Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Uongozi wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania { TCRA } ukiongozwa na Mkurugenzi Mkuu wake Dr. Ally Yahya Simba wa Pili kutoka Kushoto.
Wa kwanza kushoto ni Meneja wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania Kanda ya Zanzibar Bwana Othman Sharif.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania { TCRA } Dr. Ally Yahya Simba wa Pili kutoka Kushoto akifafanua jambo wakati timu yake ilipofanya mazungumzo na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Picha na – OMPR – ZNZ.
Picha na – OMPR – ZNZ.
Press Release:-
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania { TCRA } imejipanga kuliwezesha Kitaaluma Jeshi la Polisi Nchini katika azma yake ya kukabiliana na wimbi jipya la matumizi mabaya ya mitandao ya mawasiliano linaloonekana kushika kasi katika maeneo mbali mbali Duniani.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania Dr. Ally Yahya Simba alieleza hayo wakati akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Ofisini kwake Mtaa wa Vuga Mjini Zanzibar.
Dr. Ally Yahya Simba akiuongoza Ujumbe wa Viongozi Watatu wa Taasisi hiyo na kujitambulisha rasmi baada ya kuteuliwa kushika wadhifa huo Tarehe 6 Julai mwaka huu alisema Mamlaka ya Mawasiliano kwa mujibu wa sheria ina jukumu la kufuatilia makosa ambayo tayari yameshafanywa kwenye Mitandao.
Alisema Jeshi la Polisi ndilo lenye haki ya kufungua kesi kwa wahusika wa makosa ya Mitandao jambo ambalo askari wa Jeshi hilo wanapaswa kuwa na elimu ya kutosha itakayowapa uwezo mkubwa wa kukabiliana na wahusika wa makosa hayo.
Alifahamisha kwamba zipo Kesi Nne zinazohusu matumizi mabaya ya Mitandao hiyo ambazo zinatarajiwa kutolewa maamuzi yake hivi karibuni na vyombo vinavyohusika kufuatia kupitishwa kwa sheria ya matumizi ya mitandao ya Mawasiliano Nchini kulikofanywa na Bunge ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mkurugenzi Mkuu huyo wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania { TCRA } Dr. Ally Yahya Simba aliishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa uamuzi wake wa kuipatia Mamlaka hiyo eneo la Kiwanja kwa ajili ya kujenga Ofisi yake hapa Zanzibar.
Dr. Ali alisema hatua hiyo ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeipa nguvu Mamlaka hiyo kufanya kazi zake kwa ufanisi zaidi katika Visiwa vya Zanzibar vikiwa ni miongoni mwa Kanda Tano zinazojumuisha na kuunda Mamlaka hiyo Nchini Tanzania.
Mapema Meneja wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania { TCRA }Kanda ya Zanzibar Bwana Othman Sharif alisema yapo mafanikio makubwa ya zaidi ya asilimia 99% tokea kuanzishwa kwa mradi mpya wa Mawasiliano { post cort } katika Visiwa vya Unguja na Pemba.
Bwana Othman alisema mradi huo umetekelezwa katika shehia Nne Hapa Zanzibar akizitaja kuwa ni Selemu na Dimbani kwa Kisiwa cha Pemba pamoja na Mombasa na Chukwani kwa Kisiwa cha Unguja.
Meneja huyo wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania Kanda ya Zanzibar aliishukuru Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano Zanzibar pamoja na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwa mashirikiano makubwa ilizotoa katika kufanikisha mradi huo muhimu kwa ustawi wa Jamii Nchini.
Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar bado inaendelea kuzihimiza Taasisi za Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kuendelea kufungua Ofisi zao Zanzibar.
Balozi Seif alisema hatua hiyo ya ufunguzi wa Ofisi pamoja na huduma za Taasisi hizo italenga katika ile azma ya Waasisi wa Taifa hili ya kutaka kuimarisha Muungano wa Mwezi Aprili mwaka 1964 uliofanywa na pande hizo mbili za Muungano wa Tanzania.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliipongeza Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania { TCRA } kwa jitihada zake za kuanzisha mradi mpya wa mawasiliano { Post cort }utakaosaidia kwa kiasi kikubwa ulinzi wa Maeneo pamoja na mazingira.
Hata hivyo Balozi Seif alifahamisha kwamba zipo changamoto za baadhi ya Mitaa pamoja na Majina yake kujengwa au kuanzishwa bila ya utaratibu wa kuzingatia Mipango miji pamoja na Halmashauri za Wilaya.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
30/9/2015.