Mkuu wa Timu ya Waangalizi wa Uchaguzi wa Umoja wa Ulaya{ EU } Bibi Zudith Sargentini kati kati aliyenyanyua mikono akitaka ufafanuzi wa jinsi Zanzibar ilivyojiandaa na kujipanga na Uchaguzi Mkuu wa Mwezi Oktoba mwaka huu wa 2015 kutoka kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi.
Balozi Seif alikutana na Ujumbe huo wa Timu ya Waangalizi wa Umoja wa Ulaya ulioongozwa na Balozi wa Umoja huo Nchni Tanzania Balozi Filiberto Sebregondi hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Picha na – OMPR – ZNZ.
Press Release:-
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imezihakikishia Timu za Waangalizi wa Kimataifa za Uchaguzi zilizoomba kushuhudia Uchaguzi wa Mwezi Oktoba mwaka huu kwamba uchaguzi Mkuu wa Zanzibar na ule wa Tanzania utafanyika katika hali ya Amani na utulivu.
Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati akizungumza na Ujumbe wa Waangalizi wa Uchaguzi wa Umoja wa Ulaya { EU } aliokutana nao hapo Ofisi ni kwake Vuga Mjini Zanzibar ambao tayari upo nchini kwa kazi hiyo takriban mwezi mmoja sasa.
Balozi Seif Ali Iddi alisema Serikali imejizatiti na kujipanga vyema katika mazingira ya kuona hali ya Nchi inaendelea kuwa ya Amani muda wote, kwa hivi sasa, wakati wa uchaguzi na baada ya kukamilika kwa zoezi zima la uchaguzi.
Alisema taratibu za kutatua Changamoto pamoja na matatizo yanayojitokeza katika kipindi hichi cha harakati za Kampeni zimekuwa zikichukuliwa chini ya usimamizi wa Tume ya Uchaguzi wa Zanzibar { ZEC } katika Vikao mbali mbali kwa kuwahusisha wadau wote wa uchaguzi.
Balozi Seif aliueleza Ujumbe huo wa Waangalizi wa Uchaguzi wa Umoja wa Ulaya unaoongozwa na Balozi wa Umoja wa huo Nchini Tanzania Balozi Filiberto Sebregondi kwamba Kampeni za uchaguzi zimekuwa zikiendelea vyema kwa wagombea wa nafasi mbali mbali za Uongozi kutoka vyama vya Siasa wakinadi sera zao.
Hata hivyo Balozi Seif alisema zipo kasoro zinazojitokeza katika baadhi ya maeneo wakati huu wa kampeni ambazo baadhi ya watu huonyesha ishara za kutaka kuwazuru wafuasi wa Vyama vya siasa wakati wanaporejea kutoka kwenye Mikutano yao ya hadhara ya Kampeni.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alitahadharisha kwamba tabia hiyo mbaya inafaa kuachwa mara moja kwa vile inaweza kuamsha hamasa zinazoweza kusababisha vurugu na hatimae kuvunjika kwa hali ya amani ya Nchi.
Aliuhakikishia ujumbe huo wa Waangilizi wa Kimataifa wa Uchaguzi kwamba Serikali kupitia vyombo vyake vya Dola imekuwa ikisisitiza umuhimu wa Wanachama na Viongozi wa vyama vya Siasa kufuata Kanuni na Taratibu zilizowekwa na Tume za Uchaguzi za Zanzibar na ile ya Tanzania ili kuona uchaguzi Mkuu unafanyika na kumalizika katika njia ya amani na usalama.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliupongeza Umoja wa Ulaya kwa uamuzi wake wa kuleta Waangalizi wa Uchaguzi kwenye chaguzi mbali mbali za Tanzania katika vipindi tofauti.
Mapema Mkuu wa Timu ya Waangalizi wa Uchaguzi wa Umoja wa Ulaya { EU } Bibi Zudith Sargentini alisema Timu yake itajigawa katika makundi mawili yatakayojipanga kuangalia uchaguzi Mkuu kwa pande zote mbili za Unguja na Pemba.
Bibi Zudith alisema Timu hizo pia zitapanga utaratibu wa kukutana na wadau wa Uchaguzi wakiwemo Viongozi wa juu wa Serikali katika kuona mazingira ya kampeni, uchaguzi na hata matokeo ya kura yanakuwa katika hali ya amani na upendo miongoni mwa wadau wote.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
29/9/2015.