Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi akizungungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Sekretarieti Afisi Kuu ya CCM Zanzibar.
Waandishi wa Habari wakimsikiliza Katibu wa Itikadi na Uenezi Nape Nnauye alipokuwa anazungumzia maazimio ya kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM kilichofanyika Zanzibar tarehe 13 Januari 2015
Waandishi wa Habari wakimsikiliza Katibu wa Itikadi na Uenezi Nape Nnauye alipokuwa anazungumzia maazimio ya kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM kilichofanyika Zanzibar tarehe 13 Januari 2015
CCM YAITAKA SERIKALI KUENDELEA KUTEKELEZA
MAAZIMIO YA BUNGE
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI.
Jana tarehe 13/01/2015 Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa chini ya uongozi wa Mwenyekiti wake wa Taifa Dr. Jakaya Mrisho Kikwete ilifanya kikao chake cha kawaida cha siku moja Kisiwandui Mjini Zanzibar.
Pamoja na mambo mengine baadhi ya mambo yaliyojadiliwa na Kamati Kuu ni pamoja na:-
1. SAKATA LA AKAUNTI YA ESCROW
Chama Cha Mapinduzi kimesikitishwa sana na sakata hili. Baada ya kulijadili kwa muda mrefu na kwa kina Kamati Kuu imeamua yafuatayo:-,
i). Pamoja na yale ambayo yameshatekelezwa na serikali, Kamati Kuu imeitaka serikali na vyombo vinavyohusika kuendelea kutekeleza maazimio ya bunge juu ya swala hilo.
ii). Kamati Kuu imewataka wote wanaopewa dhamana wajenge utamaduni wa kuwajibika kwa dhamana zao, na wasipowajibika waliowapa dhamana wachukue hatua za kuwawajibisha.
iii). Aidha Kamati Kuu imeiagiza Kamati Ndogo ya Maadili kuchukua hatua za kimaadili kwa wale wote waliohusika na ukiukwaji wa maadili kwenye sakata la Escrow na wako kwenye vikao vya maamuzi vya Chama. Kikao cha Kamati Ndogo ya Maadili kitafanyika tarehe 19/01/2015 kwa ajili ya utekelezaji wa agizo hilo.
2. WALIOPEWA ADHABU KWA KUKIUKA MAADILI YA CHAMA.
Itakumbukwa kuna makada sita wa CCM walipewa adhabu kwa kuhusishwa na ukiukwaji wa maadili kwenye mchakato wa kutaka kuteuliwa na CCM kugombea urais, watamaliza muda wa adhabu zao mwezi wa pili mwaka 2015.
Baada ya muda wa adhabu zao kuisha, itafanyika tathimini kuona kama walizingatia mashariti ya adhabu zao. Na kama kuna ambao watakutwa hawakuzingatia mashariti ya adhabu zao wataongezewa adhabu.
3. SOKO LA MAHINDI
Kamati Kuu imepokea taarifa ya mwenendo wa soko la mahindi nchini. Baada ya tathimini na uchambuzi, pamoja na kazi iliyofanywa na serikali, Kamati Kuu imeiagiza serikali kuangalia upya mfumo unaotumiwa na Hifadhi ya Taifa ya Chakula ( NFRA)katika ununuzi wa mahindi, ili unufaishe zaidi wakulima badala ya utaratibu wa sasa ambao kwa kiasi kikubwa unanufaisha zaidi mawakala badala ya wakulima moja kwa moja.
4. RATIBA YA VIKAO VYA CHAMA.
Kamati Kuu imepitisha ratiba ya shughuli mbalimbali za Chama kwa mwaka 2015.
Aidha ratiba ya mchakato wa kuwapata wagombea wa CCM ndani ya dola utapangwa na vikao vijavyo vya Chama.