Home » » Tigo yakabidhi Halmashauri ya Wilaya ya Kaskazini “B” Vifaa vya Maabara

Tigo yakabidhi Halmashauri ya Wilaya ya Kaskazini “B” Vifaa vya Maabara

Written By CCMdijitali on Friday, October 2, 2015 | October 02, 2015

 Uongozi wa Kampuni ya simu za Mkononi ya Tigo ukikabidhi vifaa vya Maabara kwa Halmashauri ya Wilaya ya Kaskazini “B” vilivyotolewa msaada kwa ajili ya Skuli ya Sekondari ya Fujoni
iliyomo ndani ya Wilaya hiyo.

Kutoka kulia ni Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Sekondari ya Fujoni Mwalimu Mbarouk Ishak Daima,Mwakilishi wa Kampuni ya Tigo Bibi Sylvia Balwire, Meneja Uhusiano wa Tigo Bibi Halima Okash pamoja na Mkurugenzi waq Halmashauri ya Wilaya ya Kaskazini B Ndugu Hassan Ali
Kombo.

Aliyesimama nyuma yao ni Mbunge anayemaliza muda wake wa Jimbo la Kitope ambaye pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi.

Mwakilishi wa Kampuni ya mtandao wa mawasiliano ya simu za Mkononi wa Tigo Bibi Sylvia Bwalwire aliyepo kati kati akielezea msimamo wa Kampuni yake kusaidia huduma za jamii hapa
Nchini.

Kulia ya Bibi Sylvia Balwire ni Balozi Seif Ali Iddi, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kaskazini “B” ambao kushoto ya Bibi Sylvia ni Meneja Uhusiano wa Tigo Bibi Halima Okashi na Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Sekondari ya Fujoni Mwalimu Mbarouk Ishak Daima.
Picha na –OMPR – ZNZ.

 Press Release:-

Baadhi ya Halmashauri za Wilaya hapa nchini zinaendelea kufanya
jitihada katika kuimarisha miundo mbinu kwenye masomo ya Sayansi kwa lengo la kuwawezesha Wanafunzi wa Skuli za Sekondari kupata taaluma inayokwenda sambamba na 
mabadiliko ya sayansi na teknolijia Duniani .

Juhudi zilizochukuliwa na Halmashauri ya Wilaya ya Kaskazini “B” Mkoa wa Kaskazini Unguja kwa kushirikiana na Mbunge anayemaliza muda wake wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi hatimae zimezaa matunda yaliyosaidia Skuli ya Sekondari ya Fujoni Wilayani humo kupata vifaa vya Maabara .

Kampuni ya mtandao wa Mawasiliano ya simu za Mkononi ya Tigo
imeikabidhi Halmashauri ya Wilaya ya Kaskazini “B” Vifaa vya Maabara vyenye Thamani ya ya zaidi ya shilingi Milioni 20,000,000/- kwa ajili ya Skuli ya Sekondari ya Fujoni iliyomo ndani ya Jimbo Jipya la Mahonda.

Hafla hiyo fupi iliyoshuhudiwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ambae pia ni mgombea Uwakilishi wa Jimbo la Mahonda Balozi Seif Ali Iddi ilifanyika Nyumbani kwake Mtaa wa Kama Wilaya ya Magharibi “A ”.

Akikabidhi vifaa hivyo vya Maabara kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kaskazini “ B” Ndugu Hassan Ali Kombo Mwakilishi wa Kampuni ya Simu za Mkononi ya Tigo Bibi Sylvia Balwire aliishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuwajengea mazingira bora wawekezaji wanaoamua kuwekeza miradi yao ya kiuchumi Nchini.

Bibi Sylvia alisema taasisi yake ya Mtandao wa mawasiliano ambayo imekuwa ikitoa huduma za mawasiliano Nchi nzima imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuendesha biashara na faida inayopatikana huelekezwa katika kusaidia miradi ya Kijamii kama elimu, afya na maji safi na salama.

Akipokea msaada huo wa vifaa vya Maabara, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kaskazini “ B ” Ndugu Hassan Ali Kombo alieleza kwamba anaamini msaada huo uliofika kwa wakati utaimarisha fani ya sayansi kwa wanafunzi wa Wilaya hiyo.

Ndugu Hassan alisema upungufu wa vifaa vya maabara uliozikumba skuli nyingi za Sekondani Nchini umepelekea Serikali za Wilaya kupitia Halmashauri zake kutafuta mbinu na kuweka mikakati za kutanzua changamoto hiyo.

Alisema Uongozi wa Halmashauri hiyo ulilazimika kufanya juhudi za kutafuta msukumo na msaada kutoka kwa wafadhili na washirika wa Maendeleo katika kuunga mkono Sekta ya Elimu inayobeba nguvu ya maendeleo ya Taifa lolote.

Akitoa shukrani zake Mbunge anayemaliza muda wake wa utumishi wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema Serikali itaendelea kuimarisha miundo mbinu ya uwekezaji ili kuwajengea mazingira ya uhakika wawekezaji wanaoamua kuwekeza miradi yao hapa Zanzibar.

Balozi Seif ameipongeza Kampuni ya Simu za Mkononi ya 
Tigo kwa uamuzi
wake wa kusaidia sekta ya Elimu katika skuli iliyoonyesha 
juhudi kubwa katika kuimarisha masomo ya sayansi ambayo
 ndio yenye soko kubwa la ajira kwa hivi sasa.

Alisema Skuli ya Sekondari ya Fujoni imeweka historia kubwa ndani ya Wilaya ya Kaskazi “B ” kwa kuimarisha masomo ya sayansi kiasi kwamba Halmashauri ya Wilaya hiyo ikalazimika kuiunga mkono katika kusaidia
kukabiliana na changamoto zinazoikabili skuli hiyo.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
2/10/2015.
Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link