Home » » Magufuli 65% Lowassa 25%

Magufuli 65% Lowassa 25%

Written By CCMdijitali on Wednesday, September 23, 2015 | September 23, 2015

 Mgombea Urais wa CC, Dk John Magufuli.

TAKRIBANI mwezi mmoja kabla ya Watanzania kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu ujao Oktoba 25 mwaka huu, Taasisi ya Twaweza imetoa matokeo ya utafiti wake kuhusu ‘Sauti za Wananchi’ kwenye siasa na kuonesha kuwa, kama uchaguzi huo ungefanyika leo, mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk John Magufuli angeibuka mshindi kwa asilimia 65.

Watanzania watapiga kura Oktoba 25, mwaka huu kuchagua Rais, Wabunge na Madiwani na kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Twaweza, Aidan Eyakuze, matokeo hayo ni ya utafiti wa hivi karibuni uliofanywa na taasisi hiyo kwa kukusanya taarifa za madodoso kutoka kwa washiriki utafiti zaidi ya 1,300 wa Tanzania Bara.

Katika matokeo hayo, utafiti ulionesha kuwa iwapo uchaguzi ungefanywa leo, Mgombea urais wa CCM, Dk Magufuli angeibuka mshindi huku akimshinda mpinzani wake wa karibu, Mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa ambaye ana asilimia 25.

Wananchi na CCM Eyakuze alisema wahojiwa hao walipoulizwa wanajisikia kuwa karibu zaidi na chama gani, asilimia 62 walisema wako karibu na CCM huku Chadema ikipata asilimia 25 na vyama vingine vikiambulia asilimia moja.

“Utafiti wetu tunaomba ueleweke, tuliwauliza wananchi maswali bila kutaja majina ya wagombea na wao katika swali la unadhani uchaguzi ungefanyika leo, ungemchagua nani, asilimia 65 walisema watamchagua Magufuli na asilimia 25, walisema Lowassa,” alifafanua Eyakuze ambaye alibainisha kuwa utafiti ulifanyika katika mikoa yote ya Tanzania Bara.

Katika utafiti huo uliofanywa mapema Agosti hadi Septemba mwanzoni mwaka huu, wahojiwa waliulizwa swali ni mgombea yupi watampigia kura na kwa nini, na majibu yalikuwa asilimia 26 walisema watampigia Magufuli kwa sababu ni mchapakazi huku asilimia 12, wakisema watampigia Lowassa kwa sababu ya kutaka mabadiliko.

Aidha, mkurugenzi huyo wa Twaweza alisema vigezo muhimu vinavyohusu makundi mbalimbali ya watu vilitumika kuchambua ni nani au makundi gani yanayowaunga mkono mgombea wa CCM, Dk Magufuli na Lowassa.

Hata hivyo, makundi ya vijana na wasomi zaidi na wakazi wa mijini walionekana zaidi kumuunga mkono Lowassa, huku makundi ya watu wazima na wenye elimu ya kiasi na wakazi wa vijijini wakimuunga mkono Dk Magufuli.

Hata hivyo, katika makundi hayo yote bado Dk Magufuli ameonekana kuongoza; mfano, asilimia 57 ya watu wenye umri wa miaka 18 – 29 na asilimia 76 ya watu wenye umri wa 30 – 39 wanamuunga mkono.

Huku asilimia 33 ya wananchi wenye umri wa miaka 18 – 29 na asilimia 30 ya wenye umri wa miaka 30 – 39 wanamuunga mkono Lowassa, tofauti na asilimia 15 ya watu wenye umri zaidi ya miaka 50.

Hata hivyo, utafiti huo ulibainisha kwamba kwa miaka minne mfululizo kuanzia mwaka 2012 hadi sasa, bado wananchi wana imani na CCM kwa asilimia kubwa ukilinganisha na vyama vingine.

Mchanganuo wa imani hiyo kwa wananchi kwenye nafasi ya udiwani hadi urais, wananchi wengi wameonesha bado wana mapenzi na CCM ingawa kuna kupungua kwa asilimia, ila bado vyama vingine havikuweza kukishinda.

Nafasi ya Urais mwaka 2015, CCM, imeonekana kuongoza kwa 66%, Chadema 22%, CUF 1% na nafasi za ubunge CCM imeonekana kuongoza kwa asilimia 60, Chadema 26%, CUF 3%, NCCR-Mageuzi na ACT- Wazalendo 1%.

