Kiongozi wa ACT - Wazalendo, Zitto Kabwe. |
Imeandikwa na Halima Mlacha, Pangani.
MGOMBEA Mwenza wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan, amevunja ngome ya upinzani mkoani Tanga, baada ya kuzoa wanachama zaidi ya 600 kutoka upinzani wakiwemo wagombea udiwani watano kutoka chama cha ACT - Wazalendo.
Wanachama hao waliamua kujiunga na chama hicho tawala wakati wa mikutano mbalimbali ya kampeni ya Mgombea Mwenza huyo mkoani Tanga. Katika mkutano uliofanyika Usagara jijini Tanga, mgombea huyo aliwapokea wagombea udiwani hao ambao walipokea rasmi kadi mpya za CCM.
Wagombea hao wa ACT ni Wilson Elia (wa Kata ya Duga), Gasper Maboko (Kata ya Nguvumali), Charles Luanda (Maweni), Mary Scott (Kata ya Tanga Sisi) pamoja na Sada Mbwambo (Viti Maalumu).
Aidha, katika mikutano hiyo, pamoja na wagombea udiwani hao, takribani wanachama 561 kutoka vyama vya ACT, CUF na Chadema walijiunga na chama hicho tawala. Wanachama hao walijiunga katika mikutano ya kampeni ya Samia iliyofanyika Usagara, Muheza, Korogwe Mjini na Pongwe mkoani Tanga.
Katika mkutano wa Korogwe Mjini, Mwenyekiti wa Kata ya Mswaha kutoka CUF akifuatana na wanachama 280 kutoka chama hicho na Mwenyekiti wa Chadema kutoka Kata ya Chagunda walijiunga na CCM.