Rais wa Jumuiya ya Samael Academy Sheikh Nassir Bin Said akitoa salamu kwenye hafla ya maulidi ya Kuzaliwa Mtume Muhammad { SAW } yaliyofanyika Masjid Rahman Gombani chake chake Pemba.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akiteta na Rais wa Jumuiya ya Samel Academy Sheikh Nassir Bin Said wakati wa hafla ya Maulidi ya uzawa wa Mtume Muhammad { SAW } hapo Gombani chake chake Pemba.
Afisa Mdhamini Wizara ya Katiba na Sheria Pemba Sheikh Omar Khamis aisifu Samael Academy kwa uamuzi wake wa kusaidia jamii Kisiwani Pemba.
Mwanafunzi Isra Hilal Mwadini akifuatiwa na mwenzake Tamima Abass Sheha wakipokea zawadi kutoka kwa mgeni rasmi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif wakati wa hafla ya Maulidi ya Jumuiya ya Chuo cha Samael Academy.
Kulia ya Balozi Seif ni Rais wa Sameil Academy Sheikh Nassir Bin Said.
Mwanafunzi Chum Hijjaakifuatiwa na Awat Abdulla wa Samel
Academy wakipokea zawadi kutoka kwa Balozi Seif baada ya kuhitimu mafunzo yao.
Picha na – OMPR – ZNZ.
Press Release:-
Jamii ya Kiislamu Nchini inapaswa kufuata vilivyo mafundisho
sahihi aliyokuwa akiyasimamia Kiongozi
wa Dini ya Kiislamu Mtume Muhammad { SAW } ili
Jamii hiyo ipate fursa nzuri ya kuishi katika maisha ya furaha na
ustaarabu wa maendeleo makubwa ndani ya Dunia hii.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo katika
hafla ya maulidi ya uzawa wa Mtume Muhammad { SAW } yaliyoandaliwa na Chuo cha
Samail Academy na kufanyika katika Msikiti Rahman uliopo Gombani Mjini Chake
chake Kisiwani Pemba.
Balozi Seif alisema kigezo chema alichokuwanacho Kiongozi
huyo wa waislamu kilijikita zaidi katika kusimamia vyema suala la kudumisha
amani katika Dunia, kuleta umoja baina ya waislamu, kujikubalisha kuishi na
mayatima sambamba na watu wa rika zote bila ya ubaguzi.
Aliupongeza Uongozi wa Chuo cha Samail Academy kwa juhudi
zao walizozichukuwa na hatua waliyoifikia katika kuijenga jamii kitaaluma na
maadili yanayokubalika.
Balozi Seif alitoa
wito kwa vijana kujishughulisha zaidi katika kutafuta elimu kwani ndio nyenzo
pekee inayomfanya mwenye nayo anapoitumia vizuri hupata maendeleo makubwa.
Hata hivyo alionya kwamba wapo baadhi ya watu wamekuwa
wakiitumia vibaya elimu waliyobarikiwa kwa kupotosha wenzao wasiokuwa nayo ili
kufikia malengo yao binafsi.
“ Kuna Watu huitumia
elimu kuwageuza wenzao kuwa ngazi ya kupandia kuyafikia malengo yao binafsi.
Mwenyezi muungu hayataki mambo hayo. Tutumie elimu kwa kuelimisha wengine “. Alisisitiza Balozi
Seif.
Alisema mafanikio makubwa kitaaluma na kijamii yatapatikana
endapo jamii itajikubalisha kujituma
katika misingi ya uaminifu licha
ya changamoto za kimaisha
zinazowazunguuka katika maeneo yao.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar akiridhia kukubali kuwa
mlezi wa chuo hicho cha Samael Academy aliahidi kuzishughulikia changamoto
zinazowakabili Walimu na Wanafunzi hao
kwa kutoa mchango wake kadri hali itakavyoruhusu.
Akisoma Risala Mudiri wa Samaeil Academy Sheikh Said Abdulla
Nassor alisema Taasisi hiyo iliyoasisiwa mwaka 2012 na kusajiliwa rasmi Mwaka
2014 inajishughulisha na masuala ya kijamii katika maeneo mbali mbali hapa
nchini.
Mudir Said alisema Samael Academy imejikita katika kusaidia
jamii katika uchimbaji wa visima, kuunganisha Madrasa kuwa na nguvu za pamoja,
kuwakusanya watoto yatima kwa kuwajengea mazingira bora ya kielimu na maisha
yao ya baadae pamoja na kuanzisha mafunzo kwa walimu wanaotoa hotuba
misikitini.
Alisema yao mafanikio makubwa tokea kuanzishwa kwa taasisi
hiyo mwaka 2012 akizitaja kuwa ni pamoja
na kuzikusanya na kuzisajili madrasa zipatazo 95 zenye wanafunzi elfu 10,995,
kusajili mayatima 712 pamoja na kuzitembelea madrasa kwa kuangalia changamoto
zinazozikabili.
Mudiri huyo wa Samael Academy Sheikh Said Abdulla Nassor
alifahamisha kwamba moja kati ya jambo lililopewa kipaumbele na taasisi hiyo ni
kuwaendeleza wanafunzi na vijana waliofanikiwa kumaliza kuhifadhi juzuu 30 za
Quran tukufu.
Hata hivyo Sheikh Said Abdulla Nassor alielezea changamoto
zinazoikabili Taasisi hiyo akizitaja kuwa ni pamoja na vikwazo kwa baadhi ya
watendaji wa taasisi za umma wanavyovitoa kwa Taasisi hiyo pamoja na usumbufu
wa vifaa vya msaada vinavyotolewa wanafadhili wakati wa kutolewa bandarini.
Akitoa salamu zake Rais wa Samael Academy Sheikh Nassir Bin
Said alisema Uongozi wa Jumuiya ya Taassi hiyo unafarajika na muitikio mkubwa
wa wazazi na walezi waliooonyesha katika kuipokea taasisi hiyo yenye mnasaba na
mazingira yao.
Sheikh Nassir alisema juhudi zitaendelea kuchukuliwa na
Uongozi huo ili kuona malengo yaliyokusudiwa ya kusaidia jamii kukabiliana na
mazingira yanayowazunguuuka yanafanikiwa vyema na kustawisha jamii zao.
Akimkaribisha mgeni rasmi katika hafla hiyo ya Maulidi ya
uzawa wa Mtume Muhammad { SAW } Afisa mdhamini Wizara ya Katiba na Sheria Pemba
Bwana Omar Khamis alisema Samel Academy tayari imeshaonyesha nia sahihi ya
kutaka kusaidia jamii hapa nchini.
Sheikh Omar alisema Taasisi hiyo iko mbioni kujenga misikiti
mikubwa mitatu Kisiwani Pemba,maandalizi ya ujenzi wa chuo Kikuu cha Kiislamu
Chamanangwe pamoja na ujenzi wa chuo cha Amali Chake chake Pemba.
Alisema uanzishwaji wa chuo hicho cha amali umelenga
kuwajengea mazingira mazuri wanafunzi watakaopata taaluma kwenye taasisi hiyo
ambapo maandalizi yameanza katika kuhakikisha kwamba wanafunzo hao wanapata
ajira ndani na nje ya Nchi.
Alifafanua kwamba Nchi za Saudi Arabia na Iraq ambazo
zimeamuwa kujitolea kusaidia harakati za ujenzi wa chuo hicho cha amali
Kisiwani Pemba zimekubali kuwapokea baadhi ya wanafunzi wa chuo hicho wamalizapo mafunzo kwa kuwapatia fursa za
ajira katika Mataifa hayo.