Rais JAKAYA KIKWETE
Rais JAKAYA KIKWETE ametoa salamu za mwaka mpya wa 2015 kwa
Watanzania na kuelezea kuridhishwa na mafanikio yaliyopatikana kwenye sekta
mbalimbali mwaka 2014 ikiwemo hali ya usalama wa mipaka ya nchi, utekelezaji wa
miradi mikubwa ya kimkakati hususani ile ya maji na miundombinu ya usafirishaji
na uchukuzi.
Katika salamu zake, Dakta KIKWETE pia ameelezea dhamira ya
serikali ya kuondoa ada katika elimu ya sekondari kuanzia mwaka 2016.
Rais KIKWETE amelimwagia pongezi Jeshi la Polisi kwa juhudi
zake za kupambana uhalifu nchini ukiwemo ugaidi.
Amesema taarifa za polisi zinaonyesha kuwa mwaka 2014
vitendo vya uhalifu vimepungua ikilinganishwa na mwaka 2013 pamoja na kutambua
mtandao wa viongozi na washirika wao wanaotuhumiwa kupanga na kufanya
mashambulizi ya kigaidi.
Aidha Rais KIWETE amesema katika mwaka 2014 hali ya uchumi
wa nchi imeendelea kuimarika ambapo makusanyo ya mapato ya serikali
yameongezeka na kufikia Asilimia 90 ya lengo na kuongeza kuwa Ofisi ya Takwimu
imekamilisha marekebisho ya takwimu za Pato la Taifa.
pia amesema amefarijika na kuendelea kupungua kwa matukio ya
ajali za barabarani ikilinganishwa na mwaka 2013, mafanikio katika vita dhidi
ya biashara na matumizi ya dawa za kulevya nchini ikiwemo kukamatwa kwa vigogo
wa biashara hiyo huku akisema kuwa mwaka 2014 mapambano dhidi ya ujangili na
biashara haramu ya bidhaa zinazotokana na wanyama pori yameimarishwa.
Masuala mengine ambayo Rais KIKWETE ameyazungumzia katika
hotuba yake ni pamoja na jitihada za kuboresha hali ya usafiri ikiwemo kazi ya
kujenga barabara za lami na kuimarisha barabara za udongo ili ziweze kupitika
wakati wote, kuimarisha huduma ya usafiri wa Reli ya Kati na kukua kwa sekta
usafiri wa anga.
Aidha Rais KIKWETE amesema serikali imeendelea kupiga hatua
za kuridhisha katika kuboresha elimu nchini ikiwa ni pamoja na kupunguza tatizo
la upungufu wa maabara, vitabu na walimu wa shule za msingi na sekondari.
Rais KIKWETE pia amesema wajibu wa viongozi wa Serikali za
Mitaa Vitongoji na Vijiji waliochaguliwa katika uchaguzi uliofanyika Desemba 14
na Desemba 20 mwaka jana ni kufanya kazi waliyoiomba.