Na Charles Charles
SIKU tatu zilizopita, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilitangaza kamati ya watu 32 ya uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani uliopangwa kufanyika Oktoba 25, mwaka huu.
Timu hiyo ambayo inaongozwa na Katibu Mkuu wa CCM, Komredi Abdulrahman Kinana ilitangazwa kwa waandishi wa habari na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye.
Kinana ambaye ndiye Mwenyekiti wa Kamati hiyo iliyoteuliwa na Kamati Kuu ya CCM, chini ya Rais Jakaya Kikwete, Jumatatu wiki hii, atasaidiwa na Makamu Wenyeviti wawili.
Wote ni Naibu Makatibu Wakuu wa CCM, Rajabu Luhwavi wa Tanzania Bara na Vuai Ali Vuai wa Zanzibar.
Wajumbe wa Kamati hiyo ni Stephen Wassira, Shamsi Vuai Nahodha, Sophia Simba, Dk. Asha-Rose Migiro, Dk. Harrison Mwakyembe, Samwel Sitta na Muhammed Seif Khatibu.
Wengine ni January Makamba, Mwigulu Nchemba, Amina Makilagi, Christopher ole Sendeka, Abdallah Bulembo, Khadija Aboud, Mohammed Aboud, Lazaro Nyalandu, Issa Haji Ussi na Waridi Bakari Jabu.
Katika orodha hiyo pia kuna Mahmoud Thabit Kombo, Maua Daftari, Stephen Masele, Pindi Chana, Shaka Hamidu Shaka, Makongoro Nyerere, Benard Membe, Sadifa Juma Khamis, Anthony Diallo, Livingstone Lusinde na Ummy Mwalimu.
Tayari baadhi ya wajumbe wa timu hiyo, siku ileile walizungumza na gazeti hili, ingawa kwa kifupi kuhusiana na shughuli waliyopewa, hususan ya kuongoza harakati za kumzuia Waziri Mkuu aliyejiuzulu kwa kashfa, Edward Lowassa ili asiwe rais wa nchi hii.
Mathalani, Wassira ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, anasema pamoja na tuhuma nyingi za ufisadi mkubwa, Lowassa pia ni mgonjwa anayeshindwa mpaka kuzungumza vizuri na kuongeza:
"Wapo wanaokwenda kumwangalia (mikutanoni), lakini wakirudi wanasema kumbe ndiyo huyu? Mbona mgonjwa na anashindwa hata kuongea?"
Najua kauli hiyo ya Wassira kamwe haiwezi kuwapendeza viongozi wa Chadema kama Mwenyekiti wa Taifa, Freeman Mbowe; Makamu Mwenyekiti, Profesa Abdallah Safari au Naibu Katibu Mkuu (Tanzania Bara), John Mnyika.
Haiwezi kuwafurahisha viongozi wa Chadema kama Naibu Katibu Mkuu (Zanzibar), Salum Mwalimu, Mwanasheri mkuu wao, Tundu Lissu na wengineo.
Pamoja na kuona Lowassa alivyodhoofika kiafya tofauti na alivyokuwa zamani, lakini wapambe wake ambao sasa wamo mpaka viongozi hao wa Chadema hawawezi kukubali.
Dalili zinazoonyesha kuwa afya ya mgombea huyo wa urais imedhoofu, kwa namna moja ama nyingine ni pamoja na zungumza yake ya sasa, tembea yake na kadhalika.
Mathalani, wapo waliomuona wakati wa ziara ya Kinana, Monduli mapema mwaka huu wanaodai alishindwa hata kunyanyua kitofali kidogo, tena chenye uzito usiozidi hata chupa moja tu ya soda.
Wapo waliomuona kwenye mazishi ya mtoto wa Makamu Mwenyekiti wa CCM (Tanzania Bara), Philip Mangula kule Njombe au ya aliyekuwa Mbunge wa Mbinga Magharibi mkoani Ruvuma, Kapteni John Komba wanaodai ilikuwa shida hata kuweka mashada ya maua juu ya makaburi yao.
