Baadhi ya Sehemu za jengo la Jiko la Hoteli ya Kendwa Rocks iliyoko Mkoa wa Kaskazini Unguja ambalo iliuungua moto ulisababishwa na hitilafu za umeme.
Wahandisi wa Hoteli ya Kendwa wakijaribu kurejesha miundo mbinu ya umeme iliyoathirika kutokana na moto mkubwa uliotokea kwenye Hoteli hiyo.
Jengo la Jiko la Hoteli ya Kendwa Rocks lililoungua vibaya mwa moto uliosababishwa na hitilafu ya umeme.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akimfariji Mwakilishi wa Hoteli ya Gold Zanzibar iliyopo Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unguja Bwana Andrea Azzala baada ya paa la jengo lao kuungua moto.
Balozi Seif akikaguzwa kuangalia maeneo yaliathirikia
kutokana na moto kwenye Hoteli ya Kendwa Rocks Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Kulia ya Balozi Seif ni
Msaidizi Menja Mkuu wa Kendwa Rocks Bwana Omar Ibrahim Kilupi, Mkuu wa
Mkoa wa Kaskazini Unguja Kanal Mstaafu Juma Kassim Tindwa na Waziri wa Nchi
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Moh’d Aboud Moh’d.
Picha na – OMPR – ZNZ.
Press Release:-
Hitilafu ya umeme iliyotokea mapema asubuhi imesababisha moto mkubwa ulioteketeza jengo la jiko, Duka ,sehemu ya burdani ya Hoteli Kendwa Rocks pamoja na Hoteli ya Gold Zanzibar zilizopo katika Kijiji cha Nungwi Mkoa wa kaskazini Unguja.
Moto huo ulioripuka kwa kusaidiwa na upepo mkali uliokuwa ukivuma majira ya saa nne za asubuhi umeteketeza vitu na vifaa mbali vilivyokuwemo ndani ya majengo hayo na kusabisha hasara inayokisiwa kufikia shilingi za Kitanzania Bilioni Moja { 1,000,000,000/- }.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiambatana pamoja na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Moh’d Aboud Moh’d walifika eneo la tukio kuwafariji wamiliki wa Hoteli hizo.
Meneja wa Kendwa Rocks Bwana Ali Ibrahim Kilupi alimueleza Balozi Seif kwamba wafanyakazi kwa kushirikiana na wananchi wanaozizunguuka Hoteli hizo walijaribu kuuzima moto huo uliokuwa ukiwaka kwa kasi kutokana na upepo mkali uliovuma wakati huo.
Bwana Ali alifahamisha kwamba Uongozi wa Hoteli hiyo ulijaribu kuwasiliana na Kikosi cha Zima moto na Uokozi Zanzibar kujaribu kusaidia uokozi huo lakini wakati huduma hizo zinakaribi kufika kasi ya moto huo iliyochukuwa baina ya dakika 15 na 20 tayari ilikuwa imeshateketeza vifaa na vitu vyote.
Alieleza kwamba licha ya wageni wengi kuvutiwa na mazingira ya nyumba zinazoezekwa makuti lakini Uongozi wa Hoteli hiyo umeamua kubadilisha mfumo huo kwa kutumia vitage ili kujaribu kujikinga na majanga kama hayo.
Naye Mwakilishi wa Hoteli ya Gold Zanzibar Bwana Andrea Azzala alisema kwa kwa hivi sasa ni mapema mno kujua hasara iliyopatikana kutokana na kuungua kwa paa la jengo lao moja.
Bwana Andrea aliwashukuru wafanyakazi na baadhi ya wananchi wa vijiji jirani vilivyozuunguka Hoteli hizo kwa jitihada zao zilizosaidia kukabiliana na moto huo uliovumba ghafla mapema asubuhi.
Akitoa pole kwa wamiliki wa miradi hiyo ya Hoteli Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesikitishwa kutokea kwa janga hilo la moto litakalorejesha nyuma malengo ya wamiliki wa hoteli hizo.
Hata hivyo Balozi Seif amefurahishwa na Uongozi wa Hoteli hiyo kwa uamuzi wake wa kuuwekea bima ya moto mradi wao kwani itasaidia kupunguza machungu ya hasara iliyotokea.
Alisema maafisa wa Idara ya Maafa Zanzibar ambayo iko chini ya Ofisi yake itafanya tathmini kujuwa harasa kamili iliyotokea ya janga hilo na kuripoti Serikalini ili kuangalia namna ya kusaidia wawekezaji hao wazalendo.
Akitoa shukrani kwa niaba ya Uongozi wa hoteli ya Kendwa Rocks Msaidizi meneja Mkuu wa Hoteli hiyo Bwana Omar Ibrahim Kilupi ameipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibaf kwa kuwa karibu na Wananchi wake.
Majanga ya miripuko ya moto yamekuwa yakitokea mara kwa mara katika kipindi cha kiangazi na kusababisha hasara kubwa inayochukuwa muda mrefu hasa kwenye miradi ya hotel.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
14/2/2015.