Home » » Warioba afichua siri ya Ukawa

Warioba afichua siri ya Ukawa

Written By CCMdijitali on Friday, September 11, 2015 | September 11, 2015

 
Jaji Joseph Warioba akizungumza na maelfu ya wananchi katika Viwanja vya Mkendo Musoma Mjini jana


ALIYEKUWA Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba amefichua siri ya vyama vya upinzani vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), akisema vilikwamisha mchakato huo ili baadaye viingize vipengele vyao wakiingia madarakani.

Akizungumza na maelfu ya wananchi katika Viwanja vya Mkendo Musoma Mjini jana, Jaji Warioba alisema Katiba mpya imebeba mambo mengi mazuri kwa Watanzania na kwamba kutofautiana kwake na baadhi ya wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba Dodoma, kulitokana tu na vipengele vichache ambavyo visingeweza kusitisha mchakato mzima wa Katiba hiyo.

Aliongeza kwamba anashangaa ni kwa vipi vyama hivyo vyenye malengo tofauti kuhusu Katiba hiyo viunde Umoja kwa maslahi ya wananchi. Alisema kati ya vyama hivyo, kimoja kinataka kuundwe Serikali ya Mkataba huku kingine kikitaka Serikali tatu.

Alisema nia ya vyama hivi ilikuwa ni kutaka kukwamisha mchakato wa Katiba Mpya ili baada ya kushika madaraka viingize vile ambavyo vina maslahi kwao, ikiwemo ya kuvunja Muungano.

Alisema amezungumza na Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kukubaliana kuwa baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 mwaka huu, mjadala wa Katiba mpya uendelee.

Hatua hiyo alisema, imesababishwa na Ilani ya CCM ya 2015-2020, kujikita katika kuboresha maisha ya Mtanzania katika kuwasaidia kuanzisha na kuboresha shughuli zao za kujipatia kipato, kuboresha huduma za jamii na miundombinu na kupambana na ufisadi na kuacha kuzungumzia Katiba mpya.

Ilani hiyo haikugusia mchakato huo wa Katiba ambao ulipita hatua zote muhimu mpaka kupata Katiba Pendekezwa, na akibakiza kura ya maoni, huku Ukawa na baadhi ya wajumbe wa tume hiyo, wakitofautiana na Katiba hiyo kwa madai ya kutozingatia baadhi ya maoni ya wananchi.

Kupoteza uhalali

Akifafanua namna Ukawa ilivyopoteza uhalali, Jaji Warioba alisema kwanza katika suala la Muungano, kuna chama chenye msimamo wa kuwa na Muungano wa Mkataba, ambao alisema msimamo huo anaujua ni wa kuvunja Muungano.

Pili, alisema suala kubwa lililowasumbua wakati wa mchakato wa kutengeneza Rasimu ya Katiba, ni maadili na kufafanua kuwa Ukawa iliyojinasibu kutaka kutetea maadili, leo hii ghafla haiwezi tena hata kuzungumzia rushwa, ndio maana ameona wamejipotezea uhalali wa kutetea misingi ya maoni ya wananchi.

Uadilifu wa Magufuli

Kwa mujibu wa Warioba, wakati wa mchakato wa kumpata mgombea urais wa CCM, alikuwa na wasiwasi kama angepatikana mwenye maadili, lakini alipopatikana Dk John Magufuli, wasiwasi uliondoka kwa kuwa hana makundi, ameweza kuwaunganisha na ni muadilifu.

Akizungumzia uadilifu wa Dk Magufuli, Jaji Warioba alisema mwaka 1996, Rais Benjamin Mkapa alimteua kuongoza Tume ya Kero ya Rushwa ambapo walipofanya uchunguzi, walibaini katika ripoti yao wakaeleza kuwa rushwa kubwa na nyingi ipo katika ujenzi wa barabara.

Jaji Warioba alisema baada ya Dk Magufuli kuanza kusimamia Wizara ya Ujenzi, sasa ni miaka 15 hajasikia tena kelele za rushwa katika sekta hiyo, jambo lililomthibitishia kuwa mgombea huyo ni muadilifu.

Jaji Warioba akifafanua zaidi, alisema ameshangazwa kusikia baadhi ya makada wa Ukawa, wakiwemo waliowahi kuwa mawaziri wakuu, kusema kuwa katika miaka 54, Serikali haijafanya jambo lolote.

Alisema alipoingia sekondari, Shule ilikuwa ya Bwiru ikihudumia mikoa mitano, wakati leo kila kata ina shule moja ya sekondari na wakati huo hakukua na chuo kikuu lakini leo viko vingi. Kuhusu afya, alisema Tanzania ya leo hospitali zinafanya upasuaji wa moyo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na Hospitali ya Rufaa ya Bugando, matibabu ambayo yalikuwa yakifanyika nje ya nchi tu.

Alisema hata Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2015-2020, imeitaka Serikali kununua mashine ya upasuaji wa kichwa, ambayo haipo na kuhoji hayo si mafanikio? Katika sekta ya maji, Jaji Warioba alisema maji yamevutwa kutoka Ziwa Victoria mpaka Shinyanga na sasa yanatarajiwa kwenda Nzega mpaka Tabora, na kuendelea kuhoji hayo si maendeleo?

Alikwenda mbali zaidi na kuhoji amani ya miaka 54 si maendeleo na kutaka wnaopinga hilo, waeleze ni nchi gani iliyokaa kwa miaka 54 na amani kati ya nchi zinazoizunguka Tanzania.

Wanaokana maendeleo

Jaji Warioba alisema anachoshangaa ni baadhi ya watu waliosimamia maendeleo hayo walipokuwa mawaziri wakuu, kudai kuwa hakuna kilichofanyika katika miaka 54, wakati walitoa taarifa ya mafanikio ya utendaji wao ya kila mwaka na kurekodiwa bungeni.

Alisema viongozi hao waliohama CCM na kuingia Ukawa, wamekuwa wakisema uongo na kukana hata mafanikio waliyosimamia wenyewe.

Naye Joseph Lugendo anaripoti kuwa Magufuli, akihutubia umati katika eneo la Nyamongo mkoani Mara jana kwenye mgodi wa dhahabu wa North Mara alisema katika maeneo yenye migodi na ujumbe wa kuweka hesabu sawa, kila kinachochimbwa kijulikane na faida ya mwekezaji na kinachobakia viwe wazi.

Alisema anawapenda wawekezaji na anawakaribisha waje kuwekeza ili kutoa ajira, lakini akasema hawaji kutoa zawadi bali kufanya biashara. Huku akitumia mfano wa mwenye duka na muuzaji, Dk Magufuli amesema mwenye duka lazima ajue bidhaa zake, mapato yake na faida inayopatikana, la sivyo atajikuta duka jeupe.

“Hii migodi tumepewa na Mungu, ndio maana hawa wamekuja… hawajaja kutupa zawadi wamekuja kufanya biashara sasa tutataka hesabu tujue kila kitu kinachotoka mgodini,” alisema.

Kuhusu watumishi wa umma, Dk Magufuli alisema Serikali atakayoiongoza itajali kazi zaidi na hivyo mtumishi wa umma atakayeharibu kazi, hakuna kuhamishwa, ataondoka moja kwa moja.

Imeandikwa na Waandishi Wetu, Musoma - Habari Leo
Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link