Wapo waliomuona Shinyanga kwenye mazishi ya aliyekuwa Mufti wa Tanzania, marehemu Issa Shaaban bin Simba mwezi Juni, mwaka huu.
Hao pia kuna wengine wanadai alipata taabu kutupia udongo kaburini, hatua iliyotokana kwa kiasi kikubwa zaidi na mikono yake kukosa nguvu za uhakika.
Hali hiyo iliibua minong'ono na mshangao mkubwa makaburini, hatua iliyokana na ukweli kuwa katika kipindi hicho, Lowassa alikuwa ameshachukua fomu ya kuomba uteuzi wa kugombea urais kupitia CCM.
Waliokuwa wakimuona wakati wa vikao vya NEC, Makao Makuu ya CCM mjini Dodoma wanajua pia jinsi alivyokuwa, wakati mwingine akisaidiwa hata kushuka ngazi moja tu na fupi mlangoni!
Pamoja na kukabiliwa na tuhuma kubwa kabisa za ufisadi, lakini pia inawezekana CCM ilimwengua katika mbio hizo kwa sababu afya yake inaonekana kuwa ni tete.
Namfahamu Lowassa kwa kuonana na hata kuongea naye tangu mwaka 1995 alipokuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo Mijini wakati wa utawala wa Serikali ya Awamu ya Pili.
Namfahamu hadi alipokuwa Waziri Mkuu wa Kwanza wa Serikali ya Awamu ya Nne , kipindi ambacho aliwahi kuniita na kuongea naye mara mbili.
Kwanza alinipigia simu usiku na kuagiza tukutane Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (Terminal One), kesho yake saa 3.30 asubuhi.
Siku chache baadaye, Lowassa aliniita tena ofisini kwake, Magogoni jijini Dar es Salaam ili kwenda kuongea naye.
Katika hali hiyo, mimi ni mmoja kati ya Watanzania ambao wanamjua kwa kumuona kwenye picha magazetini, kupitia televisheni na hata uso kwa uso.
Mara yangu ya mwisho kuongea naye kwa dakika chache, tena mazungumzo ya faragha ingawa hadharani, ilikuwa ni Jumamosi ya Julai 11, mwaka huu, mjini Dodoma.
Lowassa niliyekuwa namfahamu kwa kukutana na kuongea naye kati ya mwaka 1995 - 2008 na yule wa sasa, laigwanaan ambaye tuliteta kwa mara yetu ya mwisho siku 42 zilizopita ni watu wawili tofauti.
Huyu anayegombea urais kwa tiketi ya Chadema ana dalili zote kuwa amedhoofika mno kiafya, hivyo sidhani kama hata akina Freeman Mbowe, Profesa Abdallah Safari, John Mnyika, Salum Mwalimu au Tundu Lissu wana huruma naye!
Nadhani wanacholenga hasa kwake ni kile kinachosemekana kuwa mamilioni ya fedha aliyonayo, yale ambayo anayejua chanzo chake ni yeye mwenyewe.
Bila shaka wanachotaka kwake ni 'kuibeba' Chadema kifedha wakati wote wa kampeni, lugha ambayo kuna wengine wanasema ni 'kumchuna'.
Wanajua hata iweje kamwe hawezi akashinda katika kinyang'anyiro cha urais, lakini hawataki kumwambia ukweli maana ataondoa misaada yake.
Wanajua akishashindwa itabidi arudi kwao akasimamie mifugo yake, lakini akitaka anaweza pia akabaki jijini Dar es Salaam ili kuwa na uhakika wa kupata ushauri wa kisaikolojia.
Wanajua kuwa kushinda kwa Lowassa, kwa namna yoyote ile ni sawa na chura kugeuka tembo. Nani amewahi kuona?
Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa Simu Na. 0659 220 220 na 0762 633 244