Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akisalimiana na Madaktari wa Cuba wanaomaliza muda wao wa utumishi hapa Zanzibar ambao aliwaandali chakula cha Jioni nyumbani kwake Mazizini nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Balozi Seif akisalimiana na Mkuu wa Mafunzo wa Madaktari Wazalendo wa Zanzibar waliopata taaluma chini ya Madaktari Mabingwa wa Cuba Dr. Daisy Batlle kabla ya chakula cha jioni alichowaandalia Madaktari mabingwa wa Cuba.
BaloziSeif akibadilishana mawazo na Kiongozi wa Madaktari wa Cuba Profesa Ulpiano hapo nyumbani kwake Mazizini nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Kiongozi wa Madaktari Mabingwa wa Cuba Profesa Ulpiano wa kwaza kutoka kulia akiwa pamoja na Mwenyeji wake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar wakipata mlo kwenye hafla fupi waliyoandaliwa Madaktari hao.
Baadhi ya Madaktari Mabingwa wa Cuba wanaomaliza muda wao wa kazi hapa Zanzibar wakipata mlo wa jioni nyumbani kwake Balozi Seif Ali Iddi hapo Mazizini.
Balozi Seif akimzawadia Kasha Kiongozi wa Madaktari wa Cuba Profesa Ulpiano mara baada yam lo wa jioni kama ishara ya kumbukumbu ya uwepo wao hapa Zanzibar.
Mkuu wa Mafunzo wa Madaktari Wazalendo wa Zanzibar waliopata Taaluma chini ya Madaktari Mabingwa wa Cuba Dr. Daisy Batlle akipokea zawadi kutoka kwa Balozi Seif.
Picha na – OMPR – ZNZ.
Press Release:-
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeipongeza Serikali ya Cuba kwa juhudi inayoendelea kuchukuwa katika kuunga mkono harakati za maendeleo ya Kijamii ya Zanzibar hasa katika Sekta ya huduma za Afya.
Pongezi hizo zimetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi katika hafla Maalum ya chakula cha Jioni aliyowaandalia Madaktari Mabingwa wa Cuba wanaotoa huduma za Afya pamoja na kutoa mafunzo kwa Madaktari wazalendo wa Zanzibar.
Hafla hiyo iliyofanyika katika Makazi ya Balozi Seif yaliyopo Mazizini nje kidogo ya Mji wa Zanzibar imetayarishwa ili kuwaaga rasmi Madaktari hao baada ya kukamilisha muda wao wa kutoa huduma za Afya wa miaka miwili ambapo wanatarajiwa kurejea nyumbani Cuba Mwezi Septemba Mwaka huu.
Balozi Seif alisema kwamba huduma za afya zilizokuwa zikitolewa na Madaktari Mabingwa hao wa Cuba zimeweza kuleta faraja kubwa kwa Wananchi walio wengi hapa Zanzibar.
Alieleza kuwa yapo mafanikio makubwa yaliyopatikana kutokana na uimarishwaji wa mfumo wa huduma za afya uliopekelea kuongezeka kwa Madaktari wazalendo Nchini kasi ambayo imekwenda sambamba na ile azma ya Serikali ya kulenga kuwa na huduma za Afya katika maeneo yasiyozidi kilomita Tano.
Balozi Seif alisisitiza kwamba bado Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inahitaji kuongeza nguvu zaidi katika Sekta hiyo muhimu kwa ustawi wa Jamii ili kufikia kiwango bora cha utoaji wa huduma za afya kilichowekwa na shirika la Afya Duniani { WHO }.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliwatakia maisha ya furaha na upendo Madaktari hao wa Jamuhuri ya Cuba wakati watakaporejea Nyumbani kwao mnamo Mwezi Septemba mwaka huu wa 2015.
Katika hafla hiyo fupi ya chakula cha jioni Balozi Seif aliwazawadia Madaktari hao Makasha Maalum kama ishara ya ukumbusho wao wakati walipokuwepo hapa Zanzibar wakitoa huduma za Afya pamoja na kutoa mafunzo kwa Madaktari Wazalendo.
Akitoa shukrani kwa niaba wenzake Kiongozi wa Madaktari hao Profesa Ulpiano alisema wakati wa utumishi wao hapa Zanzibar walilazimika kufanya kazi kwa juhudi, bidii na maarifa kutokana na ukarimu walioupokea kutoka kwa Wananchi wa Zanzibar.
Profesa Ulpiano alisema kwamba Madaktari hao wa Cuba wataendelea kukumbuka maisha ya Zanzibar ambayo yaliwapa fursa ya kujihisi kwamba wanaishi katika maisha ya kifamilia kama wapo Nyumbani kwao Cuba.
Zanzibar imekuwa na uhusiano wa muda mrefu na Nchi za Jamuhuri ya Cuba pamoja na Jamuhuri ya Watu wa China ambapo Mataifa hayo mawili yamekuwa yakiendeleza ushirikiano huo na Zanzibar kwa kusaidia kitaaluma huduma za Afya hapa Zanzibar tokea miaka ya 60 mara baada ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Mwaka 1964.