Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akiwa na Viongozi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya awali akifurahia mandhari nzuri ya Jengo la Maktaba Kuu ya Zanzibar Tawi la Pemba mara baada ya kuweka jiwe la msingi la uendelezaji wa njengo hilo hapo Chachaani Chake chake Pemba.
Wanafunzi wa Sekondai Chake chake Pemba wakionyesha igizo safi lnaloonyesha umuhimu wa matumizi ya Maktaba katika mazingira ya mwanaadamu popote pale alipo.
Picha na Hassan Issa wa –OMPR – ZNZ.
Press Release:-
Shirika la huduma za Maktaba
Zanzibar limetakiwa kuangalia uwezekano wa
kuzidisha kasi ya majukumu yake katika kupeleka huduma za maktaba
Vijijini ili wananchi waweze kuongeza maarifa yanayokwenda sambamba na mahitaji
ya maisha yao.
Wito huo umetolewa na Makamu wa
Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati akiweka jiwe la msingi la
ujenzi wa Jengo la Maktaba Kuu ya Zanzibar Tawi la Pemba hapo Mtaa wa Chachaani
Mjini Chake chake Pemba ikiwa ni muendelezo wa shamra shamra za maadhimisho ya
kusherehekea kutimia miaka 51 ya Mapinduzi Matukufu wa Zanzibar ya Mwaka 1964.
Balozi Seif alisema anaelewa
juhudi zinazochukuliwa na shirika la huduma za Maktaba Zanzibar lakini kasi
hiyo ni vyema kwa hivi sasa ikaelekezwa zaidi vijijini kwa vile wananchi wengi
wanaoishi katika maeneo hayo hawana fursa za kutosha za kujisomea na
kujiendeleza.
Alisema hivi sasa huduma nyingi
za maktaba zinapatikana zaidi katika maeneo ya miji ambako watu wengi wana
maarifa pamoja na vyanzo mbadala vya kupata huduma hiyo kwa kujisomea na
kuongeza maarifa yao.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
alifahamisha kwamba Serikali imefanya juhudi za kuongeza maktaba ikifahamu
kwamba eneo hilo ni muhimu kwa kuweza
kuwapatia wananchi maarifa mbali mbali ya fani tofauti.
Balozi Seif alitoa wito kwa
wananchi wa Kisiwa cha Pemba kujenga utamaduni wa kujisomea vitabu, magazeti na
majarida tofauti kwa lengo la kuongeza maarifa mapya yatakayowasaidia katika
maisha yao lakini pia ni sehemu ya kujiburudisha.
Alisisitiza kwamba elimu bora
haipatikani madarasani tu bali pia maktaba ina mchango mkubwa katika kuwawezesha
kupata elimu iliyo bora. Hivyo amewahimiza wanafunzi kuitumia fursa waliyoipata
ya kuitumia maktaba ili kupata maarifa za ziada.
Alieleleza kwamba kupanuka kwa
huduma za elimu hakuna budi kwenda sambamba na upatikanaji wa miundombinu na
nyenzo mbali mbali za elimu ikiwemo huduma za maktaba za kisasa.
Alisema pamoja na wanafunzi
kwenda skuli na kujifunza lakini bado kuna haja kubwa sana kwa wao kupata
taaluma zaidi ya ziada kwa lengo la kujiongezea maarifa ili kukuza kiwango chao
cha elimu.
Alieleza kwamba Serikali
imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kueneza huduma za elimu katika maeneo mbali mbali
Unguja na Pemba mijini na vijijini na hili linadhihirika wazi kutokana na
ongezeko kubwa la Skuli 279 za maandalizi, msingi 250, msingi na kati 109 na
sekondari 147.
- “ Mwaka 1964 wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wakati inaanza kuongoza baada ya kufanya Mapinduzi ilikuwa na skuli 62 tu za msingi na skuli 4 tu za sekondari wakati elimu ya vyuo vikuu wanafunzi walilazimika kuvuka maji kwenda Tanzania bara au nchi za Ulaya “. Alisema Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar aliwaasa wananchi na watu wote watakaotumia maktaba hiyo kuhakikisha
kwamba wanaitunza pamoja na vifaa vyake vyote ili lengo la kuwepo kwake lifikiwe na kuchangia maendeleo ya elimu.
Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar aliipongeza Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali pamoja na Bodi ya
huduma za Maktaba kwa juhudi za kufikishia huduma za maktaba karibu na wananchi
na kuwashauri waongeze nguvu za kuweka mataba kila Wilaya Unguja na Pemba.
Mapema akisoma risala yenye
mnasaba na shughuli hiyo ya Maktaba Kuu ya Zanzibar Tawi la Pemba Msaidizi
Mkutubi Mkuu wa Maktaba hiyo Bibi Mwache Moh’d alisema ujenzi wa jengo la
Maktaba hiyo ulioanza mwezi Septemba mwaka 2013 tayari umeshafikia asilimia 90%.
Bibi Mwache alisema ujenzi huo
unaotarajiwa kukamilika na kutoa huduma za Maktaba kwa wanafunzi, wataalamu na
wananchi mwezi ujao umezingatia pia
mahitaji ya watu maalum kama wale wenye ulemavu, watoto wadogo pamoja na watu
wazima.
Msaidi Mkutubi Mkuu huyo wa
Huduma za Maktaba Tawi la Pemba ameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar kwa kugharamia ujenzi huo
utaofikia jumla ya shilingi Milioni 655,000,000/- ambapo huduma za kijamii
zitakuwa zimesogezwa kwa Wananchi.
Hata hivyo Bibi Mwache Moh’d
alisema bado Shirika la Huduma za Maktaba Kuu Zanzibar Tawi la Pemba
linaendelea kukabiliwa na baadhi ya changamoto akiitaja sugu zaidi kuwa ni
suala la usafiri.
Alisema Watendaji wa Shirika hilo
wanashindwa kutekeleza vyema majukumu yao kutokana na ukosefu wa huduma za
usafiri jambo ambalo linawanyima fursa za kutoa na kufuatilia huduma za Maktaba
katika Wilaya na Maskuli mbali mbali Kisiwani humo.
Naye Naibu Waziri wa Elimu na
Mafunzo ya Amali Zanzibar Mh. Zahra Hamad alisema Wizara hiyo hivi sasa
imejikita kuelekeza nguvu zake katika ujenzi wa Maktaba za Wilaya ili
kuwajengea utamaduni wa kupenda kusoma Wanafunzi na Wananchi wa maeneo yote Mjini na Vijijini.
Mh. Zahra alisema ujenzi huo ulio
chini ya mradi wa I.G.P utakwenda sambamba na ununuzi wa Mabasi yatakayoliwezesha
shirika la Huduma za Maktaba kutoa huduma za Maktaba hadi Vijijini.
Alisema Wizara ya Elimu hivi sasa inaendelea na juhudi za
kusomesha wakutubi kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar {SUZA }
pamoja na Shirika la Huduma za Maktaba ili kukabiliana na uhaba wa
wakutubi uliopo katika Wilaya na Skuli
mbali mbali za Zanzibar.
Mh. Zarha alifahamisha kwamba
shirika hilo kwa kushirikiana na Wizara na SUZA tayari limeshawapatia
mafunzo tofauti wakutubi mia mbili na
ishirini na saba ngazi ya Stashahada, 75 ngazi ya Cheti pamoja na 25
kushiriki semina mbali mbali.