Home » » Mwili wa Kombani kuwasili Dar leo

Mwili wa Kombani kuwasili Dar leo

Written By CCMdijitali on Friday, September 25, 2015 | September 25, 2015


Imeandikwa na Mwandishi Maalum - Habari Leo

MWILI wa aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Celina Kombani, unatarajiwa kuwasili jijini Dar es Salaam leo saa 9 alasiri kutoka nchini India, alikofariki wakati akipatiwa matibabu ya saratani.

Taarifa ya Ofisi ya Bunge iliyotumwa kwa vyombo vya habari jana, imeeleza kuwa mwili huo, utaletwa kwa ndege ya Shirika la Ndege la Emirates na kupokewa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Kombani anatarajiwa kuzikwa mkoani Morogoro katika shamba lake. Mipango ya mazishi imekuwa ikiendelea kufanywa na Serikali kwa kushirikiana na Ofisi ya Bunge na familia ya marehemu.

Rais Kikwete Wakati maandalizi ya kupokea mwili huo yakiwa tayari, Rais Jakaya Kikwete aliyepo safarini Marekani, amemtumia salamu za rambirambi Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kutokana na kifo cha Waziri Kombani.

“Pokea rambirambi zangu za dhati, sote kwa pamoja tumepoteza mama mchapakazi, hodari na aliyependa kushirikiana na wenzake katika kazi zake, hakika tutamkumbuka siku zote,” amesema Rais Kikwete katika salamu hizo.

Rais pia amemtumia salamu za pole mume wa marehemu Kombani, Swaleh Ahmad Pongolani, watoto, ndugu na jamaa wa Kombani. “Nimepokea taarifa za kifo cha mama Kombani kwa huzuni kubwa, najua machungu na maumivu mliyonayo kwa kuondokewa na kiungo muhimu katika familia yenu, poleni sana, mama ni nguzo ya familia, niko nanyi katika msiba huu mzito kwenu,” alisema Rais Kikwete.

Rais Kikwete alisema pamoja na kwamba kifo hakiepukiki, bado ni kitu ambacho kinashitua, kuhuzunisha na kuleta unyonge mkubwa kwa wafiwa katika jamii. “Naungana nanyi katika kipindi hiki kigumu kumuombea Mama Kombani ili Mwenyezi Mungu ampe mapumziko mema ya milele… Mwenyezi Mungu awatie nguvu, awape uvumilivu na subira katika kipindi hiki.”

“Niko nanyi katika kipindi hiki kigumu kwa hali na mali, nawaomba msijisikie wapweke,” alisema Rais na kuwatakia utulivu na amani katika kipindi hiki cha msiba mkubwa kwa familia ya Kombani.

Salamu za UWT Katika hatua nyingine, Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), umetoa salamu za rambirambi kwa ndugu, jamaa na Watanzania wote kwa kumpoteza Kombani.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa UWT, Amina Makilagi, umoja huo umepokea taarifa za kifo cha Kombani kwa mshituko mkubwa na kwamba ameacha pengo kubwa kutokana uhodari wake katika utendaji kazi. 

Amina akizungumzia kifo hicho jana, alisema UWT imepata pigo kubwa kwa kumpoteza kiongozi shupavu na mwenye msimamo katika utendaji wa kazi za serikali.

“UWT imempoteza kiongozi shupavu. Wanaulanga wamempoteza mtu muhimu ambaye alikuwa kimbilio la matatizo ya alipokuwa mbunge wa jimbo lao katika miaka mitano iliyopita. “Kwa Watanzania wamempoteza Waziri mchapa kazi asiyeyumba na mchango wake katika kuleta maendeleo hautasahaulika,” alisema.

Katibu mkuu huyo aliwaomba ndugu, jamaa, marafiki na Watanzania wote kuwa wavumilivu katika kipindiki hiki cha kuomboleza msiba wa mpendwa wao na kumuombea apumzike kwa amani. Kombani pia alikuwa mgombea ubunge wa Jimbo la Ulanga Mashariki mkoani Morogoro kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Amekuwa mbunge wa jimbo hilo kwa kipindi cha miaka 10 iliyopita. Historia yake Kombani alizaliwa Juni 19, 1959. Alifariki juzi Septemba 24, 2015 nchini India, ambako alikuwa anapatiwa matibabu baada ya kugundulika kuwa na saratani. Ameacha mume, watoto watano na wajukuu wanne.

Alisoma katika Shule ya Msingi Kwiro wilayani Ulanga mwaka 1968-1975 na Shule ya Sekondari Kilakala 1975-1978. Baadaye alisoma katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Tabora kwa masomo ya juu ya sekondari mwaka 1979-1981.

Baada ya masomo ya elimu ya sekondari, Kombani alijiunga na Chuo cha Maendeleo ya Uongozi Mzumbe (IDM Mzumbe) mwaka 1982-1985 na kati ya 1994-1995 alisomea Shahada ya Pili ya Uongozi katika Chuo hicho cha Mzumbe.

Kombani aliwahi kuwa Ofisa Utawala Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA)mkoani Morogoro, Meneja Kiwanda cha Ngozi Morogoro, Ofisa wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa mkoa wa Morogoro, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi) mwaka 2008-2010 na Waziri wa Katiba na Sheria. Mungu ailaze roho ya Kombani mahala pema peponi.
Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link