Balozi Mteule wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Balozi Hemed Iddi Mgaza kulia akisalimiana na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Ofisini Vuga Mjini Zanzibar alipofika kujitambulisha rasmi na kuaga baada ya kuteuliwa kushika wadhifa huo.
Balozi Hemed Iddi Mgaza akimuhakikishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kwenda kutekeleza vyema majukumu yake ya Kidiplomasia wakati atapowasili kwenye Kituo chake cha Kazi Nchini Saud Arabia.
Picha na – OMPR – ZNZ.
Picha na – OMPR – ZNZ.
Press Release:-
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeipongeza Serikali ya Mamlaka ya Saud Arabia kupitia Mfuko wake wa Misaada ya Maendeleo { Saud Fund } katika kuiunga mkono Zanzbar kwenye miradi ya Maendeleo katika Sekta ya Mawasiliano ya Bara bara.
Pongezi hizo zimetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati akizungumza na Balozi Mteule wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Nchini Saudi Arabia Balozi Hemed Iddi Mgaza aliyefika Ofisini kwake Vuga kuaga rasmi baada ya kuteuliwa rasmi kushika wadhifa .
Balozi Seif Ali Iddi alisema misaada ya Maendeleo inayotolewa na Serikali ya Saud Arabia imewezesha kukamilika kwa ujenzi wa Bara bara za Wete - Gando yenye urefu wa Kilomita 11.4 na Wete - Konde Kilomita 14.9 ambao umekifanya Kisiwa cha Pemba kufungua milango ya Kiuchumi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameelezea faraja yake kutokana na Nchi hiyo kuahidi tena kugharamia ujenzi wa Bara bara ya Chake chake - Wete yenye urefu wa Kilomita 22.1 kwa kushirikiana na Benki ya Kiarabu kwa Maendeleo ya Afrika { Badea } unaotarajiwa kutumia zaidi ya Dola za Kimarekani Milioni 11.9.
Alisema kwa vile Saudi Arabia imeonyesha kuendelea kuunga Mkono harakati za kiuchumi za Zanzibar na Tanzania kwa Ujumla alimuomba Balozi huyo Mteule wa Tanzania Nchini Saud Arabia Balozi Hemed Iddi Mgaza kupeleka salamu za shukrani kwa misaada hiyo.
Balozi Seif alifahamisha kwamba licha ya majukumu makubwa yatakayomkabili Balozi Hemed lakini lakini pia atakuwa na kazi ya ziada katika kuhakikisha kwamba Waumini wa Dini ya Kiislamu kutoka Tanzania wanatekelezea Ibada yao ya Hijja Nchinu humo katika hali ya amani na utulivu.
Alisema licha ya kwamba Wauimini hao wanasimamiwa na Vikundi mbali mbali vya kusafirisha Mahujaji lakini bado jukumu la Ofisi ya Kibalozi ya Tanzania iliyopo Nchini humo ina jukumu la kuhakikisha usalama wa Raia zake.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimuomba Balozi Hemed Iddi Mgaza kushajiisha Wawekezaji wa Saud Arabia kutumia fursa zilizopo Zanzibar za Uwekezaji kuanzisha miradi yao ya Kiuchumi kwa lengo la kuendelea kuimarisha uhusiano wa Kihistoria uliopo kati ya pande hizo mbili.
Balozi Seif alisema ni vyema shajiisho hilo likaenda sambamba na kuomba nyongeza zaidi za nafasi za masomo kwa Wanafunzi wa Zanzibar na Tanzania ili wapate fursa za elimu ya juu kwenye vyuo vikuu vya Nchi hiyo.
Alimpongeza Balozi Hemed Iddi Mgaza kwa kuteuliwa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Jakaya Mrisho Kikwete kushika wadhifa huo ukionyesha wazi uwezo alio nao katika kutekeleza jukumu katika Nyanja ya uhusiano na Diplomasia ya Kimataifa.
Naye Balozi Mteule wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Nchini Saud Arabia Balozi Hemed Iddi Mgaza alimuhakikishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba atatekeleza makujumu yake kadri ya uwezo na Taaluma aliyonayo.
Balozi Hemed aliahidi kwamba moja kati ya kazi yake kubwa ni kusimamia Uhusiano na ushirikiano wa Kihistoria ulioanzishwa kati ya waasisi wa Mataifa hayo mawili.
Mradi wa Ujenzi wa Bara bara za Wete – Konde na Wete – Gando ulioendeshwa na Kampuni ya Ujenzi ya Mecco na kuchukuwa kipindi cha Miezi 29 umegharimu Dola za Kimarekani Milioni 17,325,593.96 sawa na Shilingi za Kitanzania Milioni 23,389,551,848.75.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
12/9/2015.