Katibu wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Kaskazini “B” Bibi Subira Mohammed Ali akitoa matokeo ya kura za Maoni baada ya kukamilika kwa zoezi la kupiga kura ndani ya majimbo Manne yaliyomo ndani ya Wilaya hiyo.
Matokeo hayo yalitolewa kwenye Ofisi ya CCM Jimbo la Kitope iliyopo Kinduni ambapo Bibi Subira aliwatanabahisha wananchi na Wanachama kuelewa kwamba maneno yaliyokuwa yakiandikwa mwenye mitandano ni uzushi, unafiki na uongo mtupu unaofaa kupigwa vita.
Picha na – OMPR – ZNZ.
Press Release:-
Chama cha Mapinduzi Wil;aya ya Kaskazini “B” Kimetoa matokeo ya kura kwa Majimbo Manne yakijumuisha wadi zake yaliyomo ndani ya Wilaya hiyo baada ya kukamilika kwa zoezi la upigaji kura za maoni.
Zoezi hilo lilifanyika Jumamosi ya Tarehe 1 Agosti kwa Majimbo yote ya Wilaya hiyo kama yalivyopanya kwa majimbo yote Nchini lakini Tawi la CCM Mahonda likaahirisha uchaguzi huo kwa nafasi pekee ya Ubunge baada ya kutokea hitilafu ndogo na kuendelea kufanyika jioni ya Tarehe 3 Agost.
Akitangaza matokeo ya kura hizo Katibu wa CCM Wilaya ya Kaskazini “B” Bibi Subira Mohammed Ali alisema Jimbo la Bumbwini lilikuwa na wagombea saba ambapo walioongoza nafasi ya kwanza alikuwa Mbarouk Juma Kura 802,Ramadha Haji kura 445 na Ame Bakari kura 52.
Bibi Subira alisema nafasi ya Uwakilishi jimbo hilo la Bumbwini wagombea walikuwa Wanane ambapo walioongoza wa kwanza ni Mtumwa Pea, kura 631, Khamis Juma kura 238 na Mlinde Mabrouk kura 169.
Katibu huyo wa CCM Wilaya ya Kaskazini “B”Bibi Subira alieleza kuwa Jimbo la Kiwengwa kwa nafasi ya Ubunge walikuwa wagombea Sita ambapo walioongoza wa mwanzo alikuwa Msimba Makame Mbaourk kura 765, Khamis Mtumwa Kura 484 na Khilika Khamis Kura 404.
Katika Jimbo la Donge Bibi Subira alieleza kwamba nafasi ya Ubunge wagombea walikuwa Saba na walioongoza Mshindi wa Kwanza alikuwa Sadifa Juma Khamis aliyepata kura 2,410, Moh’d Hija kura 372 naKombo Ali kura 83.
Alisema upande wa Uwakilishi Jimbo la Donge wagombea walikuwa Wawili ambapo katika matokea hayo aliyepata nafasi ya kwanza alikuwa Khalid Salum Mohammed aliyepeta kura 2,989 na Mashauri Sheikh kura 404.
Alisema nafasi ya Uwakilishi jimbo hilo la Kiwengwa wagombea walikuwa Wanane ambapo walioongoza wa kwanza ni Asha Abdulla Mussa kura 739, Zamir Makame kura 668 na Moh’d Sijamini kura 163.
Kuhusu Jimbo jipya la Mahonda Bibi Subira alisema kwa nafasi ya Ubunge wagomea walikuwa wanane ambapo washindi walioongoza wa kwanza alikuwa Bahati Abeid Nassir kura 1,364, Kidawa Hamid Saleh kura 821 na Mwinyi Jamal Ramadhan alikuwa wa tatu.
Bibi Subira aliwaomba washiriki wa mchakato huo kuondoka na kazi moja ya kuhakikisha Chama cha Mapinduzi kinashinda nkwenye uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi oktoba mwaka huu.
Alisema washiriki hao wanaondoka kwenye ukumbi huo wa Ofisi ya CCM Jimbo la Kitope hakujatangazwa mshindi katika matokeo hayo ya kura bali kililichotangazwa ni matokeo ya kura.
Katibu huyo wa CCM Wilaya ya Kaskazini “B” alifahamisha kwamba uchaguzi huo wa kura za maoni umekwenda salama na kuuhakikishia umma kwamba yale maneno yaliyoenezwa mwenye mitandao ni uzushi na uzandiki mkubwa unaofaa kupuuzwa.
Bibi Subira aliwatahadharisha washiriki wa mchakato huo kuelewa kwamba Chama hakitomvumilia kiongozi au mwanachama ye yote atakayejaribu kuleta majungu na fitina wakati huu wa kuelekea kwenye uchaguzi Mkuu.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
3/8/2015.