Baadhi ya wana CCM na wananchi wa Jimbo la Uzini wakiwa katika Mkutano wa uzinduzi wa Kampeni za Uchaguzi za Jimbo hilo zilizofanyika katika uwanja wa Michezo wa Kiboje Muembe Shauri.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kampeni ya CCM Balozi Seif Ali Iddi akimnadi mgombe nafasi ya Ubunge wa Jimbo la Uzini kwa Tiketi ya Chama hicho Ndugu Salum Rehani wakati wa uzinduzi wa Kampeni za uchaguzi za Jimbo hilo.
Balozi Seif akimnadi kwa wapiga kura Ndugu Moh’d Raza Hassanali anayewanifa nafasi ya Ujumbe wa Baraza la Wawakilishi Jimbo la Uzini liliopo Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja.
Balozi Seif akiwanadi wagombea wa nafasi za Udiwani wadi zilizomo ndani ya Jimbo la Uzini wakati akizindua rasmi Kampeni za Uchaguzi za Jimbo hilo.
Kushoto ya Balozi Seif ni Bibi Khaina Ali Makame anagombea Wadsi ya Kiboje, Kulia ya Balozi Seif ni Nd. Victor Fabian anayegombea Udiwani Wadi ya Koani na Nd. Rashid Abass Othman Udiwani Wadi ya Bambi.
Press Release:-
Mwenyekiti wa Kamati ya Taifa ya Kampeni ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amewatahadharisha Wana CCM na Wananchi kuwa na tahadhari na baadhi ya watu walioamua kupita mitaani kununua Vitambulisho vya kupigia kura.
Alisema mpango huo umelenga kupunguza asilimia kubwa ya ushindi wa Chama cha Mapinduzi kwenye uchaguzi Mkuu ujao wa mwezi Oktoba ambao uko wazi kutokana na utekelezaji makini wa Sera na Ilani yake ya mwaka 2010 – 2015 iliyoleta maendeleo makubwa ya Kiuchumi na Kijamii Nchini Tanzania.
Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati akizungumza na Wana CCM na Wananchi wa Jimbo la Uzini akiizindua rasmi Kampeni za Uchguzi za Jimbo hilo hapo katika uwanja wa michezo wa Kiboje Muembe Shauri Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja.
Alisema Viongozi pamoja na wafuasi wa Vyama vya Upinzani Nchini tayari wameshabaini kwamba nguvu ya ushindi wa CCM Kwenye uchaguzi Mkuu ujao wa mwezi huu inatisha kasi ambayo inavijengea mazingira ya kifo vyama hivyo kwa kukosa uhimili wa kuungwa mkono na wananchi walio wengi.
Balozi Seif ambae pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliendelea kuwatoa hofu Wananchi hasa wale wenye asili ya Tanzania Bara kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia vyombo vyake vya Dola itakuwa makini katika kulinda usalama wao.
Alisema cheche ya baadhi ya watu kujaribu kujiandaa kutaka kufanya fujo kabla na baada ya uchaguzi zimetambuliwa licha ya baadhi ya viongozi wa Upinzani kutafuta mbinu za kukanusha mpango huo wa hatari.
Aliwakumbusha Wananchi na Wana CCM wote kujitokeza kwa wingi Tarehe 25 Mwezi huu katika kupiga kura na kuwachagua wagombea wote wa Chama Tawala cha CCM.
Balozi Seif aliwaomba wananchi hao kurejea nyumbani mara wanalizapo zoezi hilo ili kulinda amani ya nchi pamoja na kusaidia kuepusha ile shari ambayo tayari baadhi ya watu wametia nia ya kuianzisha kipindi hicho.
Mapema Mwenyekikti wa CCM Jimbo la Uzini Ndugu Haji Shaaban alisema watu wanaoeneza uzushi kuwa hakuna Maendeleo Zanzibar wanastahiki kuzomewa kwani ushahidi wa huduma za kijamii kama Maji safi na salama, umeme na Bara bara ndani ya kipindi cha miaka 50 upo wazi.
Nd. Shaaban alisema miaka 100 ya utawala wa Kikoloni wazee walishuhudia madhila, ugaguzi na ukosefu wa maendeleo ambayo yale finyu yaliyokuwepo yaliyolenga zaidi kwa watawala hasa mji Mkongwe.
Katika Mkutano huo wa uzinduzi wa Kampeni ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi Jimbo la Uzini Balozi Seif aliwanadi wagombea nafasi mbali mbali za Uongozi wa Jimbo hilo kupitia CCM.
Wagombea hao ni Nd. Salum Reheni anayegombea Nafasi ya Ubunge, Nd. Moh’d Raza Hassanali nafasi ya Ujumbe wa Baraza la Wawakilishi, Bibi Khania Ali Makame nafsi ya Udiwani Wadi ya Kiboje, Nd.Rashid Abass Othman Udiwani Wadi ya Bambi na Nd.Victor Fabian Udiwani Wadi ya Koani.
Wakiomba kura kwa Wana CCM na Wananchi wa Jimbo hilo la Uzini Wagombea hao wameahidi kusimamia vyema Sera na Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya Mwaka 2015 – 2020 ambayo wana uwezo nayo katika kuwaletea maendeleo Wananchi wa Jimbo la Uzini.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
1/10/2015.
Picha na –OMPR – ZNZ.