HALI ya kisiasa
ndani ya chama cha Demokrasia na maendeleo (Chadema) mkoa wa Iringa si shwari baada ya mwenyekiti wake mkoa wa Iringa Mustapher Msowela kumfikisha polisi mwenyekiti wa chama hicho wilaya ya Iringa
mjini, Frank Nyalusi
Nyalusi ambae pia ni
diwani wa kata ya Mvinjeni jimbo
la Iringa mjini juzi alitiwa nguvuni na
jeshi la Polisi kabla ya kuachiwa kwa dhamana.
Nyalusi aliyeshitakiwa katika kituo cha Polisi cha kati cha
mjini Iringa jana, anatuhumiwa kumtusi mwenyekiti wake huyo wa mkoa kupitia
mitandao ya simu; matusi yanayoendelea kuchunguzwa na jeshi hilo.
Nyalusi amekamatwa kwa tuhuma hiyo ikiwa ni siku chache tu
baada ya kudaiwa kutoa tuhuma za uongo kwa lengo la kujipatia umaarufu dhidi ya
mfanyabiashara maarufu wa mjini Iringa, Salim Asas ambaye pia ni Kamanda wa
Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) mkoa wa Iringa.
Katika mkutano wa hadhara uliofanywa na Chadema Desemba 21
kwenye uwanja wa Mwembetogwa mjini Iringa, Nyalusi ambaye pia ni diwani wa kata
ya Mivinjeni alitoa tuhuma zinazowahusisha vijana watatu ambao hata hivyo
hakuwataja majina kwamba walitumwa na Asas kwenda kumuua.
Asas kwa kupitia kwa wakili wake, Alfred Kingwe amekanusha
tuhuma hizo alizoziita ni za kipuuzi ambazo haziwezi kubebeka hata kwa mzani
mdogo wa kupimia madini.
Ili kumsafisha mteja wake, Kingwe alisema ndani ya siku 14
toka akabidhiwe hati ya madai (Demand Note), Nyalusi anatakiwa kuitisha mkutano
katika eneo lile lile alilotolea tuhuma hizo na kuzikanusha vinginevyo
atafikishwa mahakamani.
Akizungumza na wanahabari jana, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa
Iringa, Ramadhani Mungi alisema; “Kuhusu
tukio la kumtukana mwenyekiti wake wa mkoa, Nyalusi alikamatwa jana mara baada
ya Msowela kuwasilisha malalamiko yake polisi, akahojiwa na kuachiwa baada ya
kukamilisha taratibu za dhamana.”
Alisema jeshi la Polisi linaendelea kuchunguza tukio hilo la
kijinai na endapo litathibitika kuwa la kweli, Nyalusi ambaye pia ni Diwani wa
Kata ya Mivinjeni mjini Iringa atafikishwa mahakamani.
Kuhusu tukio linalomuhusisha na Asas, Kamanda Mungi alisema
jeshi la Polisi limefanya mahojiano ya awali na wahusika hao.
“Jambo hili lipo, tunachunguza; yapo maneno Nyalusi ameyatamka kwenye mkutano wao wa hadhara kwamba ametishiwa kuuawa, ametumiwa watu watatu kwenda kumuua wakiwa na visu. Kumtishia mtu ni kosa la jinai na kumtuma mtu kwenda kumdhuru mtu mwingine ni kosa la jinai, kwahiyo tunachunguza” alisema.
Alisema katika mazingira ya uwazi, Polisi inachunguza suala
hilo ili kujua Nyalusi alitishiwa katika mazingira gani; alitishiwa na nani na
kwanini hakwenda kutoa taarifa hiyo Polisi na kufungua kesi ili Polisi
iwakamate wahusika na kulinda maisha yake.
“Lakini tunajaribu kuangalia kama hakutishiwa na ametamka
vile katika mkutano wa hadhara, lengo lake lilikuwa ni nini na kama anajua
madhara yake kwa jamii iliyosikia taarifa hiyo ni yepi,” alisema.
Alisema kama itabainika taarifa zilizotolewa na Nyalusi ni
za uongo, sheria itachukua mkondo wake na kama itadhihiri ni za kweli sheria
pia itachukua mkondo wake.