hao walielezea matumaini yao kwamba Serikali pamoja na vyombo vyake vya ulinzi vitafanya juhudi za ziada katika kuona kwamba matukio kama hayo yanadhibitiwa kabisa.
Madaktari hao wanne wa Cuba ni Dr. Barbara, Dr. Daisy Batle, Dr.Katia wakiwa na Kiongozi wao Profesa Ulpiano walivamiwa ghafla na vijana walioshuka na mapanga kwenye Gari aina ya Noah wakati wakitokea Kikwajuni kuelekea nyumbani kwao Vuga.


Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar


Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link