Meneja wa Kampeni Jimbo la Mahonda Nd.Julius Suleiman Zakaria akiwanadi Balozi Seif Ali Iddi kulia yake anayewania kugombea nafasi ya Uwakilishi na Mh. Bahat Ali Abeid kushoto yake anayewania Ubunge Jimbo la Mahonda kwenye kampeni za uchaguzi za Jimbo hilo Hapo Tawi la CCM Kiom ba Mvua.
Nd. Julius Suleiman Zakaria akiwanadi Nd. Haji Fadhil Mkadam Kulia yake anayewania Udiwani Wadi ya Mahonda na Bibi Hadia Juma Chumu anayewania Udiwani Wadi ya Fujoni Kushoto yake kwenye kampeni za uchaguzi za Jimbo la Mahonda Hapo Tawi la CCM Kiom ba Mvua.
Mgombea Nafasi ya Ubunge Jimbo la Mahonda Bibi Bahati Ali Abeid Nassir akiahidi kuisimamia Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020 wakati akiomba kuchaguliwa kushika wadhifa huo kwenye kampeni za uchaguzi zinazoendelea nchini Kota.
Balozi Seif Ali Iddi akiahidi kuisimamia kikamilifu Suala la Elimu kwa lengo la kuwajengea maisha bora wananchi hasa Vijana wa Jimbo la Mahonda wakati akinadi sera za kutaka achaguliwa kushika wadhAfa huo hapo Kiomba Mvua Tawi la CCM.
Picha na – OMPR – ZNZ.
Picha na – OMPR – ZNZ.
Press Release:-
Wagombea nafasi za Uongozi Jimbo la Mahonda kupitia Chama cha Mapinduzi { CCM } wamesema endapo watapewa ridhaa na Wananchi kuliongoza Jimbo hilo katika kipindi cha Miaka mitano ijayo watakuwa tayari kushirikiana na Wananchi hao katika kutekeleza Ilani ya CCM yenye sifa zote zinazoweza kutekelezeka.
Wamesema Ilani hiyo imeainisha mambo mengi ya msingi kwa jamii ambayo wao wako tayari kuyasimamia kwa nguvu zao zote katika utekelezaji wake ili lile lengo la kuleta maisha bora kwa Umma lipatikane.
Viongozi hao Nd. Haji Fadhil Mkadamu anayewania nafasi ya Udiwani Wadi ya Mahonda, Bibi Hadia Juma Chumu Wadi na Fujoni, Bahati Ali Abeid Nassir Ubunge na Balozi Seif Ali Iddi Uwakilishi Jimbo Jipya la Mahonda walieleza hayo walipokuwa wakiomba ridhaa ya kuchaguliwa kushika nyadhifa hizo.
Wagombea hao walikuwa wakizungumza na Wananchi na Wanachama wa CCM wa Matawi Matano ya Mangapwani, Uwandani, Mkadini, Zingwezingwe na Fujoni hapo katika Tawi la CCM Kiomba Mvua Wilaya ya Kaskazini B.
Nd. Haji Fadhil Mkadam anayewania Udiwani Wadi ya Mahonda alisema kazi inayowakabili Wananchi na hsasa Vijana wa Jimbo la Mahonda ni kuhakikisha wanakijengea mazingira imara chama cha Mapinduzi ili kiendelee kuongoza Dola ya Watanzania.
Nd. Haji alisema CCM iliyotokana na mifupa ya Vyama vya TANU na ASP ndio yenye dhamira sahihi ya kuendelea kuyalinda Mapinduzi ya Zanzibar yaa Mwaka 1964 yaliyozaa Muungano wa Tanzania.
Naye Bibi Hadia Juma Chumu anayegombea Uduwani Wadi ya Fujoni alisisitiza na kuiasa Jamii kuelewa kwamba amani iliyopo Nchini ndio hazina inayoringia Tanzania hivi sasa na kuondoka kwake ni kuangamia kwa Mwanamke na Mtoto kama jamii zinavyoshuhudia wanawake wa Mataifa jirani wanavyodhalilika kwa kuchezewa amani yao.
Mh. Bahati Ali Abeid Nassir aliyeamua kuomba nafasi ya kuwania Ubunge Jimbo hilo la Mahonda alisema moja ya tatizo kubwa watakalolipa kipaumbele endapo watachagulkiwa kuliongoza Jimbo hilo ni kukabiliana na changamoto la Ajira linalowasumbua Wananchi hasa Vijana.
Alisema suala la ajira limekuwa ikiyakumba Mataifa mbali mbali Ulimwenguni yakiwemo pia yale yaliyoendelea kiviwanda. Hivyo Wananchi wanapaswa kuwa makini katika kuuepuka ushawishi unaoendelea kuenezwa na baadhi ya Wanasiasa kwa kuahidi kulifanya.
Mh. Bahati alisema kwa vile hakuna njia ya mkato katika kukabiliana na changamoto ya ajira yeye pamoja na Viongozi wenzake wameamua kujipanga vyema katika kuwakusanya Vijana katika vikundi vya ushirika ili wawapatie vifaa na zana zinakazowawezesha kuendeleza miradi ya kujitegemea kwenye mitaa yao.
Alifahamisha kwamba kwa vile Serikali Kuu inaendelea na kuimarisha miundo mbinu ya Sekta ya Kilimo katika miradi ya umwagiliaji Wananchi wanaweza kutumia maeneo madogo yaliyoimarishwa ili kuendeleza kilimo cha mboga mboga ambacho tayari kimeonyesha mafanikio makubwa.
Balozi Seif Ali Iddi anayewania nafasi ya Ujumbe wa Baraza la Wawakilishi katika Jimbo la Mahonda akimwaga sera zake alisema Elimu ni moja ya Mkakati utakaoimarishwa katika kuona skuli zote za Jimbo hilo zinakuwa katika mazingira rafiki.
Balozi Seif alisema juhudi aliyoichukuwa katika kuwatumikia Wananchi wa lililokuwa Jimbo la Kitope katika kipindi cha Miaka Kumi iliyopita ya Uongozi wake katika Jimbo hilo ataihamishia Jimbo jipya la Mahonda.
Aliwaahidi Wanafunzi wa Skuli zilizounda Jimbo la Mahonda wakae tayari kupokea huduma nzuri zitakazowajengea mazingira mazuri ya Kielimu likiwemo suala la vikalio, vifaa vya maabara sambamba na mfumo mpya wa mawasiliano ya Teknolojia ya Kisasa.
Akizungumzia sekta nyengine za Kijamii Balozi Seif ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwaeleza Wananchi hao wa Kiomba Mvua kwamba huduma za Maji safi na salama, Umeme na Afya zitaimarishwa mara dufu katika kuwaondoshea usumbufu Wananchi wake.
Alisema nguvu kubwa itachukuliwa katika kuona kila kijiji ndani ya Jimbo la Mahonda kinapata huduma muhimu za Maji safi na salama, Afya pamoja na Elimu jambo ambalo litawaondoshea kadhia watoto kufuata masomo katika maeneo ya mbali.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
23/9/2015.