Home » » Balozi Mteule wa Tanzania Nchini Zimbabwe Luteni Kanali Mstaafu Charles Makakala

Balozi Mteule wa Tanzania Nchini Zimbabwe Luteni Kanali Mstaafu Charles Makakala

Written By CCMdijitali on Saturday, August 22, 2015 | August 22, 2015

Balozi  Mteule wa Tanzania Nchini Zimbabwe Luteni Kanali Mstaafu Charles Makakala amtembelea  Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi

 Balozi Mteule wa Tanzania Nchini Zimbabwe Luteni Kanali Mstaafu Charles Makakala akisalimiana na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alipofika Ofisini kwake kujitambulisha na kuaga rasmi baada ya kuteuliwa kushika wadhifa huo wa Kidiplomasia.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akibadilishana mawazo na Balozi Mteule wa Tanzania Nchini Zimbabwe Luteni Kanali Mstaafu Charles Makakala.Picha na – OMPR – ZNZ.

 Press Release:-

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesisitiza umuhimu wa Mataifa ya Kusini Mashariki mwa Bara la Afrika {SADC} kuendelea kushirikiana katika Nyanja ya kiuchumi kutokana na Historia ndefu ya Mataifa hayo ya kusaidiana wakati wa kujikomboa kutoka katika makucha ya wakoloni.

Balozi Seif alieleza hayo wakati akizungumza na Balozi Mteule wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Nchini Zimbabwe Luteni Kanali Mstaafu Charles Makakala aliyefika Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar kujitambulisha pamoja na kuaga rasmi baada ya kuteuliwa kushika wadhifa huo wa kidiplomasia hivi karibuni.

Alisema Zimbabwe ikiwa miongoni mwa Mataifa hayo ya Sadc ilijikomboa kutoka mikononi mwa Warodesia kupitia juhudi kubwa zilizochukuliwa na Tanzania ambazo Balozi Makakala anawajibika kuendelea kuisimamia sifa hiyo wakati akitekeleza majukumu yake ya kidilpomasia Nchini Zimbabwe.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimueleza Balozi huyo Mteule wa Tanzania Nchini Zimbabwe kwamba kazi kubwa anayostahiki kuisimamia kwa wakati huu ni kuhakikisha uhusiano kati ya Tanzania na Zimbabwe hasa katika masuala ya Kiuchumi unaimarika zaidi.

Alisema Zimbabwe inaeleweka vyema Kimataifa katika medani ya Kisiasa kutokana na msimamo wake wa kupinga ukoloni mamboleo unaosababisha mgawanyo wa kikabila miongoni mwa wananchi wake.

Balozi Seif alifahamisha kuwa juhudi zinazopaswa kuchukuliwa hivi sasa kwa wataalamu na wachumi wa Mataifa ya Sadc chini ya usimamizi wa Wana Diplomasia wa Mataifa hayo ni kuweka mkazo zaidi katika kuona wananchi wa Ukanda huo wanakomboka kiuchumi.

Naye Balozi Mteule wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Nchini Zimbabwe Luteni Kanali Mstaafu Charles Makakala ameahidi kwamba atatekeleza kwa umakini jukumu lake la Kidiplomasia alilokabidhiwa na Taifa.

Balozi Makakala alisema anafarajika kuielewa vyema Zimbabwe katika kipindi kirefu wakati akishiriki ukombozi wa Nchi hiyo jambo ambalo alieleza kwamba linampa nguvu na mbinu za kujua namna gani aanze kushirikiana na Viongozi wa Taifa hilo la Kusini mwa Afrika katika kudumisha uhusiano wa Kidiplomasia wa pande hizo mbili.

Alifahamisha kwamba atahitaji kuwekewa mlango wazi na Viongozi wakuu wakati atakapohitaji msaada wa mawazo na nguvu za uwezeshaji ili atumie fursa hiyo kwa lengo la kufanikisha kazi hiyo nzito inayohitaji busara na umakini mkubwa.

Luteni Kanal Mstaafu Charles Makakala aliwahi kuwa Mkuu wa Chuo cha Kijeshi Kunduchi ambapo baada ya kustaafu kwake miezi ya hiuvi karibuni akabahatika kuteuliwa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Jakaya Mrisho Kikwete kushika wadhifa huo.

 
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
22/8/2015.
Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link