Aidha, utafiti umebaini kuwa CCM inaungwa mkono kama ilivyokuwa miaka ya nyuma na kwamba Chadema ni chama cha pili kinachopendwa kushinda vyama vingine vya upinzani, ingawa wananchi wengi hawakukiunga mkono chama hicho kwenye nafasi mbalimbali za wagombea.

Kuhusu Ukawa Akizungumzia kuhusu Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Eyakuze alisema katika utafiti huo yapo maswali yaliyouliza iwapo wananchi wanaelewa maana ya Ukawa ni nini.

Katika majibu yao, utafiti huo ulibainisha kuwa asilimia 43 ya waliohojiwa walisema wanafahamu kwamba Ukawa ni chama cha siasa kilichosajiliwa Tanzania na asilimia 33, walisema hawafahamu kama ni chama cha siasa.

Aidha, asilimia 57 ya waliohojiwa walisema katika Uchaguzi Mkuu ujao, Ukawa itaonekana kwenye karatasi ya kupigia kura. “Hapa ndio kuna kazi ya kuelimisha wananchi kuwa Ukawa sio chama cha siasa na hakitakuwepo kwenye makaratasi ya kupigia kura,” alisisitiza Eyakuze.

Maoni kuhusu utafiti Baadhi ya wanachama wa vyama vya siasa na wanaharakati wamesema matokeo ya utafiti ni maoni na yanaweza kubadilika wakati wowote. Wamesema uchaguzi huu ni tofauti ukiwa mgumu na kuwa na mtikisiko wa kisiasa wenye ushindani ulio mkubwa.

Akitoa maoni yake baada ya kuzinduliwa kwa utafiti huo, Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Kitila Mkumbo alisema nusu ya wapiga kura wanaamini kuwa Ukawa ni chama cha siasa jambo ambalo sio sahihi huku vyama vya siasa vikitakiwa kutoa elimu zaidi kwa umma.

“Mseto wa vyama vya upinzani, Ukawa unajumuisha vyama vinne vya siasa ambapo uliundwa ili kuwawezesha wanachama kuingia katika uchaguzi huu wakiwa na Ilani moja na mgombea mmoja kutoka chama kimojawapo kwa kila jimbo,” alisema Dk Mkumbo ambaye pia ni mwanachama wa chama cha ACT - Wazalendo.

Alisema mseto huo haujasajiliwa kama chama cha siasa na jina la Ukawa halitokuwepo katika karatasi za kupigia kura na kuvitaka vyama kutoa elimu kuhusu hilo. Aidha, alisema utafiti huo ni maoni tu kutoka kwa wananchi sio matokeo halisi ya uchaguzi na kwamba tafiti za aina hiyo zipo duniani kote.

“Kwa mfano nchini Kenya, wakati wa uchaguzi ambapo moja ya utafiti uliofanyika humo kwa siku moja ulimtangaza Odinga (Raila) kuongoza na kesho yake kubadilika ukimtangaza Kenyatta (Uhuru) kuongoza,” alisema Mkumbo.

Aidha, alisema utafiti wa Twaweza ni wa 27 ambapo wamekuwa wakitoa tafiti zinazoheshimika na kwamba ni muhimu kujenga tabia ya kupinga tafiti kwa utafiti mwingine. Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Kampeni na Uchaguzi wa chama cha NCCR-Mageuzi, Faustine Sungura alidai matokeo ya utafiti huo yamepikwa na CCM kupitia kwa mawakala wao wanaofanya kazi katika taasisi hiyo ili kuhalalisha utafiti uliofanywa na chama hicho.

Mratibu wa Kitaifa wa Mtandao wa Asasi zisizo za Kiserikali za Haki za Binadamu Kusini mwa Afrika (SAHRINGON), Martina Kabisama alisema endapo Watanzania wangehojiwa leo, wangeweza kutoa majibu tofauti na yaliyotolewa na Twaweza kwa kuwa mwamko ni mkubwa zaidi wa kisiasa kadri siku zinavyosonga mbele.

Alisema matokeo hayo ndivyo utafiti unavyosema, lakini watu wanauelewa tofauti tofauti kuhusu uchaguzi wa mwaka huu na ilivyokuwa zamani.
Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link